KIPAJI: Mwalimu anayetumia talanta ya uimbaji kukuza wale chipukizi
Na SAMMY WAWERU
BI Annastacia Mitau ni mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za Injili.
Mwanamuziki huyu kutoka kijiji cha Ngaa, Kaunti ya Kitui, anasema nyimbo zake ni ujio kupitia maandiko ya Biblia.
Ni kipaji alichotambua kujaaliwa akiwa katika shule ya msingi ambapo alitungia wanafunzi wenza nyimbo, na kuwapa waimbe na kutumbuiza, hasa katika gwaride na hafla zilizoandaliwa.
Katika shule ya upili, St Ursula Tungutu iliyoko Kitui, Annastacia anasema aliendelea kupalilia kipaji chake katika usanii wa uimbaji, akidokeza kuwa akiwa kidato cha tatu alichaguliwa kuwa kiongozi wa michezo ya kuigiza na muziki.
Anafichua kwamba aliimba nyimbo za Kiislamu; Taarabu na Kaswida pia Qaswida, ambapo alishiriki mashindano yake hadi katika daraja la kitaifa. “Hata ingawa sikuibuka kidedea, nilikabidhiwa vyeti kadhaa,” asema mwanadada huyu.
Alipohitimu elimu ya shule ya upili mwaka 2009 alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mosoriot, kilichoko Kaunti ya Nandi mwaka wa 2010 na aliendelea kubobea katika muziki.
“Uimbaji na utumbuizaji wowote chuoni nilikuwa katika mstari wa mbele,” anasema Annastacia.
Alikamilisha kusomea taaluma ya ualimu 2012.
Annastacia ambaye ni mama wa mtoto mmoja, ameimba nyimbo zake kwa lugha ya Swahili na Kikamba. Ana albamu moja yenye nyimbo sita; Mbiwie tei – ninakupenda Mungu, Neema, Niseng’ete – nimeshangaa, Lyikie vinya – jitie nguvu na Ninukilitye wasya – nimeinua sauti.
Kulingana na mwanamuziki huyu serikali ya kaunti ya Kitui kupitia wizara ya michezo, vijana na turathi ndiyo imemfadhili kurekodi zake.
Sauti (audio) alirekodi mwaka 2018 na video akiifanya mwaka huu, 2019, kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti ya Kitui inayoongozwa na gavana Charity Ngilu.
Mbali na kuwa muimbaji, Annastacia ni mwalimu wa Somo la Hisabati na Kiingereza katika shule ya Msingi ya Kibinafsi na ya Bweni ya St Gabriel, Mwingi. Anasema amefanikiwa kubuni kilabu ya Muziki, Sanaa na Uigizaji shuleni humo.
“Niliteuliwa kiongozi wa kilabu hiyo. Kwa sasa ninajivunia mwanafunzi mmoja wa darasa la nne, ambaye amejaaliwa kipaji cha uimbaji. Anaendelea kutunga nyimbo na akitokota nitamsaidia kuingia studioni azirekodi,” asema, akiongeza kwamba ana orodha ya wanafunzi kadhaa ambao wakipaliliwa wataibuka kuwa wanamuziki wa kupigiwa upatu.
Anachozingatia kwenye mafunzo kupitia vipindi anavyoandaa ni utunzi wa nyimbo, sauti, namna ya kuimba, ujasiri kwa wanafunzi pamoja na vigezo muhimu katika ulingo mzima wa uanamuzi.
Nephat Mbau, ambaye ni produsa, anasema vipaji chipukizi wakipaliliwa wakiwa wangali wachanga wataibuka kuwa miongoni mwa wasanii bora nchini. “Cha muhimu zaidi ni upekee katika utunzi, sauti na ujasiri hususan wakiwa jukwaani. Msanii chipukizi akinolewa akiwa mdogo, ataishia kubobea siku za usoni na kuwa nguzo za wajao,” aeleza mweledi huyu.
Akipongeza hatua ya Annastacia, Bw Mbau anasema wasanii wengine wakiiga nyayo zake sekta ya uamuziki nchini itaimarika kwa kiasi kikubwa.
Changamoto
Changamoto kuu inayogubika wasanii chipukizi ni ukosefu wa hela kuingia studioni. Pia, kupata jukwaa kupromoti nyimbo haswa kwenye vyombo vya habari kama vile redio na runinga, ni pandashuka nyingo.
“Nyimbo za waimbaji chipukizi kuchezwa kwenye vyombo vya habari ndicho kizungumkuti kikuu. Lazima mmoja awe watangazaji anaofahamu na wenye moyo wa kusaidia,” asema Annastacia Mitau.
Isitoshe, kuna baadhi ya vyombo vya habari vinavyocheza nyimbo zao na kukosa kuwalipa, vingine vikizitumia kuimarisha biashara zao, matangazo.
Akizungumza katika mazishi ya mwanamuziki tajika wa benga John Mwangi Ng’ang’a maarufu kama John Demathew, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuangazia masaibu yanayofika waimbaji nchini.
Kiongozi wa taifa pia aliagiza ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, DPP Noordin Haji na mwenzake wa uhalifu na jinai, DCI George Kinoti kuchunguza muungano wa nyimbo nchini, MCSK kufuatia madai ya kunyanyasa wanamuziki.