Kisa cha kipekee raia kujitokeza kuonyesha shukrani kwa afisa wa polisi
Na MWANGI MUIRURI
Ni nadra upate Wakenya wakipongeza afisa wa polisi kwa kazi njema kwa kuwa kwa kiwango kikuu, nembo ya maafisa wengi huwa ni ile ya kunyanyasa raia na kuwapa kila aina ya mahangaiko.
Ingawa wengi wa maafisa hawa hufanya kazi njema kwa kiwango kikuu, ya kulinda amani nchini, kuna wachache ambao ukatili wao huzua hisia za chuki dhidi ya kikosi hiki kiasi kwamba ni vigumu kuwapata Wakenya wakijumuika pamoja kukishangilia. Kisa cha kiazi kimoja ndani ya gunia kuoza na kusambazia uozo viazi vyote ndani ya gunia hilo.
Ni katika hali za ubinadamu wa umoja ambapo katika visa vya kwa mfano, mashambulio ya kigaidi ambapo Wakenya wakiwapa waathiriwa moyo, hushangilia maafisa wa kiusalama wakipambana kunusuru manusura.
Lakini katika hali kama za uchaguzi mkuu na usimamizi wa maafisa wa polisi katika harakati za kulinda masanduku ya kura, hafla ya upigaji kura, ujumlishaji na utangazaji wa washindi, usimamizi wa harakati za kukataa matokeo na pia uapishaji wa mshindi, kwa baadhi ya Wakenya hata bila ya ushahidi huwaona maafisa hawa kama washirika wa wizi wa kura.
Lakini katika Kaunti ya Murang’a, kuna afisa afahamikaye kama Mohammed Salim Ibrahim ambaye miaka mitano iliyopita alitua katika kituo cha Sabasaba akiwa kamanda wa kituo, OCS.
Kwa mujibu wa aliyekuwa mbunge wa Maragua, Peter Kamande, afisa huyu ni wa kipekee na ambaye alipotumwa eneo hilo, mara moja aliishia kuwa kipenzi cha wenyeji.
Aliingia katika mji huu wa Sabasaba ukiwa umeishiwa na nidhamu za kimsingi ambapo uchezaji kamari, ukahaba, uuzaji wa mihadarati mtaani, uuzaji wa pombe kiholela na ujambazi wa kila aina ulikuwa umefika kilele chake.
“Aliingia kimyakimya. Kabla ya watu waelewe kuhusu afisa huyu, alikuwa ametembea na kujipa ufahamu wa changamoto za kiusalama za mji huu na viunga vyake. Aliishia kujiweka ndani ya mitandao hiyo ya ujambazi bila kufahamika na ghafla, kukaanza kuwa na mabadiliko makuu ya kiusalama,” anasema Bw Kamande.
Ni katika hali hiyo ambapo baada ya wenyeji kupata habari kuwa afisa huyu amehamishiwa hadi Kaunti ya Nyeri, Ijumaa iliyopita walimiminika kituoni kumpa mkono wa kwaheri na wa heri njema aendako.
“Tumefika hapa kusema ahsante kwa Mzee Ibrahim kwa kazi njema alitufanyia. Daima tutamkumbuka. Alituelimisha kuhusu haki zetu. Akazima maafisa waliokuwa wakihudumu naye hapa kukamata watu kiholela. Akasitisha vituko vya sisi kukamatwa na kudaiwa hongo. Mzee Ibrahim akikukamata na uishie kuwasilishwa mahakamani, jua uko na makosa ambayo hayasemeheki,” akasema mwenyekiti wa wafanyabiashara, Wagocho Kiarie.
Wenyeji wanasema kuwa mzee huyu akiingia Sabasaba kuanza huduma yake, hata nyumba zilikuwa zinakosa wapangaji kutokana na ukora, biashara kukosa wateja wakihofia usalama wao, na kwa ujumla, mji ukiwa chini ya uthibiti wa magenge ya vijana.
“Leo hii hayo yamebadilika na yule atakayeingia hapa kuchukua hatamu za uongozi ajue kuna vigezo vya utendakazi ambavyo vimewekwa. Ajue akianza kusambaratisha ufanisi huo ambao umeafikiwa hapa, tutapiga kelele kwa dhati na tutadai usalama wa mji wetu,” anasema.
Bw Ibrahim aliambia Taifa Leo kuwa yeye ni mtu wa kujituma kazini.
“Sina chuki na yeyote na huwa najaribu sana kuwarekebisha vijana walio ndani ya uhalifu. Sio mara moja nimenusuru vijana kutokana na hatari kuu ya vyombo vya kiusalama na mikakati yake,” anasema Bw Ibrahim.
Wanaomfahamu wanamtaja mzee Ibrahim kama “mweledi mkuu wa kuwindana na mitandao ya kijambazi na ambaye uwezo wake wa upelelezi na utumiaji silaha ni wa kutamanika na wengi ndani ya kikosi cha polisi.”
Wingi-lugha
Anasemwa kuwa mtu ambaye ni mweledi wa lugha nyingi asili za hapa nchini, aliye na uwezo hata wa kujigeuza kuwa chokoraa akipeleleza suala fulani, ataingia kwa shamba la mshukiwa akijifanya kuwa kibarua na alime kwa jembe kwa muda wa saa kadhaa akichunguza na hatimaye iibuke mtu ambaye msukumo wake mkuu ni kuwapa anaohudumia usalama wao.
Ni katika hali hityo ambapo wenyeji wa Sabasaba walikuwa mara kwa mara wakizima juhudi za kumhamisha na alikuwa amegeuka kuwa mmoja wa wenyeji katika maisha yao ya kila siku, akila nao, akinywa nao na akiomboleza nao na pia akijumuika nao katika hafla za furaha.
Akiwa Mwislamu mswalihina hasa, kuna masuala ambayo alikuwa akikataa katakata akiegemea imani yake lakini akijumuika na wengi ambao ni Wakristo katika mambo yao ya kila siku bila kujitenga kwa msingi wa kidini.
“Ni mtu ambaye tutamkosa. Hata hivyo, ametuhudumia, acha asambaze moto wa huduma kwa Wakenya wengine. Ikiwa maafisa wote huwa na moyo wa kujituma kama huyu anayeenda zake Nyeri na kutuacha, Kenya ingekuwa bora kiusalama kimataifa,” anasema aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau.