• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
KINA CHA FIKIRA: Kinaya cha waandishi wa Kenya na Tanzania kuongoza katika kukivyoga Kiswahili

KINA CHA FIKIRA: Kinaya cha waandishi wa Kenya na Tanzania kuongoza katika kukivyoga Kiswahili

Na KEN WALIBORA

MNAMO Mei 21, 2019, nilimwandikia mkubwa mmoja wa kituo cha runinga ujumbe huu: “Watu wako wanaandika kero la. Je ni kero ya au kero la?”

Akajibu kwamba hanielewi nasema nini. Nadhani labda ni tatizo la iktisadi ya arafa au ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani.

Mara nyingine unakuwa na mawazo ila maneno ya mkato ya arafa yasikidhi haja ya mawasiliano. Nilichotaka kusema ni kwamba watu wanaofanya kazi chini yake walibebwa na mawimbi ya kurusha kila nomino katika ngeli ya LI-YA.

Hawaheshimu uainisho wa ngeli bali wanafikiria kila nomino ipo katika ngeli hiyo. Hilo linatatanisha upatanisho wao wa kisarufi kwa maana wanaambisha viambishi visivyo. Utawasikia wakisema kero hilo, kero la, shule la msingi, lugha la Kiswahili, kalamu langu, pua langu shingo langu (badala ya pua/shingo yangu).

Madereva wa bodaboda wakisema pikipiki langu, tutaonea imani. Wapishi wakisema kijiko langu, tutawaonea huruma. Madaktari wakisema maradhi lako, tutawasamehe maana taaluma yao haijakitwa katika umilisi wa Kiswahili safi.

Ila ukweli ni kwamba wapo madereva wa bobaboda, wapishi, na madaktari wanaosema Kiswahili kizuri kuliko baadhi ya wanahabari wa Kiswahili.

Mimi hilo ndilo linaloniuma siku zote, linaniuma kuliko changamoto ya Victor Wanyama kuselelea katika timu ya Tottenham Hotspurs.

Wanyama amewachezea Spurs kwa kujituma, sasa wanaonyesha kutaka kumtema kama mtu anayejaribu kutema shubiri. Ila kama Wanyama bado ana siha nzuri na weledi anaweza akaendelea kuchezea kwengineko anakotakiwa. Wanahabari wa Kiswahili wamejiambika tabia za ki-Spurs; wanataka kukitema Kiswahili safi, wakitelekeze, wakitupilie mbali, wasiwe nacho tena kabisa. Wanataka Kiswahili safi kiende kuchezea timu gani?

Wakiua hatua kwa hatua

Hususan nawalaumu wanahabari wa Kenya na Tanzania, nchi ambazo zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa kielelezo chema cha matumizi ya Kiswahili.

Wanahabari wanaendelea kukiua Kiswahili hatua kwa hatua. Hili mimi nimelitafakari kwa tafakuri za miaka na mikaka. Nadhani kwamba Kiswahili kilianza kuugua kilipoingia katika awamu ya Kiswanglish, yaani mchanganyiko wa maneno ya Kiswahili na Kiingereza katika mfumo wa kimsingi wa Kiswahili.

Maneno ya Kiingereza yalipoingizwa katika Kiswahili, yaliswahilishwa ili yafaane na mfumo wa Kiswahili k.v. wametia saini. Neno “sign” au “signature” liliswahilishwa kimatamshi na kuongezewa mfumo wa Kiswahili wa “tia,” ambao haupo kwenye Kiingereza.

Ila mtindo ulioshika sasa ni kufuata moja kwa moja mfumo wa Kiingereza, “saini” kama katika “alisaini mkataba.” Sisemi kwamba ni kosa, ila nahofia kwamba tumehama kutoka kwa Kiswanglish hadi kwa Kiinglish-swa, yaani muundo wa Kiingereza kutawala.

Ndio maana tunakuwa na tafsiri za ajabu za “harvesting sand” kuwa “kuvuna mchanga” katika vyombo vyetu vya habari. Nikidhani katika utaratibu wa Kiswahili mtu huvuna alichopanda tu? Mbona nafikiri neno mwafaka ni “kuzoa mchanga?” Huko kuvuna mchanga ni Kiinglish-swa kinachokipa umbele Kiingereza.

Kiswahili kinalazimishwa kusalimu amri ya Kiingereza. Si udhaifu huu?

You can share this post!

Masuala yaliyofuatiliwa na Wakenya katika Google Search...

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wajadili ufaafu...

adminleo