• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 8:55 AM
Kiwanda cha maziwa Murang’a kilichoangushwa na ufisadi kufufuliwa

Kiwanda cha maziwa Murang’a kilichoangushwa na ufisadi kufufuliwa

NA MWANGI MUIRURI

KIWANDA cha wakulima wa maziwa Murang’a kilichozinduliwa 2019 kwa kima cha Sh1. 5 bilioni japo kikasambaratika miaka mitatu baadaye kufuatia ufisaidi kinapangiwa kitafufuliwa. 

Kilianzishwa na Gavana wa kwanza Murang’a, Bw Mwangi wa Iria) aliyehudumu kati ya 2013 hadi 2022, lakini kikaanguka baada ya kuporwa mitambo yenye thamani ya Sh350 milioni.

Isitoshe, kilifilisika kikiwa na deni la Sh400 milioni.

Wa Iria alizindua kiwanda hicho kama ahadi yake kuu ya kuweka pesa mifukoni kwa wakulima na kikawa cha kuinua matumaini ya pato kwa wanachama karibu 200, 000 waliokuwa wamekumbatia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Bw Wa Iria akiingia mamlakani 2013, lita moja ya maziwa katika Kaunti Murang’a ilikuwa ikinunuliwa Sh10 pekee na madalali, lakini baada ya mwaka mmoja, bei hiyo ikapandishwa hadi Sh35.

Gavana huyo ambaye kwa sasa ni mstaafu alitangaza kwamba kila dalali wa maziwa ndani ya kaunti lazima angenunua lita moja kwa Sh35 kwenda juu, akisema alikuwa tayari kutenga pesa za kaunti kuboresha sekta ya maziwa.

Alianza kununua maziwa moja kwa moja kutoka kwa wakulima na madalali wakaanza kushindania bidhaa hiyo kupitia nyongeza ya bei, hali ambayo iligeuza Murang’a kuwa kaunti ya kipekee ambayo ilikuwa imefanikiwa kudhibiti bei ya maziwa kwa mkulima kwa Sh35 kwenda juu.

Mwaka wa 2019 Gavana wa Iria alizindua kiwanda hicho ambacho kilianza kupakia maziwa ndani ya pakiti na pia kutengeneza maziwa mala, hali ambayo ilipandisha bei ya lita moja tena hadi Sh42.

Aidha, Wa Iria alikuwa ametoa ahadi ya kuzidisha malipo hayo hadi Sh80 kabla ya 2025 na awe pia akilipa bonasi ya Sh5 kwa kila lita.

Maono hayo yaliyoenda hadi 2025 huku awamu yake ikitamatika mwaka wa 2022 inasemwa kwamba ndiyo ilizua hujuma dhidi ya kiwanda hicho kwa kuwa washindani walimuona kama aliyekuwa na nia hata ya kuamua mrithi wake angekuwa ni nani ili aendeleze ajenda hiyo ya bei.

“Washindani wangu ndio walianza kuchochea wakulima waache kuwasilisha maziwa yao kwa mradi huo. Wao wenyewe wakaandaa kesi dhidi ya mradi huo wa wakulima na wakaunda kampuni zao zilizofadhiliwa kisiasa ili zinunue lita moja kwa Sh45 hivyo basi kuwashawishi kwamba kulikuwa na afueni nje ya kiwanda chao,” Wa Iria anasema.

Bw wa Iria alizidisha njama dhidi yake alipotangaza kwamba alikuwa awanie urais na hatimaye akajiunga na mrengo wa Azimio la Umoja, hali ambayo ilifanya vita dhidi yake na miradi yake kuchacha.

Kiwanda cha maziwa cha Murang’a ambacho kitafufuliwa baada ya kusambaratika mwaka wa 2022 Picha MWANGI MUIRURI

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu anasema kwamba kiwanda hicho kilikuwa katika mkondo mzuri wa utendakazi hadi wakati ambapo kulizuka siasa za ushindani na wakulima wakachochewa wakome kuwasilisha maziwa kwa mradi wa Bw Iria.

Aidha, Bw Nyutu anaongeza kwamba usimamizi wa kiwanda hicho ulikuwa na dosari kwa kuwa wengi wa manyapara hawakuwa na ujuzi wa kuongoza mradi wa faida, bali walikuwa tu vibaraka wa kisiasa.

“Kile hatuwezi tukasahau ni kwamba kuna ripoti ambayo imeandaliwa na kamati ya bunge la kaunti kuhusu biashara na viwanda ikionyesha kwamba kuna mitambo ya kiwanda hicho ambayo ni ya thamani ya Sh300 milioni na ambayo haijulikani iliko. Pia, kuna deni la Sh400 milioni. Kando na kufufua kiwanda hicho, tunataka kujua ukweli halisi na wale waliosababisha hali hiyo washikwe na washtakiwe,” akasema.

Gavana w Murang’a, Bw Irungu Kang’ata alisema kwamba tayari kiwanda hicho kimekabidhiwa mikononi mwa muungano wa ushirika wa wakulima wa Murang’a na ambapo amekipa Sh15 milioni za mwanzo ili kukisaidia kuzindua operesheni.

“Kwa sasa kiwanda hicho kinatengeneza maziwa mala kutokana na maziwa ambayo yanakusanywa kutoka kwa wakulima. Hafla kamili ya kukizindua ni Machi 24, 2024   ambapo Waziri wa Vyama vya Ushirika Bw Simon Chelugui ndiye atakuwa mgeni wa heshima,” akasema Gavana Kang’ata.

Hayo yakijiri, wakulima wameteta kuhusu visa vya wizi wa mifugo katika kaunti hiyo na pia bei ya juu ya chakula cha mifugo cha madukani.

Hali hiyo inasemwa kuchangia idadi ya mifugo kuzidi kudidimia hivyo basi kusababisha upungufu wa bidhaa za ufugaji, hasa maziwa.

“Bila ng’ombe ina maana kuwa hakuna maziwa. Ukizindua upya kiwanda hicho cha maziwa, ihakikishwe kwamba wizi wa mifugo umezimwa na bei pamoja na ubora wa chakula cha  mifugo kwa pamoja zizingatiwe ili kuzua manufaa halisi ya mradi huo,” akasema mwenyekiti wa umoja wa wafugaji na biashara husika Bw Martin Kamande.

[email protected]

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Uzinduzi wa vitabu vya Kibajuni kudumisha tamaduni  

Mbinu za kina mama kukabiliana na wizi wa mifugo

T L