Makala

Kindiki ageuza kijiji chake Irunduni kutoka kilichochakaa kuwa kitovu cha mikakati ya ‘Tutam’

Na GITONGA MARETE, GEORGE MUNENE September 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIEZI michache iliyopita kijiji cha Irunduni kilikuwa eneo lililochakaa katika kata ya Mukothima Kaunti ya Tharaka Nithi.

Lakini tangu kuteuliwa kwa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais, kijiji hiki ambacho ni nyumbani kwake, kimebadilika na kuwa kitovu cha shughuli za kisiasa.

Hapa, mikakati ya kisiasa inatungwa na kutekelezwa, katika namna inayoshahibiana na Wamunyoro, nyumbani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika eneo bunge la Mathira

Baada ya kutimuliwa afisini Oktoba 18, 2024, Bw Gachagua aligeuza makazi yake kuwa eneo la kuwapokea wanasiasa kutoka maeneo mbalimbali nchini, kujadili na kupanga mikakati.

Sasa Profesa Kindiki amegeuza kijiji cha Irunduni kuwa kitovu cha kupanga mikakati yake ya kukomboa eneo la Mlima Kenya kutokana kwa udhibiti wa kisiasa wa Bw Gachagua.

Wakati huu wajumbe wanamiminika katika kijiji hiki kujadili siasa za kitaifa.

“Tunafurahi kuwa mtoto wetu amekiweka kijiji chetu katika ramani ya kitaifa. Tumeahidiwa kuwa barabara ya lami itajengwa hivi karibuni hadi katika boma la Profesa Kindiki,” akasema Bw Patrick Mugao, mkazi.

Ndani ya miezi mitatu iliyopita, Profesa Kindiki amekutana na zaidi ya wakazi 20,00 kutoka maeneo mbalimbali ya Mlima Kenya. Watu hao wanajumuisha vijana, wanawake, wasanii na viongozi wa kisiasa.

Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri pia anaongoza kundi la wabunge wanaoendesha juhudi za kurejesha imani ya wakazi kwa serikali ya Rais Ruto.

Kufikia sasa Profesa Kindiki amekutana na makundi ya wanawake, vijana, wanamichezo, wanafunzi wa vyuo viku na wafanyabiashara kutoka kaunti za Tharaka Nithi, Embu, Meru miongoni mwa zingine.

Wanasiasa huwa hawahusishwi katika mikutano ya makundi yasiyoshirikisha wanasiasa, mkakati unaolenga kuongezwa juhudi zinazoendeshwa na viongozi waliochaguliwa.

“Nimewahi kuhudhuria mikutano ya viongozi wa mashinani inayolenga kupokea habari kutoka kwa wananchi, malalamishi yao na mapendekezo yao kuhusu namna ya kuendeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali wakati huu,” Bw Mugao akasema.

Wakati wa vikao kama hivyo, Profesa Kindiki pia hupata nafasi ya kunadi ajenda za serikali ya Rais Ruto na kutoa hakikisho kwa wakazi kuwa ahadi za Rais zitatekelezwa.

Ni katika majukwaa kama hayo ambapo Naibu Rais alisema atawatetea wabunge kutoka Mlima Kenya wanaposhambuliwa na wafuasi wa Bw Gachagua.

Akiwahutubia zaidi ya wanawake 3,000 nyumbani kwake Irunduni mnamo Agosti 27, 2025, Profesa Kindiki alisema utawala wa Rais Ruto uko tayari kutekeleza ahadi zote za maendeleo kwa manufaa ya raia.

Profesa Kindiki alisema atawajibikia miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika kaunti hiyo ya Tharaka Nithi na zingine katika eneo pana la Mlima Kenya.

“Kuanzia sasa msiwaulize wabunge wenu kuhusu miradi ya barabara ambayo haijakamilishwa. Nitakuwa nikijibu maswali kuhusu miradi yote inatekelezwa na serikali ya kitaifa hapa katika kaunti ya Tharaka Nithi,” akaeleza.