Kilio Nairobi bei ya kutumia vyoo vya umma ikipanda kutoka Sh10 hadi Sh20
BAADHI ya wakazi wa Kaunti ya Nairobi wanalia baada ya bei ya kutumia vyoo vya umma vimeongezwa kutoka Sh10 hadi Sh20.
Taifa Leo Dijitali ilipozungumza na baadhi ya wakazi ambao huwa na shughuli mbalimbali katikati mwa jiji, walisema kuwa wanahisi kuwa hatua ya wasimamizi wengine wa vyoo vya umma ya kupandisha bei haifai.
“Nina shughuli za hapa na pale jijini na utapata kuwa ukikuja hapa, unaambiwa kuwa gharama ya kutumia choo ni Sh20. Chukulia kwa mfano hiyo siku umeenda haja ndogo mara tano, hiyo ni Sh100,” Kiberenge aliambia Taifa Leo Dijitali.
Kwa moto uo huo mkazi na mfanyabiashara mwingine kwa jina Grace alisema kuwa vyoo vya umma vinafaa kuwa Sh10.
“Mimi huenda msalani kwa kulipa Sh10. Mbona niende katika kile cha Sh20 ilhali gharama ya maisha iko juu?” Grace alishangaa.
Taifa Dijitali ilitembela baadhi ya vyoo vya umma katikati mwa jiji na kubaini kuwa kuna vingine ambavyo vinawalipisha wateja Sh20.
Wakati wa kukusanya taarifa hii, nilifanya mteja ambaye alikuwa anahitaji huduma hii,
“Ni pesa ngapi kutumia choo hapa?” nilimuuliza mhudumu nikionyesha nia ya kutolipa zaidi ya Sh10.
Wewe una pesa ngapi? Njoo uingie na hiyo Sh10 yako,” mhudumu alisihi. “Ukiwa na Sh10 hatuwezi kukosana, unaingia tu.”
Alipokuwa anatetea viwango vya gharama anazotoza wateja, alijitetea akisema kuwa vyoo vyao ni safi na kwamba kuna maji na sabuni ya kunawa mikono.
“Ingia uone, ni safi, unaona tuna hata sabuni. Hata choo chenyewe hakitoi harufu,” alisema huku akikisafisha choo.
Hata hivyo, kuna baadhi ya vyoo ambvyo havijapandisha bei.
“Unataka kuingia? Aaah…bado ni Sh10,” mwingine alisema tulipouliza bei ya kutumia sehemu hizo za kutimiza haja.
Gharama ilipanda
Haya yanajiri tu miezi michache baada ya wasimamizi wengine wa vyoo vya umma kupandisha bei kutoka Sh10 hadi Sh20.
Hii ilipingwa sana katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku baadhi wakilalamika kuwa hawafai kufinywa wakati gharama ya juu ya maisha inawazonga wananchi
Akirejelea malalamishi hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya Kaunti ya Nairobi Diwani Maurice Ochieng alisema kuwa vyoo vyote vya umma vinafaa kuwa Sh10.
“Ninakataa kabisa hatua ya wasimamizi wengine wa vyoo hivyo ya kupandisha bei. Kwenda haja katika vyoo vyote vya umma vinafaa kuwa Sh10 wala si Sh20,” alisema Bw Ochieng.
Kando na hayo, alisema kuwa hiyo ni kama kuwakandamiza wakazi wa Nairobi ambao tayari wamelemewa na gharama ya juu ya maisha.
“Tunatoa notisi na ikiwa tutakuta choo ambacho kinatoza watu Sh20 basi hatua mwafaka itachukuliwa.”