Makala

Kinyozi Jose Jay atwaa taji la Next Superstar Kenya, avuna Sh1M

Na WINNIE ONYANDO September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KINYOZI na mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka mtaa wa Donholm jijini Nairobi, Jose Jay (Joseph Japheth), ameibuka mshindi wa kwanza wa shindano la Next Superstar Kenya lililokamilika Jumapili usiku katika ukumbi wa Charter Hall, Nairobi.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alituzwa zawadi ya Sh1 milioni, baada ya kuwashinda wengine sita waliokuwa wakishindana katika fainali iliyotangazwa mubashara kupitia Runinga ya Rembo TV, Rembo Plus na kwenye mtandao wa StarTimes ON.

Shindano hilo lililoendeshwa kwa wiki 14 tangu Mei 2025, lilianza na maelfu ya vijana wakijitokeza na kuchujwa.

Jose Jay aliwashinda Brenda Morii, Albert Okumu, Andy Saharan, Jambia (Brian Koome) na Rennic (Rennick Nzalwa). Rennic alichukua nafasi ya pili na kujinyakulia pikipiki mpya, huku Jambia akimaliza nafasi ya tatu na kutuzwa Sh 150,000.

Majaji wa shindano hilo walikuwa msanii King Kaka, mwimbaji Size 8 na Motif Di Don, waliomsifia Jay kwa umahiri wa sauti na wimbo wake uliowavutia mashabiki.

Akizungumza baada ya ushindi wake, Jay alisema:

“Nimejaribu mashindano mengi ila sikuwahi kuibuka wa kwanza. Safari hii nilijipa moyo kujaribu tena. Namshukuru Mungu kwa kunijibu. Muziki ni maisha yangu, na nitauendeleza daima.”

Mkurugenzi wa Mipango katika Tume ya Filamu Kenya, Bw Collins Okoth, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisifu shindano hilo akisema:

“Zaidi ya asilimia 70 ya wasanii nchini ni vijana. Serikali inawekeza katika sera na miundombinu ili sekta ya ubunifu iwe kitegauchumi. Ubia kama huu na StarTimes huwapa vijana nafasi ya kuona sanaa kama taaluma na biashara.”

Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa StarTimes, Bw Jimmy Carter Luoh, alitangaza kuwa shindano hilo litakuwa la kila mwaka kwa kipindi cha angalau miaka kumi ijayo.

“StarTimes sasa itachukua jukumu la kuwekeza katika vipaji vya ndani. Next Superstar Kenya imethibitisha kuwa Kenya ina wasanii.”

Fainali hiyo ilioendeshwa na Amina Rabar na mchekeshaji Eddie Butita.