Makala

Kilio cha mume mila kali ikimzuia kumzika mkewe wa kwanza

February 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

Suala la mazishi katika jamii ya Abaluhya huzingirwa na tamaduni chungu nzima.

Na mkanganyiko huwa mwingi zaidi, iwapo aliyeaga dunia ni mwanamke aliyeachana na mume wa ndoa.

Wadi ya Shamakhokho, kwenye kituo cha magari, shughuli za biashara mbalimbali kama vile uuzji njugu, ndizi zinaendelea. Shughuli hizi huisha majira ya saa moja hadi saa mbili usiku, wengi wa wafanyabiashara hao wakihofia usalama wao.

Mita tatu kutoka kwenye kituo cha magari, familia ya Samson Khaojeri imemwacha mpendwa wao ambaye ni mke wa kwanza kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mjini Mbale kwa muda wa wiki nne wasifahamu iwapo watamzika au kusubriri hadi jamii itakapogawanya kipande cha ardhi.

Jamii ya Bw Khaojeri, imemzuia kumzika aliyekuwa mke wake wa kwanza, aliyekutana na mauti Januari 5, 2024 akielekea nyumbani kwa aliyekuwa mumewe, baada ya kufahamishwa mwanawe kitinda mimba anaugua ugonjwa wa kifafa na kwamba ulikuwa unamzuia kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Kulingana na ripoti kutoka kwa maafisa wa polisi, mama huyo mwenye umri wa miaka 49, aliuawa na watu wasiojulikana majira ya saa tisa asubuhi na kuchukua vitu alivyokuwa navyo.

“Nilipata habari kutoka kwa wapita njia kwamba Mama Ruth ameuawa, nilikimbia pale na kupata ni yeye. Polisi walichukua mwili wake na kupeleka kwa hifadhi ya maiti. Awali alinifahamisha atasafiri kuja kumwona mwanawe ambaye alimwacha akiwa na miaka miwili. Mwanangu anaugua ugonjwa wa kuanguka na lazima mamake angekuja kumwona,” Bw Khaojeri asimulia.

Bw Khaojeri aliambia Taifa Leo kulingana na mila za jamii ya Tiriki, haruhusiwi kumzika mke wa kwanza kabla hajafahamu mke wa pili atamzika wapi.

“Baada ya taarifa hiyo kuenea, familia yangu ilichukua jukumu la kujulisha familia yake, iliyokataa kumzika na kunipa idhini kwa sababu ni mama wa watoto wangu wanne,” aliendelea Bw Khaojeri.

“Jamii ilizuia kuzika mama kwa sababu kipande cha shamba kimesalia chini ya familia yangu na kukosa kugawanywa. Iwapo shamba lingekuwa langu, ningegawanya mara mbili na kumzika,” alisikitika Bw Khaojeri.

Mzee wa jamii hiyo John Chebseba, alisema mila za jamii hiyo ni lazima apate sehemu yake na kugawanya mara mbili. Sehemu moja ikipewa watoto wa mke wa kwanza, sehemu iliyosalia kuwa ya mke wa pili ambaye anatambulika na jamii.

“Itachukua muda kwa kuwa watoto wa kiume kwenye boma hawako. Tunawasubiri waje mwezi huu. Jamii ya mama huyo pia wamekuwa wagumu kuzika mtoto wao, wanadai kuwa mahari ililipwa na sasa mzigo si wao, watakuja kuhudhuria mazishi tu,” alifafanua Bw Chebseba.

Pia, jamii hiyo imejikita kwa mila nyingine ambayo mwanamke huzikwa upande wa kushoto.

“Kuchimbwa kwa kaburi hutegemea jinsi nyumba ilivyojengwa na mlango umewekwa vipi. Iwapo mwanamke waliachana na mume kisha kuaga, huzikwa nyuma ya nyumba au kwenye ua ama kwenye shamba la ndizi kwa kuwa anafahamika kuwa mgeni kwenye jamii hiyo,” aliongeza Bw Chebseba.

Bw Chebseba alisema maziko ya mwanamke anayezikwa kwenye shamba la ndizi au nyuma ya nyumba ni yule mume wake hakupata nafasi ya kuoa tena.