• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kisanga mwanamume akiachiwa mtoto mchanga wa siku nne na mpenziwe

Kisanga mwanamume akiachiwa mtoto mchanga wa siku nne na mpenziwe

NA FRIDAH OKACHI

MALEZI kutoka kwa vijana wa Gen Z yamechangamsha hisia katika mtandao wa TikTok baada Davis Andanje kupakia video akisimulia jinsi alivyoachiwa mtoto wa siku nne na mpenziwe huku wanawake mitandaoni wakimwambia amlee mwanawe peke yake.

Hata hivyo, katika kile kinachoshanga wengi, amepokea mialiko kadhaa ya wanawake wanaotaka awaoe ili wamsaidie kulea.

Kufikia Alhamisi jioni, Andaje aliambia Taifa Leo Dijitali  alikuwa amepata maombi kutoka kwa wanawake kadhaa wakimsihi kuishi naye ili aweze kulea mwanawe.

“Saa hii kuna mama wa miaka hamsini ameniambia anaweza kuishi nami na mwanangu. Lakini sipo tayari. Muhimu ni mwanangu jinsi ya kumlea,” alisema Andanje.

Andanje alianza mahusiano na mpenziwe miaka miwili iliyopita. Uhusiano wao ulianza walipokutana kwenye gari la Climax wakisafiri.

“Tulibadilishana namba za simu wakati wa kusafiri kwenye gari. Siku mbili baadaye nilipokea simu kutoka kwake akinieleza mwajiri wake hapatikani na hivyo akaja kwangu,” alisema Andanje.

Hata hivyo, hajutii kusambaza machapisho ya kile anachopitia kwenye mtandao wa TikTok. Ameshukuru wahubiri na waliompita umri kumpa tumaini la kila siku ambalo linamtuliza.

“Sijutii kusambaza. Sikufanya vile kutafuta usaidizi. Nilitaka ulimwengu ujue ni jukumu langu kulea mtoto lakini sio sawa kumtesa mtoto,” alifafanua Bw Andanje.

Kisanga chake kilivyoanza

Nguo za mtoto zilizo kwenye karai ambazo anafaa kuosha | PICHA| FRIDAH OKACHI

Kisanga chake kilianza hivi: Mapema Februari, alipokea simu kutoka kwa jirani yake kuwa mwanawe analia na hakuna mtu ndani ya nyumba yao.

Baada ya kufanya uchunguzi, aliweza kufahamu mkewe amemwacha kutokana na ukosefu wa kazi, akifuata jamaa aliye na pesa.

“Nilikuwa nimeenda kwenye Cyber kutuma ombi la kazi. Nilipoteza kazi Juni 2023 na sasa wakati niliona mtoto amezaliwa nilijua ni wakati wa kujituma zaidi,” alianza kusimulia.

“Nikiwa pale nilipokea simu kutoka kwa jirani nirudi nyumbani kuokoa mwanangu ambaye alikuwa analia,” aliongeza Andanje.

Mpenziwe aliyetelekeza mtoto huyo, siku ya Ijumaa alijitokeza kwenye mtandao huo wa TikTok akimuonya Andanje dhidi ya kusambaza chapisho zinazomhusisha.

“Uwache kunihusisha kwenye machapisho yako. Ni vyema uweze kujua kuwa una jukumu la kumlea mtoto wako. Kiwango changu na chako hakiwezi kuwa sawa. Sasa hivi nimesonga mbele na nipo kwenye mahusiano mengine,” alisema mwanamke huyo.

Akiwa amesimama ili kuelekeza mwandishi wa habari walipomtembelea kumhoji | PICHA| FRIDAH OKACHI

Wanawake wengi walifurika katika ukurasa huo wakimweleza kuwa hakuna shida kwa kuwa wote ni wazazi sawa.

Eden Wambui, alichangia akionysha kukerwa jinsi watoto wa kike huachwa na ujauzito na wanaumme ambao hawajali.

“Kusema ukweli sioni tatizo. Ana haki sawa na mwezake. Andanje anastahii kumlea mwanawe. Mtafaruku uko wapi pale wasichana wadogo wanapoachwa na watoto au kuachwa wakiwa wajawazito? Huyo ni mtoto wake,” alisema Eden Wambui.

Muthoni Wakahiu Maina alisema kuwa wakati umefika kizazi cha kisasa wafahamishwe kuwa wanajukumu la kulea mtoto bila kugonga vichwa vya habari.

“…Vijana wetu wa kiume wanafaa kufunzwa pia. Ni haki mwanamume akiacha kujukumika ila wewe unataka kufahamika kupita vyombo vya habari…Tunataka kuwaeleza wasichana wetu iwapo baba mtoto msumbufu, msahau…pia nawe sahau huyo mama msumbufu,” alisema Muthoni Wakahiu Maina.

  • Tags

You can share this post!

MAONI: Afrika itapiga hatua hata zaidi watu wa nje wakiacha...

Kidege Shakira hapumui ‘mafisi’ wakiwania tunda lake...

T L