KINA CHA FIKIRA: Ukitumia mawazo yako vyema basi utakuwa mwema
Na WALLAH BIN WALLAH
AKILI ni nywele na kila mtu ana zake.
Kila binadamu akizitumia akili zake vizuri, zitampeleka pazuri. Akizitumia vibaya, zitampeleka kubaya!
Watu waliowahi kuyatenda mambo mema ya uadilifu duniani, walitumia akili zao vizuri kuyatenda matendo mema wakawa watu wema! Kila mtu ni dereva wa kuongoza mawazo yake na akili zake kuelekea anakotaka anavyotaka! Huo ndio ukweli!
Katika shule ya upili Tukotukae, wanafunzi arubaini wa kidato cha nne walikuwa uwanjani kucheza wakati wa mapumziko! Mwanafunzi aitwaye Kijamajani akaokota pochi yenye pesa noti za Kenya shilingi elfu kumi. Waliporudi darasani alimwomba mwalimu wa darasa Bwana Sampuli idhini ya kutoa tangazo fupi! Mwalimu alipomruhusu, Kijamajani alitangaza, “Ndugu zangu, nimeokota pochi tulipokuwa uwanjani! Aliyepoteza pochi yake ajitokeze nimpe! Lakini ataje ina shilingi ngapi na kitu gani kingine?!”
Kila mtu alijishikashika pia Mwalimu Sampuli ambaye kwa kweli hakuwa uwanjani!! Mara mwanafunzi aitwaye Ndiyenao alinyanyuka akasema, “Ni pochi yangu! Ina shilingi elfu kumi na karatasi nyeusi!” Kijamajani aliridhika akachomoa pochi akampa Ndiyenao! Wanafunzi wote walicheka kwa kejeli kuona Kijamajani karudisha pesa za kuokota kwa mwenyewe!!?
Hapo mjadala ukatokea darasani kuhusu kitendo cha Kijamajani kurudisha pesa alizoziokota! Wanafunzi wengine waliamini Kijamajani alikuwa mjinga sana! Wengine wakasema, “Huyo hajui pesa!” Wengine wakasema, “Amepoteza zawàdi na bahati yake kutoka kwa Mungu!” Hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyeunga mkono wala kupongeza kitendo cha Kijamajani kutangaza pesa alizookota! Ndiyenao mwenye pesa alisimama akasema, “Tumwacheni mjinga huyo atakufa maskini! Hajui kwamba cha kuokota si cha kuiba! Hakuniibia!”
Wanafunzi walipomwomba Mwalimu Sampuli atoe maoni yake, alisema, “Leo nimeamini kuwa ninawafundisha wajinga na wapumbavu ambao hata wakipata bahati na fursa hawawezi kutumia!” Lakini Kijamajani hakujuta wala kusikitikia kitendo chake cha kumrudishia Ndiyenao pesa! Alifurahi moyoni!
Miaka kumi na mitano baadaye Bwana Kijamajani alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni iliyosifika ya kusafisha gesi nchini! Wenzake wale waliomkejeli darasani pia walihitimu wakaajiriwa kufanya kazi kubwa kubwa nchini. Bwana Sampuli alipandishwa cheo akawa Mwalimu Mkuu wa Tukotukae! Siku moja Kijamajani aliona habari zikitangazwa, “Mwalimu Mkuu wa Tukotukae Bwana Sampuli amehukumiwa kufungwa gerezani miaka ishirini kwa kuiba pesa za shule!” Mwalimu huyo alipopelekwa katika gereza la Mashimoni, alishtuka kuwapata wanafunzi wake wale waliomkejeli Kijamajani korokoroni wamefungwa kwa wizi na ufisadi!
Kijamajani anajiuliza,”Tutajifunza uaminifu na uadilifu kutoka kwa nani kama si kwa wazazi au walimu ama kutoka kwa mimi na wewe?”
Naam, ukitumia mawazo yako vyema kama Kijamajani utakuwa mtu mwema!