Makala

Kilimohai chapigiwa chapuo

November 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wamehimizwa kukumbatia kilimohai – Organic Farming – kwa sababu imethibitishwa kwamba ni chenye faida kubwa.

Mazao yatokanayo na aina hii ya kilimo yana uwezo mkubwa wa weza kuzuia maradhi kama kisukari, na hata shinikizo la damu.

Mnamo Ijumaa kulikuwa na hafla ya kuadhimisha miaka 25 tangu shirika lisilo la kiserikali linalojulikana kama Mpango wa Ustawishaji Kilimo Endelevu katika Jamii – Sustainable Agriculture Community Development Program (SACDEP) – likisherehekea maswala ya kilimohai.

Hafla hiyo iliendeshwa katika kituo kikuu cha SACDEP eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki.

Mwanzilishi wa kituo hicho cha SACDEP Bw Ngugi Mutuura, alisema maradhi kama kansa yameongezeka humu nchini kwa sababu ya kemikali aina nyingi kuingizwa nchini licha ya kupigwa marufuku.

Alisema kilimohai ni bora zaidi kwa sababu kinawapa wakulima wa chini fursa ya kupata mazao mengi hasa wakikizingatia kwa makini.

“Niawahimiza mkumbatie kilimo cha aina hii kwa sababu upo ushahidi mwingi wa wakulima wengi ambao wamenufaika pakubwa na mpango huo,” alisema Bw Mutuura.

Alisema maradhi ya kansa huenda yakaendelea kuenea nchini ikiwa chakula kinachokuzwa kinawekwa kemikali tofauti zinazoharibu ubora wa chakula shambani.

“Kansa inaweza kupungua kuenea nchini kwa kiwango fulani tukizingatia vyakula aina ya ‘organic’ ambavyo ni bora zaidi,” alisema Bw Mutuura.

Hivyo alitoa mwito kwa vijana wanaojihusisha na kilimo kufanya hima kuendeleza kilimo cha ‘organic’ badala ya kutafuta kazi za ofisini.

Mmoja wa washikadau wa kilimo bora cha organic, Bi Annette Massman, alisema tayari amefanya ushirikiano wa karibu na shirika la SACDEP kwa lengo la kuboresha uzalishaji wa chakula cha organic.

Alisema licha ya kemikali kadha kupigwa marufuku na serikali zisitumike kwa kilimo, bado kuna wale wanaoendelea kuzitumia kwa unyunyizaji na fatalaiza kwa mashamba zao.

Baadhi ya wakulima waliohudhuria hafla hiyo waliridhishwa na utumizi wa kilimo cha organic wakisema hiyo ndiyo njia ya pekee ya kufuata ili kuboresha kilimo katika taifa hili.