• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
KIU YA UFANISI: Biashara ya mitumba yahitaji majira ya jimbi na ufahamu wa wateja

KIU YA UFANISI: Biashara ya mitumba yahitaji majira ya jimbi na ufahamu wa wateja

Na CHARLES ONGADI

NI asubuhi na mapema pembezoni mwa barabara ya Karisa Maitha hatua chache tu na lango la Chuo cha mafunzo ya Ualimu cha Shanzu.

Kila mmoja anaonekana akiwa katika mishemishe za kusaka hela, wafanyabiashara wakifungua maduka na maeneo yao ya biashara tayari kuwahudumia wateja wao.

Millicent Sweta, mama wa watoto wanne tayari yuko ange akifungua biashara yake ya nguo za mitumba kwa lengo la kuwapata wateja wanaorauka asubuki kuelekea kazini.

“Unajua biashara ni asubuhi, jioni ni stori ya kuhesabu faida ama hasara.

Hapa biashara ni lazima urauke ndipo mambo yanyooke,” asema Millicent Sweta akipanga kwa umaridadi mali yake kuvutia wateja wanaopita kuelekea kazini.

Ni nguo za kila aina ikiwemo za watoto, mashati ya watu wazima, shuka za kitandani, marinda ya akina mama na nguo za vijana wa kileo zinazopendwa na wateja wake wengi.

Kila baada ya dakika utamwona mteja akiuliza bei ya bidhaa anayopendezwa nayo kutokana na ujuzi alio nao Millicent wa kuchagua nguo za kuvutia.

“Ninaelewa vyema wanachohitaji wateja wangu na kwa hili nimeweza kuzidi kupata wateja wengi kila uchao,” asema wakati wa mazungumzo na Akilimali majuzi.

Nguo nyingi za watoto anauza kwa kati ya Sh100 hadi 500 kulingana na ilivyo nguo na mashati ya watu wazima kwa kati ya Sh200 hadi Sh450 wakati shuka moja akiuza kwa kati ya Sh400 hadi 700 kulingana na ukubwa.

Millicent Sweta akipanga nguo za watoto katika kibanda chake kilichoko pembezoni mwa barabara ya Karisa Maitha eneo la Shanzu, Kisauni, Mombasa hivi majuzi. Picha/ Charles Ongadi

Kulingana naye, alianza biashara ya kuuza nguo za mitumba kutokana na mtaji aliopata kutokana na kuweka akiba hela alizoachiwa na mumewe za matumizi ya siku.

“Nilikuwa na nia ya kuanzisha biashara ila sikuwa na mtaji lakini baada ya kuwaza na kuwazua nilifikia uamuzi wa kutenga kiasi fulani ya fedha kila siku niliyowachiwa na mume wangu za matumizi,” asema Millicent.

Na kwa kuwa kidogo kidogo hujaza kibaba baaada ya kipindi cha mwaka mmoja, alikuwa tayari ameweka kibindoni kiasi cha Sh8,000 kama mtaji.

Alijitumbukiza mzima mzima katika biashara ya kuuza nguo za mitumba akinunua furushi lake la kwanza kwa kiasi hicho chote.

Baada ya kipindi cha wiki mbili, Millicent alifaulu kupata faida ya mara mbili ya kiasi alichotumia kama faida jambo lililompelekea kutoka alikoanzia (mtaa wa Mikoroshoni) hadi pembezoni mwa barabara ya kuelekea Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu.

Kulingana naye, baada ya kuanza kuona matunda ya biashara ya nguo za mitumba, alilazimika kuajiri msaidizi.

Na ili kupata faida zaidi, kila katikati na mwishoni mwa mwezi, anaamua kuchuuza nguo zake nje ya lango la kampuni ya EPZ iliyoko Majengo Kanamai na katika kituo cha biashara cha Takaungu, Kilifi.

Ni njia mojawapo ya kuwafikia wateja wake walio mashinani na wale wanaokosa nafasi ya kumfikia kutokana na kubanwa na shughuli za kikazi.

“Biashara hii inahitaji kujituma na kujitolea na pia kujua kuzungumza na wateja ndipo uweze kuwafikia katika kila pembe walipo,” aeleza kwa bashasha.

Ijapo alidinda kutufichulia kiasi anachotia kibindoni kila mwisho wa mwezi, anakiri biashara ya nguo za mitumba inalipa maradufu endapo mfanyabiashara atafuata sheria na masharti.

Aidha, anakiri kuna kipindi ambacho biashara hii hushuka na wakati huo ndipo mfanyabiashara analazimika kutumia uzoefu katika kuhakikisha biashara inazidi kusimama kidete.

“Ni vizuri kuweka akiba ya kutosha wakati biashara inaponawiri ilikuweza kuzitumia mambo yanapoenda segemnege,” asema Sweta.

Ameweza kujikimu barabara kimaisha akitegemea biashara hii baada ya kutengana na mumewe akiwasomesha wanawe.

Kifungua mimba wake anatarajiwa kuhitimu Chuo Kikuu mwezi Desemba wakati wa pili akimaliza masomo yake ya Kidato cha Nne mwaka jana huku wawili ambao ni pacha wako Darasa la Saba.

Anawahimiza kina mama kujituma katika kila wafanyalo na wala wasithubutu kuwategemea mabwana zao kuwafanyia kila kitu maishani.

You can share this post!

Maeneobunge maskini kupata mgao mkubwa wa NG-CDF

KIU YA UFANISI: Uuzaji kinywaji cha kahawa humpa zaidi ya...

adminleo