Kina baba wanavyowaficha mabinti wao shuleni wasikeketwe
IMEBIDI baadhi ya wazazi katika Kaunti ya Wajir watafute mbinu tofauti ili kuzuia tohara ya watoto wao wa kike, huku kina mama wakilaumiwa kwa kuendeleza desturi hii.
Ili kukabili ukeketaji wa wasichana, wazazi hawa wanalazimika kuwaficha mabinti wao katika shule za bweni wakati wa likizi.
Mmoja wa Wakazi wa Wajir Kusini, Bw Hassan Said mwenye umri wa miaka 43, alilazimika kumwacha bintiye katika shule ya bweni ili kumkinga.
Hii ni baada ya mkewe kupata msukumo wa kuwasafirisha mabinti wao kwenda mashambani kwa nyanya yao ambaye alikuwa na nia ya kuwakeketa.
Bw Said alisema mamake mzazi amekuwa akiwalenga mabinti wake kwa muda mrefu. Kwa hivyo, amefanya iwe vigumu kwa mama kuwasafirisha wote watatu.
“Desturi hii ni ni kwa sababu ya utamaduni ambao umekita mizizi katika jamii yetu ya Somali. Muhula huu, nimemficha binti wangu mmoja katika shule la bweni. Niligundua mke wangu alipata shinikizo kutoka kwa mama yangu mzazi awapeleke nyumbani,” alifunguka Bw Said. “Mamangu amekuwa akitaka mabinti wangu kukeketwa. Mimi siwezi kukubali hili lifanyike.”
Bintiye Said, alifurahia hatua ya baba yake kumpeleka mafichoni ili kukwepa ukeketaji. Alisema yupo tayari kupambana na unyanyapaa hata baada ya kukamilisha masomo yake.
“Kila wakati mimi humweleza baba kuwa sitaki. Kuna siku alinyamaza nikawa na hofu sana. Lakini baadaye alizungumza nami baada ya wiki moja na kunifahamisha kuwa hataruhusu watoto wake wafanyiwe tohara hiyo,” alisimulia.
“Shule zilipofungwa, baba yangu aliomba wasimamizi nisalie shuleni. Haijalishi nitakaa huku hadi lini almuradi niwe na amani,” alifichua. “Baba yangu alimakinika hivi dhidi ya mtego wa ukeketaji kwa sababu alikuwa na mpango wa kusafiri wakati wa likizo.”
Shirika la kushughulikia maslahi ya wanawake la Women Organizing Women Networking lilisema kuna wanafunzi zaidi ya watano ambao wamesalia shuleni wakiwa na hofu ya kukeketwa.
Mkurugenzi wa shirika hilo Bw Billow Adow alisema wanatoa msaada kwa wasichana hao ambao pia waliogopa kurejea nyumbani baada ya shule kufungwa.
“Haifai kuwalazimisha wasichana wetu wakeketwe. Mbona tuzidi kuendeleza mila hii ilhali tunafahamu madhara yake?” aliuliza Bw Adow.
Kulingana na Bw Adow kila eneobunge Wajir lina wanaume watano ambao wana jukumu la kuendeleza kampeini dhidi ya uteketaji.
Anaeleza kuwa harakati hizi zimesaidia kupunguza visa vya ukeketaji kwa asilimia nne huku wanaoendeleza desturi hii wakifanya kisiri kuogopa kushtakiwa.
“Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha tumepiga hatua ya kupunguza visa kwa asilimia nne. Vyombo vya usalama vimeonya wakazi wakome kuendeleza ukeketaji la sivyo wakabiliwe kisheria,” aliongeza Bw Adow.
Sawa na Bw Said, pia Bw Adow anawalinda mabinti wake wawili dhidi ya ukeketaji. Kulinga nao, iwapo wanaume wataungana kukabili maovu haya kwa wanawake, ukeketaji utatokomezwa.
“Nina mabinti wawili wa umri wa miaka 5 ambao mama yao alinifahamisha wanahitaji kwenda mashinani kukeketwa. Nilipinga wazo hilo na kumweleza iwapo anahitaji kusafiri awaache nyumbani wakiwa na mjakazi aende pekee yake,” alieleza.