Makala

Kondomu 50,000 kusambazwa kongamano la ugatuzi Homa Bay

Na GEORGE ODIWUOR August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BARAZA la Kitaifa la Kudhibiti Milipuko ya Maradhi (NSDCC) linapanga kusambaza kondomu 50,000 wakati wa Kongamano la Ugatuzi la mwaka wa 2025 litakalofanyika mjini Homa Bay kuanza leo.

Hatua hii inalenga kupunguza maambukizi ya virusi vya HIV ambavyo bado ni vya juu katika eneo hilo.

Mratibu wa NSDCC katika eneo hilo, Bw Stephen Oyugi, alisema kuwa angalau kondomu 10,000 zitawekwa katika maeneo ya kimkakati kila siku wakati wa kongamano hilo.

Sehemu ya kwanza ya usambazaji ilifanyika usiku wa Jumapili kwa watu waliokuwa wakihudhuria tamasha la muziki katika Hifadhi ya Kitaifa ya Ruma.

Hifadhi hiyo iliandaa toleo la pili la mbio za Roan Antelope Half Marathon siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, kabla ya mbio hizo, wakazi wa eneo hilo na mashabiki wa muziki wa Luo walishiriki dansi ambapo waliburudishwa na wanamuziki wa Ohangla.

Bw Oyugi alisema NSDCC ilishirikiana na idara ya afya ya kaunti kusambaza kondomu kwa waliohudhuria hafla hiyo.

“Kile tunakabiliana nacho kwa sasa ni utupaji wa kondomu zilizotumika. Zilisambazwa kwenye maeneo ya wazi na zilitumika katika vichaka. Hili ni changamoto lakini tunapaswa kuzitupa kwa njia nzuri kulinda  mazingira,” alisema.

Alisema kuwa matumizi ya vichaka kwa shughuli za ngono bado ipo hasa wakati watu wanapokutana katika maeneo ya wazi kama hifadhi hiyo.

“Hili lilikuwa tukio la kipekee. Kwa kuwa ni hifadhi na kuna maeneo yenye giza, tulikuta kondomu nyingi zilizotumika, ishara kwamba vichaka vinatumiwa kwa ngono na mazingira yalitoa fursa kwa hilo kutokea,” alisema Bw Oyugi.

Kwa mujibu wa NSDCC, kiwango cha maambukizi ya HIV katika Kaunti ya Homa Bay ni asilimia 10.6.

Bw Oyugi alieleza kuwa matumizi ya kondomu ni moja ya njia bora za kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV.

Alisema taasisi hiyo inanuia kusambaza kondomu wakati wote wa kongamano la ugatuzi.

“Tuna akiba ya kutosha na hafla hii imepangwa vizuri kwa upande wa usambazaji wa kondomu,” alisema Bw Oyugi.

Baadhi ya maeneo ambapo kondomu zitasambazwa ni pamoja na maeneo ya malazi, ukumbi wa kongamano na sehemu za kimkakati ambapo watu wanaweza kuzipata kwa urahisi.

Mnamo Aprili mwaka huu, Gavana wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Junior, alilazimika kuomba msamaha baada ya kutoa kauli kuhusu mienendo ya wagonjwa wa HIV katika Homa Bay.

Gavana Kilonzo, ambaye alikuwa akiwatakia safari njema wanamichezo kutoka kaunti yake waliokuwa wakielekea Homa Bay, aliwashauri vijana kutoka Makueni kuwa waangalifu, akisema makosa madogo yanaweza kuwafanya kuambukizwa virusi vya HIV.

Vijana hao walikuwa wakihudhuria toleo la 10 la Michezo ya Vijana ya Muungano wa Kaunti za Kenya (KYISA), hafla inayoshirikisha timu kutoka kaunti zote 47.

Bw Kilonzo, kwa kusisitiza, aliwaambia vijana wasiharibu mambo wakiwa Homa Bay.

Akinukuu wimbo Vuta Pumzi wa Longombas unaozungumzia masuala ya kijamii kama HIV, aliwataka vijana wa Makueni wasijihusishe na tabia zisizofaa wakiwa Homa Bay.

“Kama mzazi, ni lazima niseme hili kwa sababu nitakuwa mzazi asiyejali ikiwa sitasema. Homa Bay ni kaunti nzuri lakini wanapenda starehe, tofauti na Makueni,” alisema.

Alidokeza kuwa mtindo wa maisha unachangia kuenea kwa virusi vya HIV miongoni mwa wakazi.

Kwa mujibu wa gavana huyo, HIV imekuwa kama ugonjwa wa kawaida miongoni mwa wakazi wa Homa Bay.

Video ya Gavana Kilonzo akitoa matamshi hayo ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Bw Oyugi alisema unyanyapaa kuhusu HIV ni kikwazo kikubwa katika kupokea huduma za afya.

“Iwapo watu wanaweza kushinda unyanyapaa na kufanya mazungumzo kuhusu matibabu kuwa ya kawaida, basi hilo ni jambo la msingi katika kukabiliana na HIV,” alisema Bw. Oyugi.

Baadaye Gavana Kilonzo alituma barua ya kuomba msamaha akisema hakuwa na nia ya kudhalilisha au kuwabagua watu wa Homa Bay.

“Nilikua nawaonya vijana. Natambua kwamba maneno yangu kuhusu HIV na Ukimwi katika Homa Bay huenda yalieleweka vibaya,” aliandika kwenye barua ya msamaha iliyochapishwa na Gavana wa Homa Bay, Bi Gladys Wanga.

Bi Wanga alisema ombi hilo la msamaha lilikubaliwa.