Makala

KIPAWA NA UBUNIFU: Jinsi ya kugeuza viatu vikuukuu kuwa 'dhahabu'

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMUEL BAYA

JE, ndugu msomaji, umewahi kufikiria au kufahamu kwamba viatu vikuukuu au sandali unazoziona zikiwa zimetupwa jaani au baharini zinaweza kuundwa bidhaa za kuvutia.

Kuna uwezekano hutaelewa jambo hili hadi utakapokutana na Bw Juma Kilonzi.

Mwanasanaa ambaye hutumia viatu vikuukuu na uchafu wa platiski ufuoni Bw Juma Kilonzi akionyesha mfano wa mamba na wanyama wengine ambao hutengeneza kwa viatu vikuukuu. Picha/ Samuel Baya

 

Yeye ni mjuzi wa kuunda bidhaa mbalimbali kupitia kwa viatu vikuukuu vya plastiki na takataka nyingine anazopata ufuoni.

Kwa zaidi ya miaka 10 jamaa huyu amekuwa akishughulika na ujuzi huu wa kutumia takataka ambazo zimetupwa na kugeuza kuwa sanamu na bidhaa za kupendenza.

Hiyo ndiyo kazi ambayo pia inampatia riziki yake na tulipokutana naye katika eneo la Dabaso, Watamu,katika kaunti ya Kilifi, alikuwa na bashasha tele.

“Nilianza shughuli hizi zaidi ya miaka 12 iliyopita nilipokuwa nikiuza vinyago katika ufuo wa bahari wa Watamu. Na hapo ndipo nilipokuwa nikiona viatu na takataka nyingi za bahari zilikuwa zimetapakaa na kuwaua kasa wa baharini. Nakumbuka kuna wakati tulizika kasa watatu ambao walikuwa wamenyongwa na takataka baharini,” anaeleza Bw Kilonzi.

Hapo ndipo mawazo yalimjia ya kuamua kuhakikisha kwamba takataka hizo ambazo zilikuwa nyingi sana baharini zinaweza kutumika kufanya tena bidhaa ambazo zinaweza kutumika tena.

“Nilifikiria vile ninaweza kutumia hizo takataka kuunda vitu ambavyo vinaweza tena kutumika. Hapo nakumbuka kwamba nilianza kazi ya kuokota viatu vilivyotupwa na nilifaulu kujaza gunia zima la viatu vilivyoharibika,” akasema.

Anaongeza kwamba baada ya kuokota na kujaza magunia kadhaa ya viatu vikuukuu na uchafu mwingine wa plastiki kwa miezi sita, alipata suluhisho la kuanza kutengeneza vito vya kuvutia.

“Hapo ndipo nilianza kutengeneza vitu vingi. Mimi huunda wanyama wa baharini kama vile mamba na samaki. Vilevile hutengeneza sanamu za vifaru, twiga. Ninatengeneza wanyama wa kila aina na ninafurahia kazi yangu inavutia mno,” akasema Bw Kilonzi.

Baada ya kuimarisha ujuzi wake, Bw Kilonzi alisema sasa ameelekeza juhudi zake katika kuwafundisha wakazi wa Dabaso jinsi ambavyo wanaweza pia kutumia takataka za baharini kutenengeza bidhaa zitakazo wasaidia.

“Ninapounda bidhaa zangu, huuza katika maduka ya kunadi nguo kwa watalii ufuoni maarufu kama boutique. Lakini kwa sasa pia nimeamua kuwafundisha wakazi jinsi ambavyo wanaweza kujichumia riziki kupitia kwa kuunda kama vile vipuli na shanga. Muhimu ni kuwapa njia ya kujikimu,” akasema.

“Kwa mfano ninapotengeneza mamba, kuna yale mabaki ambayo nina wafundisha jinsi ya kutengeneza mikeka, kwa hivyo uchafu baharini utapungua,” akasema

Hapo Watamu Eco World, Bw Kilonzi amemleta mamba ambaye alimuunda kutokana na viatu hivyo vikuukuu.

Mbali na mfano huo wa mamba, ana pia vidubwasha vya kuwekea funguo ambavyo pia viliundwa maridadi kwa kutumia sandali zilizokuwa zimetupwa.

“Huyu mamba ninauza Sh5,000 na hizi shanga ninauza kwa Sh400 na pia ninawafundisha akina mama jinsi ya kuunda shanga. Lengo langu ni kuhakikisha kwamba kila mtu aweze kujua kutengeneza peke yake ili akileta hapa kituoni au kwenye boutique, awe ataendeleza maisha yake,” akasema wakati huo.

Manufaa

Kwa sasa Bw Kilonzi ni mmoja wa wasanii wa kuunda bidhaa hizo katika kituo hicho cha Eco World na anasema kuwa biashara hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwake.

“Biashara hii imenisaidia sana kwa sababu nikiangalia kwa makini hakuna kazi sasa. Awali nilikuwa nikiuza vinyago baharini na nikaona kazi ya vinyago imeisha ndipo nilipoingilia kazi hii ya kuunda bidhaa hizi. Hakuna kazi zengine na kwa hivyo niliingia moja kwa moja kujikimu hapa,” anasema Bw Kilonzi.

Msanii huyo alisema kuwa ingawa kuna wengine pia wameanza kuingilia kazi hiyo bado anaendelea kusonga mbele.

“Nina umri wa miaka 55 na ni baba wa watoto wanne na mjukuu mmoja. Kuna baadhi ya watoto wangu ambao bado wako shuleni za Sekondari na ninawalipia karo kupitia kwa kazi hii,” akasema.

Sawa tu na kazi nyingine zozote, changamoto daima huchipuka mara kwa mara, hasa uhaba wa mali ghafi ambazo ni takataka.

“Changamoto kubwa ipo kwenye mauzo ya bidhaa hizi kwa sababu bado sijafanikiwa kuuza katika maduka mengi.”

Wakati biashara inakuwa nzuri, yeye hupata hata zaidi ya Sh10,000 lakini anasema kuwa yote yatategemea ana mitandao ya maduka mangapi.