Makala

AKILIMALI: Kiwanda cha maziwa chapiga jeki uchumi wa wakazi kwa ajira na soko

July 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na RICHARD MAOSI

Kuna utajiri mkubwa katika sekta ya uzalishaji na usambazaji wa maziwa, hii ndiyo sababu wakati mwingine inashangaza kuona taifa likiagiza maziwa kutoka nje ilhali tuna mifugo wengi.

Uhitaji wa maziwa ni mkubwa sana, isipokuwa wakulima wengi bado hawana tajriba ya kujitengenezea bidhaa zinazotokana na maziwa.

Hii ndiyo maana wizara ya kilimo inawashauri kuwa makini, na kukabiliana na changamoto za ukame na soko la bidhaa hii adimu inayotumika na kila mtu.

Akilimali ilitangamana na shirika la Sabatia Cooperative Society kutoka kaunti ya Baringo, muungano unaowasaidia wafugaji vijijini kupata soko la nje kwa maziwa yao.

Wanasema wameamua kubuni mfumo mpya wa kuyakusanya, kuhifadhi na kusambaza maziwa kwa ushirikiano na wakulima wadogo.

Mwenyekiti wa shirika hilo Bi Rose Maiyo anasema walianzisha mradi huo ili kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana, na wakulima wakubwa waliowekeza katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Pili walitaka kutangamana na wakulima moja kwa moja ili wawapatie ujuzi wa namna ya kujiongezea kipato pamoja na kutatua matatizo yanayowakabili.

Alieleza kuwa shirika la Sabatia lilitaka kuwaongezea wakulima kipato, mbali na kuwahimiza kuhusu umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa kuyahifadhi.

“Pindi wakulima walipoanza kutuuzia maziwa yao, shirika la Sabatia lilianza kupata pesa na kukua, huku wakulima wakiendelea kufaidika,” Rose akasema.

Mbali na hayo, shirika lenyewe limeweza kuwapatia wakulima nafasi ya kupata mbolea kwa bei nafuu, lishe bora ya mifugo na mafunzo kabambe ya kuimarisha ufugaji.

Kwa siku moja shirika la Sabatia linaweza kukusanya kati ya lita 10,000-12,000 kutoka kwa wakulima vijijini ambao mara nyingi hutumia pikipiki kuyasafirisha hadi Eldama Ravine kwenye kiwanda.

Kulingana na Rose, shirika lao hutengeneza kati ya milioni 8-9 kila mwezi, jambo linalowafanya waendelee kujiongezea mtaji na kuwahudumia wakulima mashinani kwa kuwapatia mikopo na kuyaboresha mazingira ya ufugaji.

Rose anasema kuwa jambo la msingi ni kuwawezesha wakulima kuongeza thamani katika maziwa yao, na hili lilionekana pale walipoanza kuzalisha maziwa ya unga.

Isitoshe, Sabatia wamefanikiwa kuanzisha duka la kijumla linalotengeneza Yoghurt, Cheese na maziwa ya mgando katika mji wa Eldama Ravine linalohudumia kaunti nzima ya Baringo.

“Hatua hizi zimesaidia kupanua uwanda wa soko na kuwatengenezea vijana nafasi za ajira wanakopata mkate wao wa kila siku katika sekta ya uzalishaji wa maziwa,” akasema.

Lakini kabla hawajanunua maziwa kutoka kwa mkulima hatua zifuatazo zinahitajika kuzingatiwa.

1. Kuyakagua maziwa

Kabla ya kuchukua maziwa kutoka kwa wakulima hatua muhimu ni ukaguaji ili kubaini endapo maziwa ni halisia au la. Anaamini kuwa kuna mambo mengi yanayoweza kufanya maziwa yaharibike.

Ubora wa maziwa unaweza kubainika kupitia kutumia harufu ya maziwa. Endapo ng’ombe alipatiwa dawa nyingi kupita kiasi wakati wa matibabu dawa zinaweza kuathiri maziwa.

Pia mkulima anaweza kuwa mwangalifu kwa kuangalia rangi ya maziwa ambayo ni weupe uliosheheni.

“Mara nyingi wakulima wamekuwa wakiongezea maziwa yao maji, wakitarajia kuwapunja wanunuzi na kujiongezea kipato lakini teknolojia imefanikiwa kugundua hilo,” Rose asema.

Anasema kwa kawaida kuna kipimo kinachofahamika kama lactometer ambacho hutumika kutambua kama maziwa yameongezewa maji au la.

Lactometer hutumbukizwa ndani ya maziwa, na kitaaluma kifaa hiki kinaweza kutenganisha mafuta, maji na maziwa mazuri.

Kulingana na Lactometer maziwa yakiwa ni mazuri itasoma baina ya 1.026-1.036 tofauti na hapo basi maziwa yatakuwa yameonyezewa maji au kitu kingine.

Kwa kawaida, ndani ya maziwa huwa kuna protini, mafuta, chumvi na sukari inayofahamika kama lactose.

Aidha Rose anatoa tahadhari akiwaeleza wakulima kulisha mifugo wao kwa kutumia majani makavu kwa wingi, badala ya yale mabichi kwani wakati mwingine kipimo kinaweza kuonyesha kuwa maziwa yameongezewa maji ingawa hayakuongezewa kitu chochote.

2. Kuyahifadhi maziwa yasiharibike

Kwa sababu maziwa yanaweza kuharibika haraka endapo yatahifadhiwa katika sehemu ya joto jingi, yanahitajika kuwekwa katika sehemu baridi pindi baada ya kukamuliwa.

Rose anaeleza kuwa kwa sababu maziwa yana virutubishi vingi sana bakteria waharibifu wanaweza kuzaaana kwa haraka na kuyaharibu maziwa ya mkulima.

Aidha anaonya kuwa vifaa vya plastiki havifai kuhifadhi maziwa, kwa sababu hupatia maziwa harufu mbaya inayoweza kuyafanya yaharibike haraka.

Vifaa vya chuma kama aluminium visivyoweza kupata kutu ni mwafaka zaidi kutumika, katika suala la kuyalinda maziwa yasiharibike.

Maziwa yanapofika kwenye kiwanda hiki kwanza huchujwa na baadae, kusafirishwa hadi ndani ya cooling plants ambapo kiwango cha joto huwa kimepunguzwa.

Cooling plants hutumika kuhakikisha maziwa yanahifadhiwa katika sehemu safi, mbali na kupunguza kiwango cha joto ambacho kinaweza kufanya maziwa kuganda.

Mtambo wenyewe umetengenezwa kwa chuma aina ya aluminium ambayo ina uwazi mkubwa wenye mzunguko wa hewa safi.

Maziwa yanahitajika kuhifadhiwa katika kiwango cha nyuzi joto zinazopungua sita hivi kabla ya maziwa mengine kuruhusiwa ndani ya mtambo wenyewe masaa manne baadaye.

Kwa kutumia umeme wa stima, kiwango cha joto kinaweza kupunguzwa na kuongezwa sawia kulingana na muda unaotakiwa kuyahifadhi.

3. Kuyaongezea maziwa thamani

Kulingana na Rose, kiwanda cha Sabatia kimegundua kuwa wakazi wengi kutoka kaunti ya Baringo ni wafugaji wa ng’ombe kwa ajili ya maziwa. Kwa hivo wanategemea mifugo kwa takriban kila kitu.

Pana haja kubwa ya kuboresha malisho ya ng’ombe, maji na utafiti wa mbegu za dume wakati wa kutunga ujauzito ili kuendeleza kizazi.

Awali walikuwa wakikabiliana na changamoto za kupata soko kwa maziwa yao yaliyobaki kuharibikia majumbani pao, na hata wakati mwingine wakalazimika kuyamwaga.

“Kando na kuwashauri wakulima kufanya ufugaji unaostahili pia tunawapatia huduma za matibabu kwa mifugo wao ili kufanya ufugaji wenye tija,” akasema.

Sabatia wamefanikiwa kuanzisha duka la kijumla mjini Eldama Ravine wanakotengenezea maziwa ya mgando, cheese, ghee na yoghurt kama juhudi za kuongezea maziwa yao thamani.

Biashara hiyo imewasaidia vijana wengi kutoa msururu wa huduma za kuyasambaza na kujifungulia maduka yao ya kibinafsi katika kaunti nzima ya Baringo.