Makala

KINAYA: Corona na makali yake ya kukeketa, imetufunza kudumisha usafi wetu

March 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

MAMBO yakiendelea yanavyokwenda, inaonekana ugonjwa huu wa coronavirus ndio utakuywa tiba ya taabu ambayo imeniudhi kwa muda mrefu.

Vipi tena ugonjwa ukawa tiba? Tega sikio nikueleze. Nenda kanawe mikono kisha ukalie jamvi nikupe mawili-matatu.

Je, umewahi kuudhika na watu fulani mtaani ambao huchokonoa pua zao kwa vidole vyao, kisha kukunyooshea mkono uwasalimu?

Hao, na hapa nasema bila kificho, hawana bahati! Tangu hapo mtu huyo nikimpa ngumi tu, alete yake zigongane, mwisho wa salamu uwe huo!

Naweza kuhesabu watu watatu hivi niliokua nao tangu utotoni, sasa tunakaribia kuitwa babu, lakini sijawahi kuwapa mkono wangu.

Kisa na maana? Wakipenda kutumia viganja vyao kufutia ukamasi, tabia ya kuchukiza hivi kwamba ilinipa kichefuchefu. Hao wakila kwa mikono wanaramba kila kidole!

Ikiwa umekuwa ukiwasalimu watu kwa mkono shingo-upande, umepata kisingizio cha kuwaambia waridhike na kupungiwa mkono kwa mbali, kisa coronavirus.

Najua ni maradhi, na kwamba hatupaswi kushangilia chochote, lakini, samahani mwenzangu, sitashika tama kwa ajili ya ugonjwa wa mchipuko. Utakwisha tu.

Nitatumia fursa hii kukukumbusha majukumu yako katika shughuli nzima ya kudumisha afya ya jamii, maradhi yawepo yasiwepo.

Anza kwa kukataa salamu za mkono. Hivyo utaepuka kushika mate ya watu ambao hutumia kucha zao kuchokonoa meno badala ya kichokonoo baada ya kula nyama.

Wajibika kwa kumkomesha yule rafiki yako ambaye, japo ana kitambaa mfukoni, anaziba pua moja na kupuliza makamasi nje kwa jingine, kisha kufuta mkono kwa kitambaa chenyewe.

Mkomeshe mwenzako ambaye habebi kalamu, hukuomba yako kila wakati, na mara tu akimaliza kuitumia huitoa kifuniko na kukitumia kukuna masikio yenye mwasho wa ugaga wa mwaka jana!

Pia, usimsaze yule aliyezoea kutoa matongo machoni kwa kutumia vidole, kisha akimenya chungwa au mhogo hukupa kipande kabla hujamuomba.

Ukiangalia ugonjwa wa coronavirus unavyosambaa kwa kasi, utatambua kwamba duniani kuna watu ambao wamekuwa wakilisha wengine uchafu wao.

Zingatia kwamba maambukizi ya ugonjwa wenyewe ni kupitia ama mate, makamasi au machozi. Huambukizwi kwa kupumua hewa aliyopumua mgonjwa.

Hii ina maana kwamba hadi uyaguse mate au machozi ya mgonjwa kisha ujiguse popote usoni hauwezi kuambukizwa. Inaonekana tumekula uchafu kwa muda sasa.

Ukizingatia kwamba si wote walioambukizwa ambao walibusiwa na wapenzi wao, unajijazia kuwa waliupata kupitia desturi zisizo za kistaarabu.

Niliudhika zaidi nilipohamia Amerika yapata miaka minane iliyopita pale nilipomwalika mtu nyumbani ashiriki nasi chakula cha mchana.

Baada ya kula na kushiba kiasi cha kucheua, alichukua karatasi ya kupangusia mikono iliyokuwa mezani, akachemua sawasawa na kutoa makamasi mazito!

Kisha? Akaikunja ile karatasi na kuiweka ndani ya sahani aliyokuwa amelia, akanyanyuka na kuipeleka sahani pamoja na uchafu wake huo jikoni.

Ulivyokisia ni kweli: Sijawahi kumwalika tena kwa sababu alinisababisha kutapika sana mpaka kifua changu kikauma.

Usiwe mshamba mchafu; zingatia kanuni za kimsingi za afya, utaepuka coronavirus.

 

[email protected]