Kliniki aina yake kisiwani Lamu ambapo paka hupangwa uzazi
KISIWA cha Lamu kinachojumuisha mji wa kale mara nyingi mambo yake huwa ni ya kipekeepekee.
Ni kisiwa hiki ambapo utapata watu wakitembea kwa miguu, kusukuma mikokoteni au kuparamia punda ilmuradi wasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Matumizi ya vyombo vya kisasa vya uchukuzi kama vile magari na baiskeli yamekuwa yakidhibitiwa kwenye mji huu wa kihistoria.
Ni kutokana na hali hiyo ambapo mwaka 2001, mji wa kale wa Lamu uliorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi ulimwenguni kote kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake-yaani UNESCO World Heritage Site.

Aghalabu upekee wa kimaisha kwenye Mji wa Kale wa Lamu umepelekea mambo mengi yanayotekelezwa mjini humo kuonekana kuwa nadra na ya kipekee, mengine yakiwa si ya kawaida.
Kwa mfano, ni kawaida kwa binadamu kutumia njia mbalimbali za uzazi au hata kufunga uzazi pale unapoona idadi ya watoto wako imetosha.
Ila kusikia paka kufunga uzazi si jambo lililozoeleka katika jamii zetu, hasa zile za Kiafrika.
Ni kisiwani Lamu ambapo utapata njia za kupanga uzazi pia zinatumika kudhibiti idadi ya paka, hasa wale wa kurandaranda mitaani.
Hapa, hata utapata kuna kituo cha matibabu maalumu ya wanyama au kliniki ambapo ufungaji au upangaji paka kizazi unatekelezwa.
Kituo hicho kwa jina Lamu Animal Welfare Clinic, kinapatikana mtaa wa Mkomani mjini Lamu.
Kilizinduliwa mnamo mwaka 2004.

Hii ni baada ya kushuhudiwa kuongezeka kwa idadi ya paka wanaorandaranda mitaani kwenye mji huo wa kihistoria.
Mwanzilishi na Meneja wa Kituo hicho cha Matibabu ya Wanyama na Upangaji Uzazi Paka Lamu Richarde Traeger, anasema aliibuka na fikra hiyo ya kudhibiti idadi ya paka wa mitaani alipokuwa kwenye ziara ya kitalii kisiwani Lamu.
Bi Traeger anataja mzigo wa idadi kubwa ya paka wanaorandaranda mitaani na kukumbwa na mafadhaiko kutokana na ugumu wa maisha kisiwani Lamu kufikia zaidi ya 20,000.
“Nilipokuwa nikitembea mitaa ya Mji wa Kale wa Lamu, nilijionea na kukumbana na hali ngumu ya maisha waliyoishi paka wa kurandaranda. Hapo ndipo wazo lilinijia kwamba kuna umuhimu wa idadi ya paka kudhibitiwa isiongezeke. Hivyo ndivyo nilivyoanzisha mradi wa kufunga paka kizazi. Nilijua fika kuwa tukipunguza idadi yao basi tutazuia au kudhibiti hizo changamoto zinazowakumba wanyama hao kwenye mazingira au humo mitaani wanamoishi,” akasema Bi Traeger.
Aliongeza, “Kuachilia paka kuongezeka inamaanisha watakuwa wengi kupita kiasi, hivyo kupelekea wao kung’ang’ania chakula ambacho tayari hakuna wa kuwaangalia au kuwapa. Hilo litamaanisha mahangaiko zaidi ya wanyama hao mitaani na si jambo zuri.”
Ni kupitia mpango au kampeni aliyoipa jina Kamata-Panga Uzazi-Chanja-Achilia au kwa Kiingereza ‘Trap-Neuter-Vaccinate-Release (TNVR) ambapo kufikia sasa kiliniki hiyo ya wanyama ya Lamu imefaulu kupanga uzazi paka wa kurandaranda mitaani zaidi ya 12,000.

Kliniki hiyo pia inajivunia kuwatibu na kuwachanja wanyama wengine, ikiwemo mbwa zaidi ya 36,000 kutoka mitaa tofauti tofauti ya kisiwa cha Lamu na viunga vyake.
Daktari Mkuu wa Kliniki ya Wanyama na Mtaalamu wa kufunga paka uzazi kisiwani Lamu Vivianne Jelimo Kibet, anasema tangu kuzinduliwa kwa mpango huo wa upangaji uzazi, idadi ya paka wanaotembea ovyo kwenye mitaa ya Lamu imepungua pakubwa.
Dkt Kibet anaeleza kuwa paka huwa wanabeba mimba kwa muda mfupi sana ambao ni takriban siku 65 pekee.
Hilo linamaanisha wanyama hao wasipopangwa uzazi idadi yao itazidi kuongezeka kwa kiwango kikubwa kisichotarajiwa wala kukadirika.
“Kwa mwaka, paka anaweza kuzaa zaidi ya mara mbili au tatu. Anaweza kuzaa hadi watoto sita kwa wakati mmoja. Na ndiyo sababu tukiwapanga uzazi tutapunguza idadi au ongezeko lao linalotisha. Kuwafunga paka uzazi kunapunguza idadi yao, hivyo kupunguza au kudhibiti zile changamoto wanazokumbana nazo kwenye mitaa yetu,” Dkt Kibet.
Lakini je, huo upangaji uzazi wa paka unatekelezwa vipi?
Dkt Kibet anafafanua kuwa wao huwafunga paka wa kike kizazi ili wasishike mimba kabisa ikizingatiwa kuwa wao ndio wanabeba mimba na kuzaa kwa wingi.
Anaonya kuwa endapo utaacha paka jike mmoja bila kumpanga uzazi ana uwezo wa kuzaa watoto wengi sana.
Vivyo hivyo anasema upangaji uzazi pia unashirikisha paka wa kiume ambapo wao huwa wanawahasi (castration).
Anasema paka dume mmoja pekee anaweza kuzalisha hata paka kumi.

“Ndio maana tunazingatia kufunga kizazi cha paka jike na kisha kuhasi paka dume,” akasema Dkt Kibet.
Said Shukrani, ambaye ni mhudumu wa Kliniki ya Wanyama Lamu, anaamini kufunga paka kizazi ni njia nzuri ya kuboresha ustawi wa wanyama hao mitaani.
Bw Shukrani anaeleza kuwa ili kufanikisha kampeni yao, wao hufanya doria za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ya kila wiki katika maeneo mbalimbali ya majalala ambayo watu hutupa chakula na taka nyingine.
Anataja maeneo hayo kuwa maskani mwafaka ambayo paka wa kurandaranda hupatikana kwa wingi.
“Kikubwa tunachofanya ni kuwasaka, kuwakamata, kuwafunga kizazi, kuwachanja na kuwarudisha paka kwenye hayo maskani yao. Lengo kuu ni kuboresha maisha yao kupitia kupunguza idadi yao,” akasema Bw Shukrani.
Anaeleza, “Paka wakiwa wengi mitaani idadi ao hushindwa kudhibitiwa, ikiwemo changamoto kama vile magonjwa na malezi kwa jumla. Kupanga paka uzazi kunasaidia kuzuia mambo hayo yasitokee.”
Je, paka ambao wamefungwa uzazi wanatambulika vipi?
Bw Shukrani anasema wao huwaweka alama maalum paka wote ambao wamefungwa uzazi ili iwe rahisi kwao kutambulika.
“Ukimtazama paka tuliyekwisha kumfunga uzazi utapata kuna sehemu kwenye ncha ya sikio lake ambayo huwa tumeikata kidogo. Hilo hutusaidia kuepuka kumkamata tena paka aliyekwisha kufungwa uzazi,” akasema Bw Shukrani.
Wakazi wa Lamu waliozungumza na Taifa Leo walikiri kuwa licha ya operesheni au kampeni kuwalenga sana paka wa mtaani, jamii inayozunguka kliniki hiyo pia imekuwa ikijitokeza kupata msaada wa huduma hiyo kupitia kufunga paka wao wa nyumbani uzazi.
Bw Said Alii anasema yeye huleta paka na mbwa wake kwenye kliniki hiyo kila mara ili kufanyiwa huduma ya kupanga uzazi na chanjo.
“Twashukuru. Kupitia kampeni inayoendelea ya kuwapanga uzazi wanyama, kliniki imefaulu kuzuia paka na mbwa wetu kuzaana sana na kuwa kero kwetu. Wanyama wetu pia wanapokezwa chanjo za mara kwa mara hapa. Hilo limeacha wanyama wetu wakiwa na afya bora na kuzuia mlipuko wa maradhi, hasa kwa hawa paka na mbwa wetu,” akasema Bw Alii.
Ni kupitia juhudi za kliniki hiyo ambapo pia jamii imehamasishwa na kukumbatia kuwatunza wanyama wao, ikiwemo kuwakimu kwa mahitaji na haki zao za kimsingi ambazo ni chakula, mahali bora pa kulala au kuishi, kuwatafutia tiba nakadhalika.