Makala

Kituo cha Turkwel Gorge chapoteza mvuto, uvundo ukisheheni

March 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA OSCAR KAKAI

TAKA katika kituo cha Turkwel Gorge Resort Club zimesababisha uvundo wa kila aina kuhanikiza, hali hii ikizorotesha mapato katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Turkwel Gorge kilikuwa kituo cha starehe na michezo lakini sasa sehemu hiyo ni mahame.

Aidha, paa za kivutio hicho zimeharibiwa na mchwa huku maji ya mvua yakivuja kila mvua inaponyesha katika sehemu hiyo ya kujistarehesha.

Isitoshe, popo na ndege wamejenga viota vyao kwenye paa huku wanyamapori wakitawala.

Vyoo ni vichafu katika kituo hicho.

Kituo hicho kinawavutia tu vijana wasiokuwa na shughuli za maana ambao hufika hapo kuota jua kila asubuhi.

Hakuna tena maji ya shawa na mabafu ya kuoga na mchezo wa pool baada ya miundomsingi kuharibiwa na watu wasiojulikana.

Kidimbwi cha kuogelea lkilichoharibika. PICHA | OSCAR KAKAI

Uwanja wa mchezo wa vikapu, kidimbwi cha kuogelea na maduka sasa yako katika hali mbaya.

Miaka 15 iliyopita, kituo hicho kilikuwa cha mandhari mazuri ya kuvutia, huku hapo kukiwa na miti ya kiasili iliyoleta upepo mzuri.

Watu wengi katika kituo hicho ambacho kiko eneo la mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana.

Wale ambao walikiwa wakihisi joto jingi ungewaona kwenye kidimbwi cha kuogelea karibu na mkahawa huo huku wengine wakicheza basketiboli.

Uwanja wa basketiboli katika Turkwel gorge Resort Club. PICHA | OSCAR KAKAI

Wapenda raha ungewaona ndani ya chumba cha msonge kilichoundwa na nyasi wakijiburudisha kwa vinywaji baridi na pombe huku wakila nyamachoma ya mbuzi.

Lakini sasa hali imebadilika huku wakazi wengi wakisema kupotea kwa ‘umanyanga’ wa kituo hicho ulichangiwa pia na mashambulio ya mara kwa mara na visa vya utovu wa usalama vinavyoletwa na majangili.

Wakazi hao wanasema kuwa kuna haja ya kufufua huduma zote za kampuni ya uzalishaji umeme ya Kengen eneo la Turkwel baada ya kuathirika na visa vya utovu wa usalama.

Mkahawa wa Turkwell Gorge ambao uko kilomita 76 Kaskani ya mji wa Kapenguria katika Kaunti ya Pokot Magharibi ulikuwa ukivutia watalii wa humu nchi na wale wa nchi za kigeni na viongozi.

Zaidi ya wafanyakazi 2,000 wa kampuni ya Kengen walikuwa wanaishi eneo hilo.

Mwaka wa 2006, aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori alilala kwenye mkahawa  huo wakati alikuwa mgeni wa heshima kwenye mbio za balozi wa amani Tegla Loroupe.

Mkahawa huo uliachwa mahame baada ya wafanyikazi wa kampuni ya  Kengen  kuhamia mji wa Kitale, miaka 15  iliyopita.

Changamoto kuu ilikuwa ni utovu wa usalama, suala ambalo lilifanya kampuni ya Kengen kusitisha baadhi ya shughuli baada ya mashambulio kati ya jamii za Pokot na Turkana kuzidi kushuhudiwa eneo hilo.

Bi Roselyn Rorikilim, mkazi, anasema kuwa wenyeji wamepata hasara kubwa baada ya shughuli hizo kusitishwa.

“Biashara zilikuwa zikivuma. Tulikuwa tukibebwa na basi kila Jumatano kuenda Kesegon na Kitale kununua chakula. Kulikuwa na kamati ya kusaidia jamii na kiongozi wake.Tulikuwa tukienda matembezi Olkaria, Nakuria,Tiambere, Sondomuru na Samburu,” anakumbuka siku hizo za raha.

Naye Dickson Soromuk alisema kuwa zaidi ya wafanyika reja reja 300 ambao walikuwa wameajiriwa na kampuni hiyo walipoteza kazi.

“Thomas Makori, ambaye ni mtaalamu wa ujenzi, anasema kuwa hakuna maafisa wa usalama katika eneo hilo.

“Maisha yalikuwa raha hapa lakini yakabadilika sababu ya ujangili. Mkahawa huo ulikuwa ukifanya kazi kwa muda wa saa 24.Ungedhani hauko kaunti ya Pokot Magharibi,” anaeleza Soromuk.

Bi Irene Cheyech, mkazi, anasema kuwa watu wengi walitumia kituo hicho kama eneo la kuenda kujivinjari wakati wa likizo.

Chifu wa Turkwel, Africano Asirong anasema kuwa jamii za Pokot na  Turkana zenyewe zilichangia kuanguka kwa kituo hicho kutokana na umiliki wa silaha haramu.

“Utovu wa usalama bado ni changamoto. Itakuwa vigumu ikiwa jamii hizo mbili zitazidi kumiliki silaha haramu,” anasema Bw Asirong.

Alisema kuwa hata hivyo kampuni ya Kengen imeanza kujenga vyumba vichache vya wafanyakazi na tayari imejenga ukuta na ua.

“Kituo hicho kilisaulika. Kengen na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawi wa eneo la Kerio (KVDA) zinadai kukimiliki. Ni vyema serikali ya kaunti ikichukue sasa. Ni vigumu kupata huduma za afya na usafiri na wanafunzi walikuwa wakinufaika,” anasema Bw Asirong.

Anasema kuwa wakazi walikuwa wakitegemea huduma za kampuni hiyo na sasa wanateseka.

“Klikini ilihamishwa hadi Kitale. Siku hizi mabasi hayako na wanafunzi hutembea kwa miguu,” anasema.

Anaongeza kusema kuwa mbio zaLoroupe zilikuwa zikifanyika na vijana wengi walipata ajira, kampuni kuajiri walimu na kupeana huduma za matibabu kwa wakazi.

Meneja Mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos anasema kuwa wametenga fedha za kukarabati vituo vyote ambazo viliharibiwa kutokana na visa vya utovu wa usalama eneo la Turkwel.

“Tunataka kukarabati vituo vyote ambavyo vimeharibika,” anasema.

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo katika Bunge la Kitaifa anasema kuwa serikali ina mipango ya kukarabati vifaa vyote vya serikali ambavyo vimetelekezwa  eneo hilo.

“Tunataka kuvutia watalii kwa sababu eneo hilo ni nzuri kwa wageni,” anasema Bw Lochakapong.

Kwa muda mrefu usimamizi wa kampuni ya Kengen umekuwa ukiahidi kufufua shughuli zote bila kutimiza.

[email protected]