Makala

KITO CHA THAMANI: Mauzo ya vifaa asilia vya Wasamburu yampa pato

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMUEL BAYA

JAMII za Wasamburu, Waturkana na Wapokot wanajulikana kote nchini kwa kutunza na kutathmini utamaduni wao wa kale, licha ya tamaduni za kisasa kutishia kuangamiza itikadi za jadi ambazo zilitumiwa kuimairisha maisha ya wananchi.

Ndio maana, bado jamii hizi zimehifadhi vito vya zamani ambavyo kwa sasa vinatumika sana kueneza utalii katika kaunti hizo.

Kwa yakini, uuzaji wa vito hivi vya kale vya jamii hizi umekuwa tegemeo la baadhi ya wafanyibiashara katika kaunti ya Samburu ambao wameamua kuchuma kupitia uuzaji wake.

Mmoja wa wafanyabiashara hawa ni Bw Richard Lowa mwenye umri wa miaka 40 kutoka kijiji cha Baragoi.

Tulikutana naye mjini Maralal akiendelea na shughuli ya kuuza vito hivyo asilia na aliambia Akilimali kwamba biashara hiyo imekuwa kuu kwake na imejaa faida tele.

Katika kibanda chake, tulimkuta akiuza shanga asilia, pochi na mikanda iliyoundwa kwa ngozi pamoja na vyuma kuukuu ambavyo vilitumika kutengeneza mafumo na mishale.

“Mimi ninauza vitu vya kiasili kutoka kwa jamii za Waturkana. Ni vitu kama vile shanga za zamani, pochi za kutengenezwa na ngozi ya ngamia kwa ajili ya kuweka pesa kwa watu wa Turkana. Kisha tuko na shanga za chuma za zamani ambazo zilitumika zamani kabla hata ya kuanza kutumiwa katika taifa la Slovakia,” akasema Bw Lowa.

Ni kazi ambayo alisema ameifanya kwa takribani miaka 30, hivyo basi kuaminisha kwamba alianza akiwa katika umri mdogo.

“Niko na miaka 30 ndani ya kazi hii. Zamani nikianza baada ya kuacha masomo yangu, nilikuwa mdogo na huu ni ubunifu wangu mwenyewe. Niliposhindwa kuendelea na masomo ya upili baada ya KCPE, nilianza kuwafuata watalii katika mji wa Baragoi nikiwa pia ninawauzia vitu mbalimbali,” akasema Bw Lowa.

Katika kibanda chake alichokuwa ameweka akiuza bidhaa zake, Bw Lowa alituonyesha sketi ya ngozi ambayo ni maalum kwa jamii ya Waturkana.

Hii sketi iliyoundwa kwa ngozi ya ngamia na ni vazi la ndani la wamama wa Turkana. Hii huuzwa kwa Sh2,000 na imekuwa mojawapo ya vitu vinavyovutia sana watalii,” akasema.

Alisema kuwa licha ya changamoto nyingi ambazo zimeletwa na biashara hii, bado imeendelea kuwa mojawapo ya biashara ambazo bado anazitegemea kuendelea maisha yake.

“Hii biashara mara nyengine hutegemea watalii na wanapofika katika eneo hili kwa wingi, huwa tunakuwa na biashara nyingi. Kwa siku moja mimi huweza kuuza bidhaa za Sh7,000 kwa siku,” akasema Bw Lowa.

Jamaa huyu alisema kuwa biashara hii imemsaidia kuyasukuma maisha yake na anaamini kwamba ndiyo msingi ambao atatumia kufanikisha azma yake kimaisha.

“Mimi bado sijaoa ila ninasukuma maisha yangu kupitia kwa biashara hii. Pia ninajaribu kufanya ujenzi nyumbani kwetu Baragio. Kwa sasa ninapanga kuanzisha duka langu kijijini,” akasema.

Mchungaji

Mbali na kuwa muuzaji wa vito hivyo ambavyo ni pamoja na vinyago vya jamii hizo, Bw Lowa alitueleza kwamba yeye huwa na kibarua cha kuongoza watalii na vilevile ni mchungaji akiongoza kanisa katika eneo hilo la Baragoi.

“Tunatoa hivi vitu katika eneo la Baragoi kwa sababu huwezi kuvipata vitu hivi katika mji kama Maralal. Mimi pia huongoza watalii hadi katika hifadhi ya Lolyangayan. Pia mimi ninahubiri neno la Mungu katika kanisa langu la Christ Fellowship katika eneo hilo la Baragio,” akasema.

Bw Lowa alikuwa mongoni mwa wafanyibiashara ambao walikuwa wamefika katika kijiji cha Iyare wakti wa mashindano ya ngamia na utamaduni wa jamii za Samburu, Pokot na Turkana.

Alisema kuwa bidhaa zake zimekuwa zikiuzwa kwa bei tofauti tofauti, kwanza ikiwa bei ya kuuzia watalii na bei kwa minajili ya watu wa nyumbani.

“Hii biashara yangu imeinuliwa kwa kiwango fulani na serikali ya kaunti ambayo imekuwa ikinunua baadhi ya vito hivyo na kuvitumia kutangaza utalii wa Samburu. Vile vile bei ambayo tunauzia watalii ni tofauti na ile ambayo tunauzia wenyeji,” akasema.

Na ilidhihirika wazi wakati mkanda wa ngozi ambao mwenyeji anauziwa kwa Sh500, mtalii huwa anauziwa kwa Sh1,000.

Aliwataka wakenya waendelee kufanya kazi kwa bidii kwani maisha ni magumu yanahitaji kujitolea zaidi kuyakabili.

“Mimi baada ya kugundua kwamba sikuwa na uwezo wa kuendelea na masomo ya sekondari, niliamua kwamba kwamba hii ndiyo njia pekee ya kukabiliana na maisha na sijutii kwa sababu ninapata mkate wangu wa kila siku,” akasema Bw Lowa.

Mwisho.