Kiwanda kipya cha klinka ya simiti chatoa nafasi 2,500 za kazi Pokot, je kitamaliza ujangili?
NA OSCAR KAKAI
WAKAZI katika Kaunti ya Pokot Magharibi wana matumani makubwa kunufaika na kiwanda cha kutengeza klinka ya saruji kilichogharimu mabilioni ya pesa eneo la Sebit kaunti ndogo ya Kipkomo kwenye barabara kuu ya Kapenguria-Lodwar.
Kiwanda hicho ambacho kimengojewa kwa muda mrefu kimejengwa na kampuni ya Simba Cement na kitazinduliwa Jumatatu na Rais William Ruto kwa lengo la kukomesha ujangili na wizi wa mifugo katika eneo hilo.
Klinka ni bidhaa ambayo huzalishwa kutoka kwa mchakato wa kutengeneza simiti na hutumika kubandika bidhaa hiyo.
Kutokana na kuwepo kwa kiwanda hicho, wakazi wa kaunti hiyo wanatazamia kubadilisha maisha yao.
Mradi huo pia utasaidia kuinua uchumi wa eneo hilo kutoka kwa kiwango cha juu cha umaskini.
Vijana wa eneo hilo wana imani kuwa kiwanda hicho kitawapa ajira.
“Tunatarajia kuwa wawekezaji wengi sasa watakuja,”asema Emmanuel Limarusi, kijana mwenye hana kazi.
Mkazi Augustine Loria anasema kuwa tayari kuna mabadiliko ya kiuchumi na kiwanda hicho kitainua wakazi wa eneo hilo ambao wameathirika na visa vya utovu wa usalama.
“Hitaji la mashamba liko juu kwa lengo la kujenga nyumba za kukodi. Kwa mfano robo ya ekari ya ploti inauzwa kwa Sh700,000. Wakazi wanapata kazi kwenye kiwanda,” anasema.
Anasema kuwa wana biashara wanatarajia kuwa biashara zao zitaimarika na uchumi wa kaunti nzima kuinuka.
“Hii ni dhahabu. Tunatarajia kunufaika kutoka kwa ardhi ya mababu zetu,” anasema Bw Loria.
Felix Loliposia, mkazi ambaye anafanya kazi ya ulinzi katika kiwanda hicho anasema kuwa anaona kiwanda hicho kama suluhu ya visa vya ujangili suala ambalo huletwa na ukosefu wa kazi za kiuchumi.
“Tunataraji vijana wengi kutoka maeneo ambayo yaliathirika watakuja kusaka kazi hapa,” anasema Bw Loliposia.
Katibu wa uchimbaji madini Elijah Mwangi ambaye alizuru eneo la kiwanda hicho Jumatano alisema kuwa kiwanda hicho ni hatua kubwa kwa kufungua nafasi za kazi kote nchini na itazipa kampuni zote bidhaa za saruji.
Kampuni zitapata klinka ya kutosha
“Kampuni zitapata klinka ya kutosha na hata nyingine kupelekwa maitafa ya kigeni. Kwa sasa uzalishaji unasaidia viwanda vyote vya saruji nchini,”alisema Katibu Mwangi.
Alisema kuwa kiwanda hicho kwa sasa ina uwezo wa kuajiri watu 2,500 ambao wengi ni wenyeji na kusaidia kuinua uchumi wa sekta mbali mbali.
“Jamii itanufaika pakubwa kushinda tangu ujenzi uanze. Tumeona nyumba za kukodi zikijengwa,”alieleza akisema kuwa uchukuzi umeongezeka.
Katibu huyo alifichua kuwa mapato kutoka kwa kiwanda hicho yatalipwa kwa serikali kuu, asilmia 20 yatarejea kwa serikali ya kaunti na asilimia 10 kwa jamii na asilimia 1 kwa wakazi wa karibu.
Katibu Mwangi aliongeza kusema kuwa wakazi wananufaika na elimu, afya na usaidizi kutoka kwa kampuni na msaada kwa jamii akitaka wakazi kubuni kamati ya maendeleo.
Gavana wa Pokot Magharibi Simon Kachapin anasema kuwa kiwanda hicho kitasaidia vijana kukoma kujihusisha kwenye ujangili na wizi wa mifugo na itakuwa kifunguo kwa waekezaji.
Bw Kachapin alisema kuwa, kiwanda hicho kitachangia maendeleo ya kubadilisha eneo hilo.
“Itapunguza wizi wa mifugo ambao jamii za Pokot, Turkana na Marakwet zimekuwa zikijihusisha nao,”akasema Bw Kachapin.
Anasema kuwa kiwanda hicho kitachochoea uchumi kuimarika kupitia ajira na nafasi zingine.
Bw Kachapin alifichua kuwa kiwanda hicho kitasaidia miradi nyingi kufanyika kama barabara, afya na shule.
Mwenyekiti wa kampuni ya Devki Narendra Raval almaarufu Guru anasema kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kuajiri wengi moja kwa moja na hata kwa umbali.
Bw Guru anasema kuwa mradi huo utabadilisha maisha ya wakazi na kuwapa msaada.
“Tutajenga hospitali, shule na kupeana ufadhili wa masomo ya juu. Tunataka kubadilisha sura ya kaunti ya Pokot Magharibi kwa kuhuzishwa na bunduki,”akasema Dkt Raval.
Kiwanda hicho kitakuwa kikitoa tani 6,000 za klinka ambayo ni tani milioni 2 kila mwaka. Klinka ni bidhaa maalumu kwa utengezaji simiti. Baada ya kusiagwa katika kaunti ya Pokot Magharibi, itasafirishwa hadi kwenye kiwanda cha saruji mjini, Eldoret.
Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga alizindua ujenzi wa kiwanda hicho mwaka 2010 eneo la Sebit lakini ukachelewa.