Makala

KILIMO: Vitunguu

September 27th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ASILIMIA kubwa ya vitunguu vinavyoliwa humu nchini vinatoka taifa jirani la Tanzania.

Hili hasa linatokana na uhaba wa wakulima wa zao hili humu nchini. Maeneo yanayovizalisha ni; Nyeri, Kajiado, Naivasha, Oloitoktok na Kakamega.

Vitunguu vinaaminika kunawiri katika udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji. Kulingana na wataalamu, kiwango cha asidi, pH, kinapaswa kuwa kati ya 5.8 – 6.5. Pia wanashauri haja ya mkulima kupimiwa udongo wa shamba lake kabla kuzamia kilimo.

Vitunguu aina ya Jambar F1, Islero, Red creole, Red Passion na Red Pinnoy, ndivyo hukuzwa Kenya. Vinastawi maeneo yenye joto, kiwango kikikadiriwa kuwa nyuzi 15 – 30, kipimo cha sentigredi.

Mkulima wa vitunguu vyekundu vya mviringo eneo la Thika Bw Derrick Mutugi anasema ekari moja inahitaji karibu kilo 1.5 ya mbegu.

“Ekari moja inahitaji kati ya kilo 1 hadi 1.5 kulingana na aina ya vitunguu na nafasi ya upanzi,” aeleza mkulima huyu.

Anaongeza kwamba ukubwa wa vitunguu unategemea nafasi ya upanzi.

Kuna njia mbili kukuza zao hili; kupanda mbegu moja kwa moja shambani au kupitia miche – huandaliwa kitaluni. Hata hivyo, miche inapendekezwa kwa sababu upanzi wa moja kwa moja unahitaji umakinifu wa hali ya juu.

“Taratibu za upanzi na utunzaji wa miche zizingatiwe. Miche ya vitunguu huchukua kati ya wiki nne hadi sita,” asema Julius Nduati kutoka African Soil and Crops Care Ltd.

Kulingana na mtaalamu huyu shamba linapaswa kuandaliwa vyema, wiki kadhaa kabla ya upanzi ili kuruhusu makwekwe kukauka na hata udongo kutulia.

Nafasi kati ya miche inapendekezwa kuwa sentimita 8 – 10.

Mstari wa miche hadi mwingine uwe sentimita 15.

Bw Nduati anasema mbolea ya mifugo au kuku, iliyoiva sawasawa ndiyo bora. “Mkulima pia anaweza kutumia fatalaiza yenye madini ya Ammonia au Phosphorous,” ashauri mdau huyo.

Bw Derrick Mutugi ambaye anaendelea kutatua uhaba wa vitunguu eneo la Thika anaeleza kwamba wakati mwafaka kuhamisha miche kutoka kitalu hadi shambani ni majira ya asubuhi au jioni. Wakati anga imesheheni mawingu yanayodhibiti makali ya miale ya jua pia ni bora kufanya shughuli za uhamisho.

Maji ni kiungo muhimu katika ukuzaji wa vitunguu, hususan kuunda kiazi chake.

Wiki ya nne, unahimizwa kutia kwenye mashina ya vitunguu fatalaiza yenye madini ya Nitrojini.

Palizi ni muhimu ili kudhibiti makwekwe ambayo huleta ushindani wa lishe kwa mimea, mwangaza na nafasi kunawiri.“Ikumbukwe kuwa viazi vya mviringo vinahitaji nafasi ili kunenepa, kuwepo kwa makwekwe huathiri shughuli hiyo. Palizi inapofanywa, mkulima awe makini ili asiathiri kiazi,” afafanua mtaalamu Nduati.

Maeneo yanayopokea kiwango kidogo cha mvua kama vile Kajiado, Oloitoktok na hata Naivasha, mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kwa mifereji hutumika. Baadhi ya wakulima wamesindika mifereji katika mashamba.

Vitunguu huwa tayari kwa mavuno kati ya miezi minne hadi mitano baada ya upanzi.

Dalili ni majani kuanza kukauka na kiazi kuondoa udongo. Wiki kadhaa kabla wakati huo, mkulima anashauriwa kukomesha unyunyiziaji maji.

Ekari moja iliyotunzwa vyema ina uwezo kuzalisha kati ya tani 20 – 30. Tani moja ni sawa na kilo 1,000.

Bw Mutugi anasema kilo huwa kati ya Sh40 – 80, kulingana na msimu. Masoko ya mkulima huyo ni Makongeni Thika, Githurai na Marikiti. Hali kadhalika, Mutugi hutumia mitandao kutafuta soko lenye mapato bora.

Wataalamu wanahimiza mkulima alenge kupata mazao kati ya mwezi Novemba hadi Mei, ambapo vitunguu huwa vimeadimika.