• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Kilio cha askari jela aliyefutwa kazi bila shtaka, kesi wala barua 

Kilio cha askari jela aliyefutwa kazi bila shtaka, kesi wala barua 

NA MWANGI MUIRURI

AFISA wa Idara ya Huduma za Magereza kutoka Kaunti ya Homa Bay analilia haki baada ya kufutwa kazi kwa kile anachodai hakuwa amefanya kosa lolote ili uamuzi huo uafikiwe. 

Polisi huyo anasema alipigwa kalamu baada ya kutembelea mamake mzazi aliyekuwa anaugua, licha ya kuwa na ruhusa ya wakubwa wake.

Bw Joseph Odhiambo Ochoro aliajiriwa kazi 2019 na akatumwa kuhudumu katika jela la Nyahururu, Kaunti ya Laikipia na akiwa safarini kwenda nyumbani, naye pia akaugua.

Akiwa ni kifungua mimba katika familia ya watoto watatu, Bw Ochoro anasema kwamba yeye ndiye alikuwa tegemeo kwa mamake mzazi na ambaye alikuwa ameanza kulemewa na maradhi.

“Mwaka 2022 nikielekea nyumbani kuona mamangu, niliugua nikiwa Kisii,” anasema.

Anadokeza kwamba alikuwa amepewa likizo ya siku 14.

Anasema kwamba walimpeleka hadi Hospitali ya Oasis iliyoko Mjini Kisii ambako alilazwa kwa siku nne kisha akapewa ruhusa kuenda nyumbani.

Anasema kwamba alipotoka hospitalini, alipitia katika jela la Kisii ambapo alifahamisha Naibu Kamanda wa gereza hilo kuhusu hali yake ya kiafya “na kwa kunihurumia, alinipa Sh100 kisha akaninunulia matunda, yakiwemo machungwa”.

Anasema kwamba alimuomba afisa huyo atume ujumbe spesheli kwa jela la Nyahururu kufahamisha wakubwa wake kwamba alikuwa amekumbwa na ugonjwa wa dharura na angechelewa kurejea kazini.

“Nikiwa na imani kwamba afisa huyo alikuwa ametuma ujumbe huo kazini Nyahururu, nilisafiri hadi nyumbani ambapo maradhi yalizidi kiasi kwamba nililazwa tena katika Hospitali ya St Lawrence, Homa Bay kwa mwezi mmoja,” anaelezea.

Anasema baada ya kupewa ruhusa ya kutoka hospitalini, alienda nyumbani na akakaa kwa miezi mingine miwili ili kumaliza dawa na pia kliniki.

Aliporejea kazini Nyahururu akiwa amepata nafuu, alikutana na afisa wa kinidhamu aliyempasha habari kwamba kutoweka kwake kulikuwa kumemsababishia kufutwa kazi.

Anasema kwamba alitaka barua ya kuachishwa kazi “lakini nikafahamishwa kwamba faili yangu ilikuwa imepelekwa kwa Makao Makuu ya Idara ya Magereza Jijini Nairobi”.

Anasema kwamba hali ya mshtuko ilimkumba na ndipo alipigia simu afisa wa Gereza la Kisii na ambaye alikuwa atume ujumbe spesheli wa kuwajulisha wakubwa wake kwamba alipatwa na maradhi.

“Sikuamini maskio yangu afisa huyo aliponijibu kwamba alisahau kutuma ujumbe huo. Lakini alinituliza kwa kusema kwamba alikuwa tayari kuwa shahidi wangu kwamba nilikuwa mgonjwa na hivyo basi singeweza kufika kazini,” anasema.

Kufikia sasa, afisa huyo aliyerejea nyumbani kwao Homa Bay hajawahi kupashwa kwa njia rasmi kwamba alifutwa kazi wala kuelezwa sababu za hatua hiyo kuchukuliwa.

Bw Ochoro anasema kwamba faili yake ni nambari 20190421849, nambari yake ya kazi ikiwa ni 52775.

“Kwa sasa mimi na unyonge wangu wote niko huku vijijini nikishiriki vibarua bila mtetezi na mamangu tayari ashaaga dunia kutokana na umaskini ulionikumba kiasi cha kulemewa kumnunulia dawa,” anasikitika afisa huyo.

Wakili wa Mahakama Kuu, Bw Timothy Kariuki anasema kwamba “ningemshauri Bw Ochoro aandae kesi mahakamani akidai wakubwa wake wafike kortini kuelezea hali halisi yake kuachishwa kazi”.

Aidha, alisema kwamba kesi ya kudai fidia au arejeshwe kazini inapaswa kupelekwa katika mahakama ya kutatua mizozo ya kikazi.

“Njia nyingine ya kutatua suala hili ni mwanasiasa yeyote aliye katika bunge la Kitaifa au lile la Seneti aitishe taarifa kuhusu afisa huyo kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kuhusu mazingira kamili ya ajira ya afisa huyo,” akasema.

Bw Kariuki alisema kwamba ndani ya taarifa hiyo ndipo itabainika waziwazi hali halisi kuhusu sakata ya afande Ochoro.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Safari ya Mkenya anayemiliki hospitali Amerika 

Fahamu mwalimu anayetumia TikTok kunoa wanafunzi wake  

T L