KIPWANI: Azma kuu ni kuinua vipaji vichanga Pwani
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
NIA yake kubwa kwenye tasnia ni kuhakikisha mafanikio yake yamewafaidi wanamuziki wengine.
Yusuf Shora al-maarufu MC Shora Junior alipoamua kuwa mwimbaji, nia yake kubwa ilikuwa ni kuinua kipaji chake kitakachomwezesha kuwasaidia wasanii chipukizi wa Pwani ambao wamekosa wafadhili.
“Sikujitosa kwenye fani hii kwa ajili ya utajiri wa kupindukia kama walivyo wasanii wengine watajika katika kanda hii ya Afrika Mashariki. La! Nataka niwe na kipato ambacho asilimia fulani itakuwa ni mchango wangu wa kuwainua wenzangu wanaotapatapa,” asema.
Ulianza kuimba lini, upi wimbo wako wa kwanza na uliitikiwaje?
Shora Junior: Nilianza kuimba mwaka 2010, na kuachia Platform, kibao kilichoitikiwa vizuri si haba maana na kilinisaidia kuanzisha mradi Platform na produsa Magustu Babu ili kuwasaidia wasanii chipukizi.
Kwenye mradi wenu huo, munawasaidiaje wasanii wenzenu?
Shora Junior: Tuna studio yetu ya Mk2 Music na hutoza ada nafuu kurekodia wasani chipukizi wasio na uwezo. Na japo malipo ni nafuu, nakuhakikishia viwango vya video na ‘audio’ ni vya juu sawia na ngoma za wasanii Bab’kubwa.
Zipi nyimbo zako zingine?
Shora Junior: Kama vile Blue Economy, Zip it up, Murder She Wrote na Tega Sikio.
Unatumia mitindo gani na kwa nini?
Shora Junior: Ninatumia mitindo ya Ragga, Reggae, Hip Hop na Gengetone sababu inashabikiwa na kizazi cha sasa.
Nani kakupa msukumo?
Shora Junior: Sina mwengine wa kumtaja ila produsa wangu Magustu Babu, kama si yeye, singelikuwa hapa nilipo.
Ni wanamuziki gani Pwani unaona wanapiga hatua kimuziki?
Shora Junior: Mimi (akitabasamu). Ila pia kina Fazz Hisia, Ramodee na Overdoze wanajikakamua sana.
Hebu tufahamishe waimbaji wanaokukosha katika kanda ya Afrika Mashariki?
Shora Junior: Kina Nyashinski, Nameless na King Kaka, wote wa Kenya.
Kwa nini hukutaja wale wa Bongo ambao wanapasua nyoyo za wapenda muziki hapa nchini?
Shora Junior: Umefika wakati sisi wasanii wa Kenya tupendane na kupeana moyo sisi kwa sisi na hii pia inahusu vyombo vya habari hasa redio na televisheni kwa kutupa muda tosha hewani.
Azma yako?
Shora Junior: Nataka niwe mwimbaji wa kutajika na kutambulika kote barani Afrika na sehemu zingine duniani.
Wengi wamelalama jinsi tasnia inavyoendeshwa Pwani, wazo lako?
Shora Junior: Kusema kweli viongozi wetu wanatuangusha na kututonesha mioyo yetu kwa kuwathamini wasanii wa nje na kutuacha sisi mataani.
Wawaambia nini mashabiki wako?
Shora Junior: Nawaambia watarajie makubwa hasa kupitia mradi wa Platform ambao nia kubwa ni kuwasaidia wasanii wenzetu wasiokuwa na uwezo.