• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Kitanda kidogo ni smaku ya ndoa, mshauri wa masuala ya mapenzi asema

Kitanda kidogo ni smaku ya ndoa, mshauri wa masuala ya mapenzi asema

NA LABAAN SHABAAN

KITANDA kidogo ni bora sana kwa wanandoa kwa sababu kitasaidia kupiga hatua katika mpango wa kusuluhisha mgogoro wanapotokea. Na pia, kitanda kidogo hunogesha mapenzi yakakolea.

Haya ni kwa mujibu wa mshauri wa ndoa Bi Grace Destiny ambaye anajitambulisha kuwa mtaalamu wa masuala ya mapenzi.

“Ukimwona mwanandoa anakwepa na kulala sebuleni wanapokosana na kumwacha mpenzi wake kitandani, huyo ni mtu mnyonge sana,” alisema.

“Hawezi kustahimili mawimbi makali ya ndoa na huenda akakosa kudumu.

Bi Destiny anayesisitiza kuwa wanandoa wanafaa kusuluhisha suitafahamu yao kabla ya kulala anapendekeza wachumba na wanandoa wawe na kitanda kidogo.

Anaarifu kuwa nyumba zilizo na vitanda vikubwa huwatenganisha wachumba ama wanandoa na hukaribiana tu wakati wana haja ya kurusha roho.

“Ukaribu na mgusano kati ya wapendanao huwasha cheche za mapenzi na kuweka uhusiano kuwa thabiti,” alieleza Bi Destiny.

“Na iwapo mmekosana, inawezekana muwapo na kitanda kidogo mgusano huo utaanzisha maridhiano.”

Hata hivyo, Michelle Obama, mkewe aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama, amewahi kunukuliwa akisema, “Tumejifunza kuwa ni kawaida kupigana, na huwezi kusuluhisha mzozo wakati wote kabla ya kulala. Kwa hivyo tunajifunza ujuzi wa kuelewana na kuwa karibu tena.”

Kwa mujibu wa Bi Destiny, kuna masuala mengi ambayo yanaathiri furaha ya ndoa kama vile kazi, afya, watoto na matatizo ya kibinafsi lakini ukubwa wa kitanda pia ni kigezo cha ndoa iliyofaulu.

“Wanandoa wengi siku hizi wanapendelea vitanda vikubwa vya inchi 6 kwa 6. Lakini ukichagua kitanda kidogo kutakuwa na mvuto wa mapenzi na uhusiano utanoga,” aliendelea Bi Destiny.

“Kuna sababu nyingi sana za kutia mapenzi moto kutumia vitanda vidogo kuliko kuwa na vitanda vikubwa,” aliongeza.

Hata hivyo, mshauri huyu anakiri kuwa pia vitanda vikubwa vinaweza kuwa na umuhimu wake hasa pale ambapo mwanandoa anahitaji kuwa peke yake ili atulie akitafakari mambo mengine mbali na mahusiano.

“Kuna watu ambao hawawezi kulala kama wamekaribiana na mwingine sababu ya joto na kukosa uhuru. Na kama umezongwa na mambo mengi, huenda ukahitaji kuwa na nafasi kubwa ya kitanda bila masumbufu,” alieleza.

Hata hivyo, Bi Destiny anashauri wanandoa kuelewana wanachokitaka kuhusiana na ukubwa wa kitanda na magodoro wakizingatia pia kuwa mapenzi ni kuelewana.

  • Tags

You can share this post!

Wamiliki wa nyumba wapoteza wateja mvua zikiharibu makazi

Korti kuamua iwapo itaruhusu mtoto afuate babake Amerika au...

T L