Makala

KILIMO: Ukuzaji wa matango 

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KILIMO cha hema au vifungulio almaarufu greenhouse kimeonekana kupigiwa upatu hasa kwa sababu ya manufaa yake.

Athari za wadudu na magonjwa kwa mimea inayokuzwa kwenye hema zimethibitiwa, ikilinganishwa na eneo tambarare.

Aidha, eneo tambarare magonjwa na wadudu wanasemekana kuchangiwa pakubwa na upepo.

Hema limeezekwa juu na kandokando, hivyo basi magonjwa yanayoshuhudiwa ni yanayosambazwa na mimea inayokuzwa humo.

“Baadhi ya magonjwa kulingana na familia ya mimea husalia udongoni, na hayo ndiyo mkulima hupambana nayo katika kilimo cha hema,” anasema afisa Jessica Mbaka kutoka tasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo), tawi la Thika. Karlo pia hutoa mafunzo ya uzalishaji wa mazao kwenye hema.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtaalamu huyu, ni rahisi kufuatilia mienenendo ya kila mmea kwenye hema.

Isitoshe, kilimo cha vifungulio kinahitaji sehemu ndogo ya ardhi.

Bw Raphael Ngare ni mkulima wa pilipili mboga, nyanya, matango na spinachi kwenye hema.

“Nina mahema kadhaa, yenye kimo cha mita nane kwa 30,” anadokeza Bw Ngare.

Katika makala haya tunaangazia kilimo cha matango au mamumunya na kulingana na Bw Patrick Kamuni, mtaalamu kutoka Ken Agro Suppliers Ltd ni kwamba gharama ya kuyakuza ni nafuu ikilingalinishwa na mimea mingine.

Anasema mbegu zake hazihitaji kupandwa katika kitalu. Hupandwa moja kwa moja shambani.

“Hayahitaji miche, ila hupandwa moja kwa moja, kazi ikiwa kuyatunza pekee na kuvuna,” anasema Bw Kamuni.

Mtaalamu huyu anasema ekari moja inahitaji sacheti ya gramu 500 za mbegu. Gramu 100 inagharimu kati ya Sh3, 200-3, 400.

Matango yanastawi maeneo yenye joto na kupokea kiwango cha mvua ya kutosha.

“Maji ni kiungo muhimu katika kustawisha kilimo chake. Yasiyopokea mvua ya kutosha, mkulima atumie mfumo wa kunyunyizia maji mashamba,” anahimiza Bw Kamuni.

Eneo la upanzi linapolimwa, ufanye udongo uwe mwepesi na mwororo. Andaa mashimo, nafasi kati yake iwe karibu sentimita 45. Laini ya mashimo hadi nyingine iwe na kimo cha sentimita 60.

Weka mbolea au fatalaiza kwenye mashimo yale, ichanganye sambamba na udongo uliotolewa shimoni.

Rejesha mchanganyiko huo, halafu upande mbegu na kuzifunika kwa udongo kiasi.

“Nyunyizia maji kwa kipimo, ingawa pia kuna wanaomwagilia mashimo maji kabla ya upanzi,” anashauri Kamuni.

Kifuatacho, ni matunzo kwa njia ya kunyunyizia maji.

Mbegu huchipuka ardhini kati ya siku ya tano na saba baada ya upanzi.

“Wakati jua limeangaza au msimu wa kiangazi, mimumunya inyunyiziwe maji asubuhi na jioni,” anahimiza mtaalamu Kamuni.

Palizi dhidi ya makwekwe ni shughuli muhimu kwani hupunguza uwezekano wa kusambaa kwa wadudu na hata magonjwa.

Fatalaiza

Yanapoanza kuchana maua, mkulima anahimizwa kuyaweka fatalaiza yenye madini ta Nitrojini, Potassium na Calcium.

Aidha, mbolea hii husaidia katika ustawishaji wa matango yanapotunda.

Siku ya 45 huanza kuvuna, na kulingana na Patrick Kamuni ekari moja ina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 25-30 za matango.

Yanayopaswa kuvunwa ni yenye urefu wa kati ya inchi 4-5. Yakikomaa zaidi hukataliwa sokoni. Kilo moja hununuliwa Sh30.

Magonjwa yanayoathiri mamumunya ni; early na late blight, husababishwa na baridi ya majira ya asubuhi na jioni.

Wadudu wanaoshuhudia ni viwavi, vipepeo na nzi wa matunda (fruit fly). Nzi huyadunga na kusababisha yaoze na kufanya yakatiliwe sokoni.

Kuna matango ya aina mbili; ya kijani na ya manjano-yenye ladha sawa na ya matufaha.