Korti yasimama na mwanamke aliyehepa na Sh166,700 za mwalimu mpenziwe
MWANAMUME mmoja amepata pigo baada ya Mahakama Kuu mjini Voi kukataa kumlazimisha mshirika wake wa zamani wa kibiashara kumrejeshea Sh166,700 alizompa ili kuanzisha biashara ya pamoja.
Jaji Asenath Ongeri aliamua kuwa fedha hizo hazikuthibitishwa kama mkopo au uwekezaji wa pamoja.
“Kauli ya Phelister Masalo kwamba pesa hizo zilikuwa zawadi ya kuthamini uhusiano wao inaweza kuaminikuwa kuwa ya kweli, hasa kutokana na ukosefu wa makubaliano yaliyoandikwa au mashahidi huru,” alisema jaji huyo.
Kwa mujibu wa mahakama, Mkala Maghanga alishindwa kuthibitisha kuwa fedha hizo zilitolewa kama mtaji wa biashara badala ya zawadi, ambayo haiwezi kudaiwa tena.
“Nabaini kuwa mwanamke huyo hastahili kurejesha fedha hizo, kwa kuwa mwanamume huyo hakuthibitisha kuwa ilikuwa michango ya biashara inayoweza kurejeshwa,” alisema jaji katika uamuzi wake wa Mei 16.
Hii ilikuwa mara ya pili kwa Maghanga kushindwa katika juhudi zake za kudai kurejeshewa fedha hizo, baada ya mahakama ya mahakimu kule Taveta kukataa ombi lake kwa msingi kuwa fedha hizo zilikuwa zawadi kwa mwanamke huyo na hivyo hazirejesheki kisheria.
Maghanga alikuwa amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ambao ulikataa kumlazimisha mwanamke huyo kumrejeshea pesa hizo, ikibaini kuwa hakukuwa na makubaliano halali ya kibiashara yanayoweza kutekelezwa kisheria.
Kesi hiyo ilianza wakati Maghanga alipowasilisha kesi hiyo katika mahakama ya Taveta, akitaka kurejeshewa Sh166,700—kiasi alichodai alikitoa kuanzisha biashara na Masalo.
Masalo, hata hivyo, alikanusha madai hayo, akisema alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu huyo na fedha hizo zilikuwa zawadi ya mapenzi kati yao.
Maghanga aliieleza mahakama kuwa walikubaliana kwa maneno na Masalo mwishoni mwa Oktoba 2022 kufungua baa ndogo mjini Taveta kama washirika sawa, na alimkabidhi Sh166,700 kwa njia ya pesa taslimu na vifaa kama mtaji wa kuanzia.
“Biashara ilianza vizuri, lakini kufikia mwishoni mwa Novemba, Masalo alianza kuwa na siri na akakataa kutoa taarifa kuhusu mapato ya mauzo,” alisema Maghanga.
Alidai kuwa Masalo alikubali awali kurejesha fedha hizo lakini baadaye alibadili msimamo, jambo lililomsababisha kumtumia barua akidai fedha zake na hatimaye kumshtaki mwanamke huyo.
Katika majibu yake, Masalo alikataa madai hayo, akisema kesi hiyo haikuwa na msingi na ilifunguliwa kwa nia mbaya baada ya kugundua kuwa Maghanga alikuwa ameoa, jambo lililomfanya avunje uhusiano wao wa kimapenzi.
Alipinga rufaa hiyo akisema Maghanga alishindwa kuwasilisha ushahidi madhubuti wa kuwepo kwa makubaliano yanayoweza kutekelezwa
“Pesa na vifaa hivyo vilitolewa kwa sababu ya mapenzi na havikukusudiwa kuwa mkopo au uwekezaji,” alisema.
Aliongeza kuwa ushahidi pekee uliowasilishwa—maandishi ya mkono, jumbe za WhatsApp, na risiti zilizoandikwa kwa jina lake—havikusainiwa, hazikukuwa na tarehe, na haziwezi kuthibitishwa.
Pia alibainisha kuwa hakuna mashahidi waliowasilishwa kuthibitisha madai ya Maghanga.
Mahakama ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya mahakimu , ikisema kuwa zawadi zinazotolewa katika muktadha wa uhusiano wa kimapenzi haziwezi kudaiwa tena kisheria chini ya sheria za Kenya.
Jaji aliamua kuwa Maghanga alishindwa kuthibitisha kuwepo kwa mkataba halali kama inavyohitajika kisheria, na hivyo uamuzi wa mahakama ya awali wa kutupilia mbali dai hilo ulikuwa wa haki.