• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
KILIMO NA UCHUMI: Mateso aliyopata mjini yalimfanya arejee kijijini anakovumishia kilimo cha mboga sasa

KILIMO NA UCHUMI: Mateso aliyopata mjini yalimfanya arejee kijijini anakovumishia kilimo cha mboga sasa

Na GRACE KARANJA

KWA wakati mmoja, Monicah Muthoni alifikiri kuwa kusaka kazi mijini kungemfaidi lakini rafiki yake alimwonya kwamba angechukua muda mrefu kabla ya kuajiriwa.

Hata hivyo, alipuuza hayo na kufunga safari kuelekea Nairobi.

Mateso aliyokumbana nayo kwa muda wa miezi sita yalimfanya kurejea nyumbani. Wazo la kuanzisha kilimo cha mboga lilimjia na bila kupoteza muda alijitosa katika shamba lake la nusu ekari.

Japo hakujua hasa alichotaka kulima, alianza kwa kulima sukumawiki kabla ya kuanza kulima spinachi.

“Maisha yalivyoendelea kunilemea ilinibidi nirejee nyumbani kuanza kwani kazi nilizoahidiwa mjini Nairobi zilikuwa hewa tu, sikuzipata. Hapo nikaamua kuanza kilimo ingawaje nilidharau ardhi yangu ya nusu ekari,” anaeleza mkazi huyu wa Nyandarua.

Anasema kwamba kilimobiashara cha sukumawiki ni njia mojawapo ya kujiinua kimaisha lakini wengi hawana ari kwa sababu wengine husema sukumawiki haina pesa.

Anaeleza njia rahisi za kupanda mboga hizi za sukumawiki na spinachi hasa wakulima wanaoishi maeneo yanayopokea jua kali ni kwa kutumia mfumo wa unyunyiziaji maji kwa njia ya matone maarufu kama drip irrigation lakini ikiwa mkulima yuko katika maeneo ambayo yana hali ya hewa nzuri kwa kilimo cha mboga, haina haja kwa kuwa mboga hukua vizuri bila kumwagiliwa maji.

Hata hivyo, anasema ipo haja ya wakulima kupata ujuzi wa kilimo kabla ya kupanda ili kuokoa muda wa mawazo na mwishowe kupata hasara.

“Hakuna haja ya wakulima hasa wale wanaanza kilimo kujisumbua kwa mawazo shambani ilhali wataalam wa kilimo ni wengi,” anasema.

Anatoa changamoto kwa serikali kuongeza taasisi za kilimo ili vijana wanusuriwe kutoka mikononi mwa mwa wahalifu pamoja na janga la ukosefu wa ajira nchini.

Udogo wa kipande cha ardhi

Anasema kwamba yeye hupenda kilimomseto ambapo anapanda sukumawiki na spinachi lakini hubadilisha mazao kwa kuwa kipande chake cha ardhi ni kidogo.

Changamoto anayokumbana nayo ni wakati wa kuuza mazao yake kwani madalali ambao hufika kutoka mijini huwandanganya kuhusu bei zilizoko.

“Sisi wakulima hofu yetu ni madadli tu ambao huvuna wasipopanda. Wao ndio hujua wakati mazao yetu yanakomaa na kula jasho letu. Hii ina maana kuwa mkulima ambaye anashibisha taifa lake kwa jasho lake hapati faida ni ini. Siku hizi madalali hata wamekuwa wengi kuliko wakulima na serikali yetu tu imenyamazia suala hili,” anaeleza kwa uchugu mkulima huyu wa mboga.

Licha ya changamoto hii na nyinginezo, kama vile za ukosefu wa pesa za kulima, anasema ameshuhudia matunda yanayotokana na kilimo cha aina za mboga akisema ni pesa ambazo zinahitaji subira ambayo amejifunza kuwa nayo.

Maradhi ya baridi humsumbua sana Muthoni lakini anahofia kuwa mbolea zinazotengenezwa viwadani hudhoofisha afya ya wateja wake ambao wanasusia kunua mboga. Hivyo hana budi kutumia mbolea za mifugo kila anapopanda.

You can share this post!

UFUGAJI WA FAIDA: Mbuzi kwake kimbilio akitaja bei nzuri ya...

KIU YA UFANISI: Aliona washonaji nguo ni wengi, akaamua...

adminleo