Makala

KINA CHA FIKIRA: Iweje wageni wanakifurahia Kiswahili huku wasemaji asilia wakikibeza?

November 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

WIKI hii ninaandika makala hii nikiwa Addis Ababa, jiji kuu la Ethiopia.

Nilipokuwa mdogo nilimsikia mtangazaji maarufu Job Isaac Mwamto akiita nchi hii, Uhabeshi.

Mwamto alisibu katika kuiita Ethiopia, Uhabeshi. Watu wa huku wenyewe wanajiita hivyo kwa kweli.

Mathalani nimeona Nairobi na Addis migahawa yenye jina Habesha, jina linalofungamana na ujitambulisho wa nchi ya watu hawa waungwana. Nilipokuwa Misri mnamo 2017 nilishangaa kwamba wenyewe wanajiita watu nchi ya Masri, jina linalokaribiana sana na Misri la Kiswahili.

Basi nimepokelewa hapa kwa vilili na vigoma. Watu wema sana hapa Ethiopia na ufukara tele. Nimewaona ombaomba wengi sana katika eneo Bole jijini hapa, ambapo ndipo ilipo hoteli ya Ethiopian Skylight nilikofikia.

Imepita miaka sita tangu nilipozuru mara ya mwisho jiji hili.

Ajabu ni kwamba ndani ya kipindi cha miaka sita watu wa Addis wamelibadili sana jiji lao kimandhari. Hoteli nyingi mpya, ikiwemo hii nilikofikia. Majengo mengi makubwa marefu na tena ya kisasa kila pembe. Ila ufukara bado unaonekana kila janibu. Ombaomba wengi kama mchanga ufukweni.

Idadi kubwa kama hii ya ombaomba niliona nilipozuru jiji la San Francisco, kwenye jimbo la California, Marekani.

Naam, niliona ufukara mkubwa katika jiji la San Francisco Marekani kama ombaomba ni kigezo cha kupimia ulitima.

Hata hivyo, natahadharisha kwamba baadhi ya hawa ombaomba, wa Addis Ababa, San Francisco na Nairobi wana nafasi ya hali kuliko wale wanaoombwa. Utamwona mtu anaombaomba ukampa hela kidogo, kumbe anamiliki mali nyingi kuliko utakazowahi kumiliki maishani mwako.

Kuhusu jiji la Addis Ababa, nami niligundua kwa mshangao mkubwa kwamba linamiliki mali nyingine tofauti kuliko nilivyodhani awali. Nilitarajia kusikia watu wakisema Kiswahili, angao kidogo, kwenye barabara za Addis Ababa.

Hivyo ndivyo, ilivyotukia kwenye ziara zangu Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini. Sharti nikiri kwamba mbali na salamu za Kiamhara “Salama,” neno linaelekea kuwa na usuli wa Kiarabu, sijasikia Kiswahili hata kidogo. Mkenya mmoja niliyekutana naye ni Mzungu mweusi, haongei Kiswahili.

Kwa hiyo unaweza kuelewa mshangao wangu nilipopita karibu na eneo moja la starehe na kusikia nyimbo za Diamond Platinumz zikidondoka kama maji ya mafuriko.

Nilisimama kutazama. Nilishangaa ghaya ya kushangaa. Nyimbo za Diamond za Kiswahili zinadunda huku watu wakinengua na kusowera. Hapa Addis, pahali ambapo kuwapata watu wanazungumza Kiswahili ni jambo la nadra sana, Diamond anaimba Kiswahili chake na Wahabeshi wanafaidi uhondo si haba.

Nikenda zangu. Takriban saa mbili baadaye, nilipopita hapo tena, nyimbo zake Diamond zilikuwa bado zinachezwa. Utajiri huu wa Kiswahili kutamalaki muziki hapa Addis Ababa ni jambo ambalo sikulitarajia. Basi tuhitimisheje? Kiswahili ni kitamu katika muziki, maandishi na kinywani. Kutokana na hilo kitaendelea kuwavutia watu wasiokuwa Waswahili asilia au wa kupanga. Tatizo kubwa kwa Kiswahili ni hawa Wazungu weusi na mielekeo yao hasi.