• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
KIU YA UFANISI: Huchumia juani kwa kuzungusha bidhaa za vinyago kukimu familia

KIU YA UFANISI: Huchumia juani kwa kuzungusha bidhaa za vinyago kukimu familia

Na MISHI GONGO

AMA kweli mgaagaa na upwa hali wali mkavu na mchumia juani hula kivulini, methali hizi ndizo zinazompa msukumo Josphine Matheka, mjane, anayepambana na makali ya jua kila siku akizungusha vinyago na mapambo mengine maarufu nchini kwa watalii, ili kukimu familia yake.

Matheka, aliyeachiwa ulezi wa watoto watatu baada ya mumewe kufariki aliingilia biashara ya kuuza vinyago hivyo kukidhi mahitaji ya watoto wake ambao mmoja wao anaugua maradhi ya Sickle Cell Anaemia.

Anasema mwanzo alitegemea Wasamaria Wema kumpatia mwanawe matababu ambayo hakuwa na uwezo wa kuyamudu kufuatia ada za juu za dawa.

“Babake alikuwa akimsimamia lakini baada ya kufariki nilitegemea Wasamaria Wema na familia kwa muda kabla kuanzisha biashara ambayo sasa inaniwezesha kumshughulikia yeye na hata wenzake,” alieleza.

Mama huyo anaeleza kuwa siku yake huanza saa kumi alfajiri.

“Siyo kazi rahisi kama wengi wanavyofikiria, nalazimika kutembea mwendo mrefu kufikia wateja ninaowalenga kabla ya wafanyabiashara wengine kuwafikia,” alisema.

Miongoni mwa vinyago anavyouza ni simba, chui, nyati, ndovu, kifaru, kiboko, vinyago vya sura za mashujaa nchini, vikombe vilivyorembwa kwa bendera ya Kenya na vyinginevyo.

Pia hutengeneza bidhaa za urembo kutumia shanga na mbao, bidhaa hizo ni bangili, mikufu, vipuli na vikuku vya miguu.

Vyote hivi vinatofautiana kwa ukubwa na rangi kila moja kikiwa na bei tofauti kulingana na ukubwa, ustadi uliyotumika kuunda na hata anayeuziwa.

Kwa kuwa hulenga watalii kutoka mataifa ya kigeni yeye hulazimika kutembeza biashara yake katika fuo za bahari, katika hoteli na mikahawa mbalimbali mwambao wa Pwani.

“Sina sehemu maalum ya kufanyia kazi, mimi huzunguka katika fuo za bahari na hoteli kusaka wateja,” alisema.

Ananieleza kuwa kazi hiyo ina ushindani mkubwa, na analazimika kuwa jasiri ili kupambana na wanaume ambao ndio waliotawala biashara hiyo.

“Nimejifunza kukimbilia wateja na hata kupigana kumbo na wafanyabiashara wenzangu muhimu kuuza, ukiketi chini hakuna mteja atakufuata,” alieleza.

Bi Matheka ambaye ana umri wa miaka 49, alieleza kuwa changamoto anazokumbana nazo ni kukosa kigari cha kutembeza biashara zake.

“Kwa kuwa sijafanikiwa kununua troli itakayoniwezesha kunadi biashara yangu nalazimika kuzibeba mgongoni kila siku kuzipeleka katika fuo za bahari au hoteli,” alisema.

Pia alisema msimu watalii wanapopungua biashara yake huathirika pakubwa.

Aliongezea kuwa hali mbaya ya hewa na sheria zilizowekwa kulinda misitu ni changamoto anazokumbana nazo kila uchao.

“Hakuna mkazi wa hapa anayetaka kununua vyombo hivi kwa bei ninayouzia wazungu, watalii wanapopungua nalazimika kuuza bidhaa zangu kwa bei ya chini, kwa kuwa sina sehemu maalum hali mbaya ya hewa mfano kunaponyesha siwezi kutembeza bidhaa zangu,” Matheka alisema.

Hununua bidhaa zake kutoka kwa kampuni ya kuchongesha bidhaa za mbao ya Akamba. Alisema kwa sasa hutangaza bidhaa zake kupitia ukurasa wake wa Facebook na mitando mingine ya kijamii ili kufikia wateja wengi.

Bidhaa zake anaziuza kati ya Sh10,000-50,000 kutegemea na ukubwa na jinsi bidhaa ilivyorembwa.

Alisema biashara hiyo analenga watalii wa kimataifa.

Anahadithia kuwa biashara hiyo inamuwezesha kusomesha watoto wake walio katika shule za upili na mmoja chuo kikuu.

“Kupitia biashara hii nimeweza kukimu mahitaji yangu na ya familia, kama kusomesha, kujenga nyumba yangu binafsi, kulisha na kuwavisha wanagu,” alisema.

Aliongezea kuwa amejiunga na wafanyabiashara wengine wanawake kuimarisha wanawake wengine katika jamii kupitia kuunda chama kisha kufunguliana biashara tofauti.

“Tumefungua kikundi tunakiita Boresha Mama, kikundi hiki tunakitumia kuinuana kibiashara, tunasaidia wajane na wale wanawake waliotoka kwa ndoa zao kufuatia manyanyaso ya waume zao,” alieleza.

Ushauri wake kwa wanawake wengine ambao hawajaajiriwa ni wajihusishe katika shughuli zitakazowapatia kipato halali na si kujiunga na ukahaba au kuwa vitega uchumi.

Alieleza kuwa wasichana wengi kwa kutaka maisha mazuri kwa urahisi hujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wasiokuwa umri wao hivyo kuhatarisha maisha yao.

“Wasichana wengi wadogo na hata wakubwa hupenda kupata pesa kwa urahisi bila kutokwa jasho, jambo hili linapelekea wengi wao kupoteza maisha yao wakiwa bado wachanga kwa kufanya mambo kinyume na maadili kama kushiriki katika biashara ya ngono, kufanya ngono na wanyama na kadhalika,” Bi Matheka alieleza.

Hutumia miti aina ya mahogany kutengeza vinyago vyake.

You can share this post!

Qatar Airways yazindua safari ya ziada kutoka Doha hadi...

AKILIMALI: Si mzaha, avokado za Hass ‘dhahabu’...

adminleo