Kitabu cha kuwaelimisha watoto kuhusu corona
Na DIANA MUTHEU
KUWEPO kwa janga la corona nchini kulilemaza na kupelekea kufungwa kwa sekta nyingi, mojawazo ikiwa elimu.
Watoto hawaendi shuleni na wazazi wao wamelazimika kuchukua jukumu la kuwajulisha na kuelimisha wanao kuhusu njia bora za kuwa salama wakiwa nyumbani, kuambatana na hatua na miongozo ambayo imetolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya Nchini.
Kitabu kipya cha kusaidia watoto wadogo kuelewa swala nzima la janga la corona na jinsi wanaweza kusaidia kupigana na virusi hivi, kimezinduliwa.
Mashirika mawili ya kibinafsi humu nchini ambayo yanajishughulisha kutetea haki za watoto, masomo na afya ya hedhi ya: Welthungerhilfe na WASH United yameungana na kuchapisha kitabu hicho kiitwacho “Hakuna Nafasi ya Virusi za Corona” kinachoeleza hadithi kwa ucheshi, vibonzo na kimeidhinishwa na wizara ya Afya.
Kitabu hicho kimezinduliwa na kinasambazwa katika kaunti mbalimbali ili kuongeza juhudi za wazazi katika kufundisha watoto jinsi ya kuwa salama wakati wa janga hili ambalo limelemaza shughuli za masomo shuleni tangu Machi.
Akizungumza na Taifa Leo, msimamizi wa mawasiliano katika shirika la Welthungerhilfe, Bi Asenath Niva alisema, “Janga la corona laweza kumpata mtu yeyote iwe ni mtoto, mama, baba, babu au nyanya. Kitabu hiki kinaazimia kuhimiza watoto wazingatie kunawa mikono wakitumia sabuni na maji safi, watulie nyumbani na pia wasijumuike katika makundi, ili waweze kujikinga.”
Watoto wanaolengwa sana ni wale wa shule za msingi na lugha katika kitabu hiki imerahisishwa imevunjwa kwa Kiswahili na Kiingereza ili kutoa habari na kuelimisha watoto kuhusu hali ya maradhi ya Covid-19 nchini na kote ulimwenguni.
Kwa idhini ya Wizara ya Afya nchini, kitabu hicho kimesambazwa katika maeneo ya makazi duni jijini Nairobi na pia katika kaunti zingine nchini kote.
“Kitabu chenyewe hadi sasa kimesambazwa kwa watoto zaidi ya 3,000 wa shule za msingi kote nchini na kinawalenga wanafunzi zaidi ya 7,000 katika kaunti za Nairobi, Makueni, Kitui miongoni mwa zingine,” akasema Bi Niva.
Kitabu chenyewe kinasimulia hadithi ya watoto wanne kutoka sehemu tofauti ulimwenguni ambao wameathirika na janga la corona kwa kuwa hawawezi kuwasiliana tena na marafiki wao. Kupitia mtandao, watoto hao wanaelemishana kuhusu corona.
Katika kurasa za mwisho za kitabu hiki, mbinu nne muhimu zaidi zinafafanuliwa za kuzuia ueneaji wa virusi hivi ambazo ni: kutulia nyumbani, kutotangamana, kunawa mikono kutumia sabuni na maji safi yanayotiririka.
Muktadha wa simulizi ni wa mijini na sio vijijini kwa sababu maeneo hayo yana watu ambao wameathiriwa na virusi hivi. Kwa kulinganisha, hatari katika maeneo ya vijijini ni chini.