KILIMO: Jinsi ya kutengeneza mbolea vunde
Na SAMMY WAWERU
ALIPOANZA kilimo mwaka 2011, kila msimu David Karira hakukosa kukadiria hasara iliyotokana na athari za magonjwa na wadudu.
Kwa kuwa anathamini kilimo asilia, Bw Karira alitumia mbolea ya mifugo hususan ng’ombe, mbuzi na kuku, kukuza pilipili mboga na matunda damu maarufu kama tree tomato au tomarillo.
“Nimewekeza katika ufugaji wa kuku, mbuzi na ng’ombe, nilikuwa nikikusanya kinyesi chao na kukipeleka moja kwa moja hadi shambani kama mbolea,” anaelezea mkulima huyu wa Mathira, Nyeri.
Matunda damu ameyapanda eneo tambarare na yaliyotangamana na mikahawa. Pilipili mboga anazikuza kwenye kifungulio, green house.
Bw Karira anasema magonjwa na wadudu walikuwa marafiki wa chanda na pete kwa mimea na mazao yake.
“Sikujua shida ilitokana na mbolea niliyotumia kuzalisha mazao, niliyoitoa maboma ya mifugo wangu na kuitumia moja kwa moja pasi kuipa muda iive sawasawa,” anasema.
Lawrence Ngugi, mtaalamu wa kilimo kutoka kampuni ya Hygrotech, anasema mkulima asipokuwa makini katika utumizi wa mbolea ya mifugo hataepuka mjeledi wa mimea na mazao kushambuliwa na wadudu na magonjwa.
Anadokeza kwamba mbolea ambayo haijapewa muda kuiva barabara (decompose) ni mlo wa wadudu, kando na rimota ya kusambaza magonjwa.
“Unapotazama kwa makini samadi ya mifugo au kinyesi cha kuku hutakosa kuona wadudu. Chakula cha mifugo ni mimea, ambayo mingine ina magonjwa. Hivyo basi, ukitumia mbolea kabla haijaiva, athari zake utazielekeza kwenye udongo,” anatahadharisha.
Kulingana na mtaalamu huyu, wadudu na magonjwa hujificha udongoni na ndiposa mkulima ataishia kulalamika kila wakati kwamba shamba lake ‘limerogwa’.
“Halijagangwa, wewe ndiye umeliroga. Ipe mbolea muda iive ili kuua wadudu na magonjwa yaliyomo,” anahamasisha Bw Ngugi.
Bw Timothy Mburu, mkulima wa viazi mbatata, kabichi na vitunguu Nyeri anasema ameepuka changamoto hizo kwa kujitengenezea mbolea.
Kuchanganya
Yeye hujiundia mbolea mboji kwa jina jingine vunde, maarufu mbolea hai kwa kuchanganya ile ya mifugo na majani ya mimea.
Baada ya kuvuna mboga, mahindi, viazi, vitunguu na maharagwe, mkulima huyu hutumia majani yaliyosilia kutengeneza mbolea hii. Majani ya miti, pia hutumika.
“Mbolea hai (compost manure), huitengeneza kwa kukusanya samadi ya mifugo; ng’ombe, mbuzi na kuku, ambapo huichanganya na majani, kisha mkusanyiko huo ninaufunika kwa karatasi kubwa ya nailoni na kuupa muda uive,” anaelezea Bw Mburu.
Kulingana naye ni kwamba hufunikwa kiasi cha kutoruhusu hewa au maji kuingia, na baada karibu miezi sita huwa tayari kwa shughuli za upanzi.
Anadokeza kuwa muda huo endapo kuna wadudu huangamia, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uwezekano wa kuwepo kwa magonjwa yanayosambazwa na samadi. “Mbolea ya aina hii ni salama dhidi ya magonjwa na wadudu,” Mburu asisitiza.
Ni mfumo asilia ambao hudumisha rutuba ya udongo pamoja na kuendeleza azma ya kilimo hai. Kilimo cha aina hii huepushia mkulima mazoea ya kupulizia mimea au mazao dawa kudhibiti wadudu na magonjwa.
“Mkulima afahamu wazi changamoto ibuka; magonjwa na wadudu hujiri kuanzia hatua za kwanza katika upanzi. Ni busara kuwa na msingi bora utakaozalisha mazao bora na salama,” ashauri Mburu ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo.