KINA CHA FIKIRA: Walimu wa Kiswahili daima tufanye utafiti tuepuke kujiumbua
Na KEN WALIBORA
KATIKA kikundi kimoja cha mtandaoni mtu ameuliza, “Neno Bomet lina silabi ngapi?” Hili karibu lifanane na lile swali ambalo wengi hupenda kuuliza kuhusu ngeli ya maiti. (Niachie nichepuke kidogo kwa kusema kwamba kifo cha Gavana wa Bomet, Joyce Laboso kimesadifiana na uandishi wa makala haya, hivyo sina budi kusema makiwa kwa watu wa Bomet).
Wanachama wa makundi haya huwa aghalabu ni walimu wanaotarajiwa kubobea katika Kiswahili.
Hawa ndio hubebeshwa mzigo mzito wa kuwafundisha wanafunzi Kiswahili katika asasi zetu za elimu, si shule za msingi, si sekondari si vyuoni.
Je, mwalimu wa Kiswahili anapaswa kuuliza au kuulizwa zipo silabi ngapi katika neno Bomet? Au swali hili halijuzu kuulizwa katika taaluma za Kiswahili kwa vile neno Bomet, si neno la Kiswahili ni neno la Kikalenjin?
Baadhi ya washiriki wa mdahalo walibisha sana wakisema hilo swali si mwafaka kwa sababu halihusu msamiati wa Kiswahili.
Yaani kwa maana nyingine, dhana ya silabi kama vile dhana nyingine za sarufi na isimu, haipaswi kutoka nje ya mipaka ya Kiswahili.
Je, hilo linaingia akilini, yaani wanaosomea Kiswahili wajue tu kutambua na kuhesabu idadi ya silabi katika maneno ya Kiswahili, tusiwabebeshe mizigo ya maneno ya kwingineko?
Je, wanafunzi wa Kiswahili wafungiwe katika jela ya Kiswahili wasijue lolote nje hata lile lisilohusu Kiswahili tu bali lugha nyingine?
Au lugha nyingine duniani hazihusiani na neno au dhana hii ya silabi?
Haya ndiyo maswali yaliyolewalewa akilini mwangu huku mdahalo ukiendelea kwenye jukwaa hilo la mtandaoni.
Lililoshangaza zaidi ni pale baadhi ya washiriki walipoanza kudai kwamba neno Bomet lina silabi mbili yaani Bo-met.
Hapo ndipo niliona mwalimu wa uzoefu mkubwa Chesebe, (Siku hizi rasi wa Shule ya Sekondari ya Tenwek) akiuliza: kwani maana ya silabi imebadilika?
Swali hilo la gwiji huyu lilionyesha kushangazwa kwake na mkondo wa swali na mdahalo.
Hata mimi nilikuwa sina budi kujiuliza mwenyewe, je, dhana silabi imepata mapindukizi makubwa au nini? Mbona naona silabi tatu hapa- yaani Bo-me-t.
Kubwa zaidi swali kama hili linapotoka kwa mwalimu wa Kiswahili na jibu la silabi mbili linapotoka kwa mwalimu au walimu wa Kiswahili, tunapata taswira gani kuhusu hali ya Kiswahili nchini? Pema hapo?
Unatarajia kwamba walimu wa Kiswahili watakuwa na maafikiano ya moja kwa moja kuhusu ukweli huu wa kisayansi—maana silabi ni dhana ya kiisimu na isimu ni sayansi ya lugha kama Dkt Basilio Mungania alivyonifundisha barabara katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Ni kweli kwamba wataalamu wa Kiswahili, wakiwemo walimu na wahadhiri, wanapaswa kuwa wanafunzi wa daima wa Kiswahili. Hakuna mwisho kwa kujifundisha na kujifunza mambo mapya.
Hata hivyo mambo mengine ni ya msingi sana. Endapo mwalimu bado anatapatapa kubaini nini silabi sharti tuingiwe na wayowayo kuhusu ubora wa ufundishaji.