Kitendawili cha mauaji ya Were na jaribio la kuua diwani kutoka eneobunge lake
MAAFISA wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Alhamisi walirejea eneo la tukio kuchunguza mauaji ya Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Jumatano usiku, siku nne tu baada ya jaribio la kumuua MCA kutoka eneo bunge lake.
Maafisa wa Kitengo cha Mauaji cha DCI, wakiongozwa na Mkurugenzi Martin Nyuguto, walichunguza tukio hilo kwa kuchukua video za CCTV kutoka majengo yaliyo karibu na Nairobi Funeral Home na kamera za barabarani katika mzunguko ulio karibu.
Bw Were aliuawa kwa kupigwa risasi na mhalifu aliyekuwa kwenye pikipiki saa moja na nusu jioni, wakati gari lake liliposimama kwenye taa katika barabara ya Ngong, dakika chache baada ya kutoka Bungeni.
Kwa mujibu wa familia yake, Mbunge huyo alikuwa ameeleza hofu kuhusu maisha yake, akisema kulikuwa na njama dhidi yake.
Mnamo Februari 8, alitaja visa viwili vya vurugu katika mikutano yake, akidai vilichochewa na watu kutoka nje ya eneobunge lake.
Mauaji ya Were yalifuatia jaribio la kumuua MCA mwenye umri mdogo zaidi kaunti ya Homa Bay, Vickins Bondo, 28, usiku wa Aprili 26 katika mtaa wa Lucky Summer, Nairobi.
Wakati wa shambulizi hilo, Bondo, dada yake na marafiki walishambuliwa na watu waliokuwa na silaha. Risasi ilifyatuliwa, na Bondo akapata majeraha kichwani kabla ya kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Tukio hilo halikuripotiwa katika vituo vya polisi vya Kasarani au Starehe, licha ya kuwa karibu.
Duru za familia ziliambia Taifa Leo kuwa shambulio hilo huenda lilihusiana na juhudi zake za kutaka uchunguzi wa kifo cha baba yake, aliyekuwa Inspekta mkuu Nicholas Aguk Oballa — aliyegongwa na gari akiwa kazini katika uwanja wa JKIA mnamo Februari 7.
DCI imetwaa uchunguzi wa kifo hicho baada ya kitengo cha trafiki kushindwa kufuatilia gari lililohusika.
Bw Were na MCA Bondo wote wanatoka katika wardi ya West Kasipul, eneobunge la Kasipul, jambo linalofanya uchunguzi kuhusu uhusiano wa matukio haya kuwa muhimu.
Kitengo cha Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi pia kimeanza kuchambua simu ya Bw Were ili kufuatilia mawasiliano yake kabla ya kuuawa wakilenga rekodi za simu na jumbe kutafuta vidokezo.
Ripoti zinaonyesha kuwa Bw Were alikuwa ameketi nyuma ya gari jeupe aina ya Toyota Crown aliposhambuliwa.
Wakati huo, wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki walimkaribia; mmoja akatoa bunduki na kumpiga risasi. Dereva na mlinzi wake hawakuumizwa, ikidokeza kuwa huenda yalikuwa mauaji ya kimkakati dhidi ya mtu maalum Kimombo, assasination.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kupitia msemaji wa polisi Muchiri Nyaga, alisema mauaji hayo yalikuwa yamepangwa mapema.
Uchunguzi unaendelea.
Katika hotuba yake ya awali Februari, Were alisema alikuwa anafuatwa na watu waliokuwa na nia ya kumuua, na akasema washukiwa walitoka nje ya eneo lake.
Familia yake imekanusha madai kuwa alikuwa mtu wa fujo au aliye na damu mikononi mwake, wakisema hiyo ni njia ya kuficha ukweli na kuwalinda wauaji wake.
Paul Juma, kaka yake, alisema Were alikuwa akiwasema wazi watu anaohisi walitaka kumuua lakini hakupata msaada wowote.
James Were, ndugu mwingine, alidai kuwa mikutano fulani ilifanyika kupanga mauaji hayo.
“Watu fulani serikalini huenda wanahusika,” alisema.
Dalmas Otieno, kaka mkubwa wa Were, alikanusha madai kuwa marehemu alikuwa na historia ya kupanga na kuzua ghasia.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, Alhamisi alisema uchunguzi uko katika hatua za mwisho.
Alitoa kauli hiyo alipowatembelea maafisa wa polisi walioumia kwenye operesheni huko Lamu.