Kilio kwa vijana ‘waliowekeza’ mtandaoni tovuti ilipozimika ghafla ikaenda na pesa zao
NA FRIDAH OKACHI
WAWEKEZAJI wanalia baada ya kupoteza kiasi kikubwa cha pesa baada ya kushawishika na kujiunga, kisha kuwekeza kupitia njia ya mtandao ambao walipokea pesa kwa kiasi fulani.
Waathiriwa hao ambao wengi wao ni vijana, wahubiri na wanawake waliopoteza zaidi ya Sh100,000 ‘waliwekeza’ kupitia tovuti hiyo ambayo tunabana jina kwa sababu za kisheria – hakuna kesi yoyote kortini kwa sasa kuhusu madai ya ulaghai yaliyoibuliwa.
Pasta Wilson Ambaje kutoka mtaa wa Dandora, alijiunga na tovuti hiyo baada ya kupata maelezo kutoka kwa mwanawe. Alielezwa kuwa angepata malipo ya kila siku baada ya kuwekeza.
“Mwanangu alikuja nyumbani na kunieleza jinsi alipata malipo ya Sh84 kila siku kwa kuwekeza Sh1,000. Nilipofuatilia akaunti yake nikaona alipata Sh420 kwa siku tano na ilinivutia zaidi,” alisema Bw Ambaje.
Katika ‘uwekezaji’ huo, mteja alifahamishwa kununua mashine kulingana na uwezo wake. Kisha alipewa idhini ya kutoa pesa zake wakati wowote alipohitaji.
“Nilitafakari na kuona ni njia nzuri. Nilinunua mashine ya Sh20,000. Kila siku nilikuwa napata Sh1,000. Kabla tovuti hiyo ipotee nilikuwa nimefikisha Sh100,000. Siku kama ya leo nilikuwa nimetoa Sh40,000 na nikarudisha.”
“Baada ya saa nne hivi watu walianza kutoa tetesi kwamba mtandao huo haufanyi kazi kama hapo awali. Msimamizi wa kundi alitutuliza na kisha ukapotea kabisa. Tulipozidi kuuliza ndipo alikosekana wa kutufahamisha yanayojiri,” alisikitika Bw Ambaje.
Kufungua biashara ya nguo
Christine Amwayi, 29, ni miongoni mwa wale waliojiunga na uwekezaji huo kupitia kundi la WhatsApp. Bi Amwayi alikuwa na matumaini ya kufungua biashara kwa pesa hizo.
“Nilikuwa nimefikisha Sh50,000. Ndoto yangu ilikuwa kufungua biashara ya kuuza nguo katika mtaa huu wa Dandora. Sikuwa na fikra kuwa kitaniramba hivi,” alisema Bi Amwayi.
Bi Amwayi alisema kiongozi wa kundi la WhatsApp kwa jina ‘Jennifer’ alikuwa akiwatuliza kabla ya simu zake kuzima. Pia, wakiwa kama kundi la mji wa Nairobi walielekea katika afisi walioalikwa mwanzoni na kupata hayupo.
“Malalamishi yalipozidi, tuliungana kama kundi na kwenda katika jumba la Britam, tulipigwa na butwaa tulipofika pale na kuambiwa hafahamiki,” aliongeza Bi Amwayi.
Kuongeza msumari kwenye kidonda, Bw Rama Kamau, 30, aliacha kazi na kusalia nyumbani kwake akijua, uwekezaji huo ungempa riziki ya kila siku.
“Nimebaki wa kutafuta kazi baada ya kufikiria kuwekeza kwenye tovuti hiyo ingenipa maisha bora. Mwezi wa kwanza nilipata Sh15,000 ambazo nililipa kodi na kununua chakula,” alisikitika Bw Kamau.
Taifa Leo Dijitali iliweza kubaini kuwa tovuti hiyo ilisajiliwa Agosti, 2023. Usajili huo ukiwa na mianya mingi kwa kukosa barua pepe. Nambari ya simu iliyowekwa ikiwa haipatikani hata kwenye WhatsApp.