• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Kinaya nduguye Monicah kumtaka Jowie kupasha wanahabari mauaji aliyotekeleza

Kinaya nduguye Monicah kumtaka Jowie kupasha wanahabari mauaji aliyotekeleza

NA RICHARD MUNGUTI

ILIKUWA ni kinaya kwa George Kimani kumsihi Joseph Irungu almaarufu Jowie amsaidie kuarifu vyombo vya habari mauaji ya kinyama ya dada yake Monicah Kimani bila kufahamu ndiye aliyetekeleza mauaji hayo.

Kifo cha Monicah kilisambaratisha biashara yake nchini Sudan Kusini na kuletea familia yao uchungu mwingi watakaoishi nao milele.

Katika ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia Bw Andrew Kanyutu aliyomkabidhi Jaji Grace Nzioka, familia ya marehemu Monicah na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wameomba Jowie ahukumiwe kifo.

Lakini wazazi wa Jowie pamoja naye wamedumisha msimama hakuua.

Wanakijiki wa Ngata, Nakuru alikozaliwa Jowie, na Askofu Shadrack Oloo wa Kanisa la Agape Sanctuary ambalo mshtakiwa alikuwa akishiriki ibada, walimtolea ushuhuda kwamba “ni kijana msikivu na mtiifu anayejitolea katika kazi ya kanisani kama mwanakwaya na mcheza gitaa.”

Lakini Naibu Mkurugenzi katika afisi ya DPP, Gikui Gichui, akitoa mawasilisho yake kuhusu adhabu dhidi ya Jowie alisema Serikali ilithibitisha kabisa Jowie ndiye aliyemuua Monicah kwa kumchinja kama mnyama wa mwituni hivyo basi anastahili kupata adhabu ya kifo.

Bi Gichuhi alieleza Jaji Grace Nzioka atakayesoma hukumu ya Jowie mnamo Machi 13, 2024, kwamba Monicah alikufa kifo cha uchungu mwingi ikitiliwa maanani alifungwa mikono na miguu, kisha akapelekwa bafuni na kuchinjwa kwa kisu.

Baada ya kumtoa uhai Monicah, Jowie alifungulia maji ya mfereji kwenye karai kwa lengo la “kupotosha watu Monicah alikuwa anaoga.”

Mahakama ilielezwa Jowie alikuwa na nia na lengo la kuficha kisa hicho na kujitenga na uhalifu.

Joseph Irungu almaarufu Jowie (kulia), ambaye alipatikana na hatia ya kumuua Monicah Kimani, akiwa katika mahakama ya Milimani mnamo Machi 8, 2024. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Ushahidi uliotolewa mbele ya Jaji Nzioka ni kwamba Jowie alikuwa ameiba kitambulisho cha mtu mwingine alichokiacha katika lango la kuingia makazi ya Monicah.

Alikuwa amevalia kanzu inayopendelewa na Waislamu alipoingia katika makazi ya Monicah.

Baada ya kumuua Monicah, ushahidi ulisema alichoma kanzu hiyo na kujipiga risasi begani kujifanya alishambuliwa na majambazi katika lango la Royal Park Estate, Lang’ata ambapo alikuwa akiishi na mtangazaji Jacque Maribe ambaye wakati huo alikuwa akifanyia kazi kituo cha runinga cha Citizen.

Yeye na Maribe walitoa habari za uwongo kwa polisi kwamba alishambuliwa na majambazi lakini ukweli ukachipuka alijiumiza mwenyewe ndani ya nyumba yao na Maribe walipokuwa wanalipa kodi ya Sh65,000 kila mwezi.

Jaji Nzioka alielezwa na Bi Gichuhi kwamba Monicah licha ya kwamba alishapoteza maisha, anastahili kutendewa haki.

Kiongozi huyo wa mashtaka aliomba mahakama ijikakamue na kumtendea Monicah haki kwa vile “hakustahili kufa jinsi ile bila ya kumchokoza au kumkera ama kumuudhi Jowie kiwango cha kufanya hasira yake ichemke vile na kulipuka jinsi hiyo.”

Bi Gichuhi alisema picha za jinsi Monicah alivyoshambuliwa ni za kuhuzunisha mno na huacha yeyote anayezitazama akipata jinamizi.

“Naomba hii mahakama imtendee Monicah haki, aliteswa, kudhulumiwa na hatimaye akakatwa shingo mithili ya kumchinja mnyama,” Bi Gichuhi alisema katika mawasilisho yake kabla ya adhabu kupitishwa.

Jaji Nzioka aliombwa atilie maanani ripoti ya Dkt Peter Ndegwa aliyeifanyia maiti ya Monicah upasuaji ili kufikia uamuzi wa haki.

Baba yake marehemu, Askofu Paul Kimani Ngarama, alieleza Bw Kanyutu kutoka Amerika anakoendelea na masomo ya Shahada ya Uzamifu katika somo la Saikolojia ya Ushauri na Theolojia kwamba “kifo cha Monicah ni donda ndugu kwa familia yake.”

Askofu Ngarama aliomba mahakama itende na kutekeleza haki na kupitisha adhabu inayofaa na kunukuu Biblia–Mithali 11:21 inayosema: “Hakika mwovu hatahepa kuadhibiwa, lakini waadilifu watakolewa.”

Mama yake Monicah aliugua kiharusi baada ya kupashwa habari za kifo cha bintiye.

Akiangua kilio wakati wa mahojiano na Bw Kanyutu, mama yake marehemu aliuliza: “Je, Monicah alistahili kuuawa kwa njia ya kikatili na kinyama hivyo?”

Nduguze Monicah–George na Solomon Njoroge–waliokuwa wakifanya biashara naye Sudan Kusini wangali wanagubikwa na wimbi la simanzi hata leo hii, ikiwa ni miaka minne baada ya dada yao kuuawa.

George aliyesoma na Jowie katika chuo cha Kenya Polytechnic alifichua kwamba mshatakiwa ni mtu mwenye hasira kali na mkorofi.

“Kesi ikiendelea alinifungia njia nikiendesha gari. Anastahili adhabu inayomfaa,” akasema George.

Nduguze marehemu walisema biashara yao ilisambaratika hata ikabidi warudi Kenya na familia yao iliathirika kiuchumi.

“Solomon aliacha kutazama habari za runinga tangu vyombo vya habari vipeperushe habari za mauaji ya kinyama ya dada yao waliyemtegemea kwa kila hali,” Bw Kanyutu alifichua katika ripoti yake.

Majirani wa familia ya marehemu walighadhabishwa na mauaji hayo ya kinyama na wakaomba mahakama imwadhibu ipasavyo Jowie.

Walipohojiwa, wazazi wa Jowie walisema mwana wao mwenye umri wa miaka 33 ni msikifu na mwenye kujitolea katika imani ya Ukristo.

Askofu Oloo wa Kanisa la Agape Sanctuary, Nakuru aliambia Bw Kanyutu kwamba Jowie ni muumini anayejitolea katika kazi za pale Kanisani akiwa mwanakwaya, mcheza gitaa na mwimbaji hodari.

Siku ile alipatikana na hatia alitoa  wimbo wa kidini kwa jina ‘Nishikilie’.

Wakazi wa eneo la Nguta, Nakuru ambapo alikuwa akiishi na wazazi, walisema Jowie ni mvulana mwadilifu lakini “walishtushwa na habari kwamba ndiye aliyemuua Monicah Kimani kiunyama”.

La kushangaza ni kwamba Jowie ameendelea kukana alimuua Monicah licha ya ushahidi wote kwamba “ni yeye alikuwa wa mwisho kuwa na Monicah baada ya kuachwa akiwa naye usiku wa Septemba 19, 2018, katika makazi yake akiwa amevalia kanzu.”

Akitamatisha ripoti yake, Bw Kanyutu alimsihi Jaji Nzioka atoe uamuzi wake “akitilia maanani ushahidi wa familia zote.”

Sasa kazi ni kwa Jaji Nzioka aliyemwamuru wakili Prof Hassan Nandwa anayemtetea Jowie, awasilishe ushahidi wake wa mwisho ifikapo Machi 11, 2023, ndipo atoe adhabu yake.

Matarajio ni kwamba haki itapatikana.

  • Tags

You can share this post!

Mabadiliko yaashiria anayeweza kuwa Mkuu mpya wa Majeshi...

Walimu wasio na kazi wasubiri TSC itangaze nafasi 20,000

T L