• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:55 AM
KILIMO: Namna ya kutunza miche kitaluni kabla kuihamishia shambani

KILIMO: Namna ya kutunza miche kitaluni kabla kuihamishia shambani

Na SAMMY WAWERU

UTHABITI wa miche ni miongoni mwa vigezo muhimu kutilia maanani ili kustawisha mimea inayozalishwa kutoka kwayo.

Mazao kadhaa kama ya mboga, nyanya, viazi, vitunguu, matunda, na mengineyo, huzalishwa kwa mimea iliyopandwa kutoka kwa miche.

Mbali na uhalisia wa pembejeo kama mbolea na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu, wadau katika sekta ya kilimo wanahoji udhabiti wa miche pia unategemea mbegu.

“Kuna mbegu nyingi sana bandia sokoni, na ni baadhi ya changamoto zinazomzingira mkulima. Mimea inayopandwa kutokana na miche inapaswa kuwa na mbegu bora ili kupata mazao bora na ya kuridhisha,” anaeleza Emmah Mwenda, mtaalamu.

Kando na uhalisia wa mbegu, cha msingi zaidi ni itunzavyo miche inapochipuka.

Athari nyingi za wadudu na magonjwa kwenye mimea na mazao hutokana na miche. Endapo changamoto hizo hazitakabiliwa ipasavyo, kuna uwezekano zitasambazwa kwenye mimea na mazao.

Bi Mwenda anapendekeza kitalu-eneo maalum kukuzia miche, kiwe katika mahali salama. “Ikiwezekana kiwe eneo ambapo upepo umedhibitiwa kwani ni kiini kikuu katika usambazaji wa wadudu na magonjwa,” anasema.

Anaendelea kueleza kwamba eneo lililochaguliwa lizingirwe ili kuzuia uharibifu wa mifugo na ndege.

“Mkulima akishapanda mbegu, afunike kitalu kwa chandarua au nyasi za boji zilizokauka,” anashauri Emma, ambaye ni mtaalamu kutoka HM. Clause, kampuni ya kuunda mbegu za mboga, nyanya, na pilipili mboga.

Miche ni mimea michanga inayohitaji umakinifu wa hali ya juu na inapochipuka, nyasi zile ziondolewe.

Ili kudumisha mfumo wa kilimo, Bw Simon Wagura, mtaalamu wa kilimo na mwasisi wa The Country Farm, shirika linaloangazia upanzi, utunzaji na uzalishaji wa mimea na wanyama, anapendekeza kuzingatia mbinu asilia kudhibiti wadudu na magonjwa.

“Udhibiti wa upepo kwa kuzingira kitalu ni njia bora kukabili changamoto hizo ibuka. Pia, kabla ya kuandaa kitalu hakikisha udongo ni salama. Mbolea ,” anasema Bw Wagura.

Hata hivyo, anasema dawa zisizo na kemikali (organic foliar) zimaweza kutumika.

Ufanisi katika kilimo chochote kile unategemea kuwepo kwa maji. Ni kiungo muhimu kwa miche ambapo inapaswa kumwagiliwa asubuhi na jioni, msimu wa jua kali au kiangazi.

Wagura anashauri kitalu kiandaliwe mahali ambapo miale ya jua itaweza kufikia miale. Miche ya mimea mingi huchukua muda wa karibu wiki nne, sawa na mwezi mmoja.

Wakati miche ikiendelea kukua, mkulima anashauriwa kuandaa eneo la upanzi. Kulingana na Bw Wagura, inapaswa kuhamishwa majira ya jioni au asubuhi na mapema, wakati miale ya jua si kali.

“Kitalu kimwagiliwe maji saa chache kabla ya kung’oa miche,” anashauri mdau huyu.

Aidha, miche inayopaswa kung’olewa ni ile ndefu na yenye nguvu.

Uangalifu

Kulingana na Samuel Mwaniki, mkulima wa nyanya, mboga, vitunguu na maharagwe ya Kifaransa Joska, eneo la Kamulu, Machakos, ni kwamba mkulima anapaswa kuwa mwangalifu anapong’oa miche kwani ni michanga.

Mkulima huyu anasema inafaa kung’olewa ikiwa na udongo kiasi, ili kuiwezesha kushika kai upesi inapopandwa.

Bw Mwaniki anasema kinachofisha miche mingi ni kutozingatia hili, ambapo huipa miche wakati mgumu kuelewa ‘mazingira mageni’.

“Kumbuka uhamisho wake kutoka kitaluni hadi shambani huipa mzongo wa mawazo, hivyo basi inapaswa kusalia na udongo kiasi na kubebwa kwa umakinifu,” anafafanua kauli inayotiliwa mkazo na Bw Timothy Mburu mkulima wa kabichi, vitunguu na viazimbatata Nyeri.

Kabla ya upanzi, mashimo au mitaro imwagiliwe maji, kasha shughuli hiyo iendelee. Pia, ni muhimu kuinyunyizia maji kwa kipimo baadaye.

You can share this post!

Mgonjwa aliyegundulika kuugua Ebola mjini Goma afariki

Dani Alves ahusishwa na uhamisho kujiunga na Arsenal

adminleo