Makala

Kitendawili cha mwili wa mfanyabiashara kupatikana umetupwa kando ya Bwawa Turkwel

Na OSCAR KAKAI October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA moja katika kijiji cha Sirende, mji wa  Kitale katika kaunti ya Trans-Nzoia inataka majibu kuhusiana na kifo cha mpendwa wao ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa katika eneo la Riting, kando ya bwawa la Turkwel, Pokot Magharibi.

Kulingana na familia hiyo, marehemu anaweza kuwa aliuawa siku yenyewe ambayo alipotea.

Macho yake yalikuwa yametolewa, tumbo imekatwa na uso kuonekana kama uliopigwa na kifaa butu.

Familia hiyo sasa inataka haki itendeke ikisema kuwa huenda jamaa wao aliuawa na watu wasiojulikana.

Mwili wa Bw John Njuguna Kuria almaaruf “Ndigirii” mwenye umri wa miaka 59 ulipatikana Ijumaa, Oktoba, 18, 2024 katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya kaunti ya rufaa ya  Kapenguria.

Mkewe marehemu Bi Jane Wamboi anasema kuwa mumewe alipotea wiki jana akiwa katika kilabu chake cha kuuza pombe ya “The Ndigirii’s” katika mji wa Makutano, Kapenguria, katika kaunti ya Pokot Magharibi.

“Tulifikiria kuwa alikuwa ameshikwa ama yuko katika hospitali. Tulitafuta kwenye hospitali na seli zote bila mafanikio,” anasema.

Bw Nguguna, baba wa watoto watano alikuwa akifanya kazi kwenye baa yake mjini Kapenguria na alikuwa na shamba lake eneo la Marich katika kaunti ndogo ya Pokot ya Kati.

“Niliongea na mume wangu Jumanne Oktoba 8, 2024 wiki jana kupitia ujumbe wa simu. Siku ifuatayo, nilipata amejaribu kunipigia simu nikiwa kwenye shamba eneo la Sirende, Trans-Nzoia,” anasema Bi Wamboi ambaye amepoteza mumewe katika mazingira yasiyoeleweka na wamekuwa wakimsaka kutoka wiki jana.

Bi Wamboi anasema kuwa mumewe alikuwa ameishi mjini Kapenguria kwa wiki mbili bila kuja nyumbani.

Anasema alidhani kuwa alikuwa ameenda shambani eneo la Marich.

“Nilimpigia simu DJ kwenye kilabu na akasema kuwa tajiri wake aliwacha simu kwenye kaunta. Pia niliwapigia simu vijana wa shamba eneo la Marich lakini walisema kuwa hakuwa amefika huko,” anasema.

Anasema kuwa alienda hadi kwenye nyumba ambayo amekodi eneo la Marich lakini hakuwa huko.

“Tulivunja nyumba na kuingia. Nilipata tu nguo chafu kwenye nyumba nikazichukua,” anasema.

Anasema kuwa alipiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha Kapenguria.

Anasema kuwa alipigiwa simu na mtu ambaye aliona mwili wa mumewe ukiwa umetupwa.

“Mwanaume huyo aliona habari kwenye mitandao ya kijami kisha akanipigia simu,” anasema.

Anasema kuwa mwili wa Bw Njuguna ulikuwa umepondwapondwa, majeraha mengi na nguo zimeraruliwa.

“Nilijua ni mwili wake baada ya kuangalia miguu,” anasema.

Mpwa wake marehemu David Kuria anasema kuwa Bw Njuguna alionekana mara ya mwisgo akiwa kwenye pikipiki eneo la Bendera Alhamisi, Oktoba, 8, 2024.

“Tuligundua kuwa amepotea wakati hakuwa anashika simu. Tulishangaa kuhusu kilichokuwa kinaendelea sababu huwa hakosi kushika simu. Tulijua kuwa kuna kitu kibaya kimetendeka,” anasema.

 Anasema kuwa wanangojea ripoti ya daktari ikiwa mwili wake utafanyiwa upasuaji.

Naibu wa chifu wa kata ya Kostei Joseph Siwa, alithibitisha kuwa mwili wa mtu asiyejulikana ulipatikana eneo la Riting kando ya  Turkwel. Anasema kuwa mwili huo ulichukuliwa na polisi na kupelekwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria.

“Wakazi wanasema kuwa hawakuona mtu huyo akiwa hai eneo la Riting. Anaweza kuwa aliuawa eneo lingine na mwili ukaletwa kutupwa hapa. Alikuwa na kaptura nyeupe, mshipi wa masaai, tishati na vesti,” anasema Chifu Siwa.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati Pokot(OCPD) Nelson Omwenga anasema kuwa mwili wa marehemu ulipatikana na wakazi ambao walipiga ripoti kwa polisi.

Bw Omwenga anasema kuwa maafisa wa upelelezi wanafanya uchunguzi kuhusu suala hilo.