KILIMO: Miparachichi ya kupandikiza inayozaa ajabu
Na CHRIS ADUNGO
KILIMO ni njia moja ambayo kila nchi inayojali maendeleo inawekeza kwacho kwa wingi ili kuimarisha uchumi wake.
Nchi kama vile Marekani, China, India na Brazil zimeongoza kwa kuzalisha chakula kingi sana duniani.
Kilimo ambacho kinaongoza nchini ni cha majanichai, kahawa, maua na matunda. Kilimo cha parachichi katika miaka ya hivi majuzi kimeonekana kupata mashiko na wakulima wengi wamejitosa katika kilimo hiki cha ukuzaji wa matunda hayo.
Maeneo ambayo miparachichi inakuzwa kwa wingi hapa nchini ni Nyeri, Kisii, Nyamira, Kiambu, Embu, Muranga, Meru, Tharaka Nithi na Kirinyaga. Zao hili la miparachichi huwa linanawiri vizuri katika maeneo yaliyo na baridi na mvua nyingi.
Katika Kaunti ya Kirinyaga, eneo la Mururi eneobunge la Gichugu, tunakutana naye kijana John Maina ambaye ni meneja wa kampuni ya Aberdare Technology tawi la Kirinyaga linalokuza na kuuza miche ya parachichi kwa wakulima.
Kampuni hii ina makao yake makuu katika Kaunti ya Murang’a na inajihusisha na ukuzaji wa miche ya ndizi, parachichi, mapapai, machungwa na maembe; mengi yakiwa ni ya kupandikizwa.
Tawi jingine nchini la kampuni hii liko katika Kaunti ya Kisii. Bw Maina mwenye umri wa miaka 32 amekuwa akisimamia shughuli zote za uzalishaji wa maparachichi katika kituo hiki kutoka mwaka wa 2015.
Hapa huwa anahakikisha kazi ya kupanda, kutunza na kuuza bidhaa hizi zinaendelea kwa njia nzuri. Bw Maina anasema kwamba mbegu wanazozipanda ni za kienyeji ambazo huwa zinatolewa katika maeneo ya kutupa takataka haswa jijini Nairobi.
Katika sehemu ya robo ekari ya shamba katika kituo hiki, huwa wanapanda mbegu 10,000 kila msimu ambazo kabla ya kupandwa, huwa wanazitibu ili kuzuia magonjwa yanayofanikiwa kutokana na mchanga.
Katika shughuli za upanzi, Bw Maina huwa anaajiri wafanyakazi ambao huwa wanatia mchanga na mbolea ya mbuzi katika mifuko ya vijikaratasi kisha kuweka mbegu. Baada ya hapo, kazi huwa ni kunyunyizia maji kila siku na kwa kawaida miparachichi huchukua mwezi mmoja ili kuweza kukua.
Kulingana na Maina, huwa wanaanza kupandikiza miche hii baada ya miezi miwili kutoka siku ya upanzi. Madhumuni ya upandikizi ni kupata aina mwafaka ya parachichi wanazozitaka na zenye usawa wa kufanana. Kwa kawaida, wana aina mbili za parachichi wanazokuza ambazo ni ‘Hass’ na ‘Fuerte’. Maina anasema aina hizi mbili ndizo zinahitajika sokoni kwa wingi.
“Lengo hasa la kufanya upandikizi ni kuhakikisha ya kuwa aina sawa ya parachichi imepatikana na zaidi ni kupunguza muda wa parachichi kukua na kukomaa,” Maina anaelezea.
Wateja wake wengi anasema ni wapita-njia katika Barabara Kuu ya Nairobi kuelekea Meru, vikundi vya wakulima kutoka eneo la Kirinyaga, Embu, Tharaka Nithi na Meru.
Pia wana ushirikiano na Kaunti ya Kirinyaga na Tharaka-Nithi ambako serikali za kaunti hizo huwa zinasimamia masomo ya wakulima katika kituo hiki na pia kuwauzia miche. Katika misimu ya mvua, huwa wanauza miche mingi ya parachichi ikilinganishwa na misimu mingine katika mwaka.
Anasema kwamba kila mwaka wana uwezo wa kuuza miche 10,000 na ambapo huwa wanauza Sh150 kwa kila mche moja.
Ina maana kwamba kwa kipindi cha miezi 12, Maina hujivunia zaidi ya Sh1.5 milioni. Maji ya kunyunyizia mimea yake huwa anatoa kwenye kijito kinachopitia karibu, lakini anasema huwa anapata changamoto ya ukosefu wa maji wakati wa kiangazi kwani maji hayo huwa yanapungua ama kukosekana kabisa.
Ombi lake kuu kwa serikali kuu na vile vile ya Kaunti ya Kirinyaga ni kuelimisha wakulima ili waweze kupata ujuzi zaidi katika kilimo hiki ili walime zaidi.
Pia maji ya mifereji isambazwe kote ili kuwezesha wakulima hawa kufanya kilimo cha unyunyiziaji jambo ambalo litahakikisha ubora wa mazao yao. La mno ambalo Maina anasema ni kwamba serikali hizi ziwe mstari wa mbele kuwatafutia wakulima masoko zaidi, ya hapa nchini na ya kimataifa vilevile. Hili lina umuhimu maanake wakulima watapata motisha ya kuzamia kilimo zaidi.