Makala

‘Kona za masafara’ zaongezeka jijini Nairobi vijana wakikosa ajira

Na JACKSON NGARI, MICHAEL OCHIENG’ September 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA wapita-njia, vijana wanaoketi katika bustani au maeneo kadhaa ya jiji huonekana kama wavivu au wasio na shughuli.

Lakini wengi wao ni wahitimu wa vyuo vikuu; wahandisi, walimu, wanasayansi wa kompyuta –Wakenya waliowahi kuamini kwamba elimu ingewafungulia milango ya mafanikio.

Sasa, siku zao hupita wakiwa wameketi au kulala kwenye nyasi katika maeneo yanayojulikana kama “kona za masafara” jijini Nairobi, wakibeba wasifu kazi na vyeti kwenye mafaili au mikoba yao.Kadri ukosefu wa ajira unavyozidi kuwa tatizo, maeneo haya ya kupumzikia kwa vijana wasiokuwa na kazi yameongezeka.

Taifa Leo ilizuru bustani za Jeevanjee Gardens, Nairobi Cinema Park, KenCom, na Uhuru Park, miongoni mwa nyingine, ambako wanaume na wanawake hukusanyika wakitumaini kupata kibarua au hata tu kupitisha muda.

Katika bustani ya Jeevanjee, Nairobi, vijana wengi waliohitimu vyuo vikuu wanaketi kwenye viti na nyasi, wakisubiri kwa matumaini ajira au kibarua cha siku. Maisha magumu ya mtaani sasa yamewalazimisha kutangatanga mitaani na mafaili ya vyeti chini ya mikono. Moses Mbugua, 36, mhitimu wa uhandisi wa kompyuta, alilazimika kuacha biashara yake na kilimo baada ya hali ya uchumi kuwa ngumu.

“Nimechoka kuhangaika. Nimetuma maombi kila mahali lakini hakuna kazi. Hapa ndipo ninakuja kulala mchana. Usiku huenda KPCU kusaidia abiria kutafuta magari ya kusafiri. Nikibahatika, ninapata Sh100 au Sh200,” anasema.

Wakati mwingine, wanasiasa huwalipa Sh500 kusimama nyuma yao kwenye mikutano ya waandishi wa habari. “Ni pesa ya siku moja tu, si kazi ya kudumu,” Mbugua anaeleza.Willy Maina, 28, ni mhitimu wa Shahada ya Biashara kutoka Zetech University. CV yake ina kurasa saba na ameshatuma zaidi ya maombi 100, lakini bado hajawahi kupata ajira ya kudumu.

“Kila CV ni Sh70 kuchapisha. Nimetumia maelfu ya pesa, lakini bado hakuna kazi,” asema.Maina anasema kama humjui mtu serikalini, hupati kazi yoyote.Hali hiyo imemlazimu kuongoza kikundi cha kijamii, Nairobi Masafara Foundation, kinachosaidia familia za mitaani kupata vitambulisho na huduma za kijamii.

Alikuwa na matumaini kuwa kazi hiyo ingegeuka kuwa ajira, lakini mpaka sasa ni kujitolea tu. Ili kujikimu, anawazia huuza data za shirika hilo kwa wanasiasa wanaotafuta kura.Kwa Enoch Odhiambo, 25 aliye na shahada ya Hisabati na Takwimu (Chuo Kikuu cha Rongo), maisha yamekuwa magumu. “Nilikuja Nairobi nikiwa na matumaini, lakini kila siku ninaomba kazi bila mafanikio.”

Nikikaa nyumbani, nitapata msongo wa mawazo.”Ripoti ya Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu na ile ya hali ya Uchumi zinaonyesha kuwa mwaka jana, zaidi ya wahitimu 123,000 walihitimu kutafuta kazi, lakini ni kazi 78,600 pekee zilipatikana.

Utafiti wa TIFA wa Septemba 2025 ulionyesha mmoja kati ya Wakenya wanne hana ajira ya kudumu.Katika hali hii, vijana hawa wanaendelea kuamka kila siku, wakielekea “Kona za masafara” kwa matumaini kuwa siku moja, maisha yatabadilika. “Huku tunapumua,” anasema Maina. “Ni mahali pa amani, hata kama hatuna kazi