Makala

Kozi za kiufundi zapigiwa upatu kufaa uchumi wa Kenya

April 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

UFICHUZI wa Naibu Rais William Ruto kuwa kozi za kiufundi hapa nchini zitafadhiliwa kwa Sh100 bilioni kuanzia sasa hadi 2025 ni ushahidi tosha kuwa serikali imejituma kusaka suluhu la ukosefu wa ajira, wadadisi wanasema.

Ni msimamo wa serikali ambao umetajwa kuwa utafaa pakubwa hatua za kuafikia malengo ya ruwaza ya 2030 ambapo uchumi unatazamiwa kuafikia pato la kadri kwa wote.

Aidha, kozi za kiufundi zinapigiwa upatu mkuu wa kusaidia vijana wengi kuafikia maamuzi ya kitaaluma ya kujigeuza kuwa waajiri badala ya waajiriwa.

Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa anasema kuwa huu ni mtazamo thabiti wa kuwekeza rasilimali kwa uchumi ili kuupa ule msukumo wa kutegemea taaluma za kiufundi kujenga uchumi badala ya kutegemea ajira za afisini.

“Mtazamo huu wa kuwekeza kwa kozi za kiufundi utasaidia kutupa ule mwamko mpya wa kutegemea viwanda vidogovidogo kustawisha jamii na uchumi,” anasema.

Kwa mujibu wa mwanakamati katika bunge la Seneti kuhusu Elimu, John Kinyua ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Kirinyaga soko la ajira nchini litageuka kuwa la walio na uwezo kamili wa kiufundi badala ya kuwa na uwezo wa kuelekeza ufundi.

“Kuna ushahidi tosha kuwa serikali kwa sasa imejituma kubadilisha hali ya kiuchumi nchini. Kitita hiki kitatumika kujenga vituo 130 vya kiufundi na ambavyo vitawekwa mitambo na  vifaa muafaka kuwezesha wanataaluma kujipa ule uhalisia na ungangari wa ushindani kimataifa,” anasema.

Katika bajeti ya 2018/19 serikali ilizidisha bajeti ya kozi hizi kwa asilimia 175 ambapo kutoka Sh6 bilioni, ilitoa Sh16.5 bilioni.

Ipo haja

Waziri wa Fedha, Henry Rotich alisema kwamba kuzidisha bajeti hiyo kulikuwa na maana kwamba kunahitajika ujenzi wa vituo vingi vya kiufundi, kuvihami kwa wataalamu wa kuwaelimisha wanafunzi na pia kuzindua mtaala mpya wa elimu ili kuvipa vituo hivyo uwezo wa kujenga bongo mufti kitaaluma kwa mujibu wa ulinganisho wa kimataifa.

Prof Margaret Kamar ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati ya elimu ya Seneti anasema kuwa bajeti hiyo ya Sh100 bilioni itolewe kwa awamu za Sh25 bilioni Juni 2019 na kisha masalio yasambazwe kwa bajeti zitakazofuata za hadi 2023/2024.

Anasema kuwa kwa sasa waajiri wengi wameachana na ule mtindo wa kushikilia ushahidi wa shahada kuwa wewe ni mtaalamu hadi kwa ushahidi wa uwezo kamili wa kuchapa kazi.

“Hali hiyo ndiyo tunakimbizana nayo ambapo tunahitaji ushahidi kuwa unaweza kuunda barabara au kuunda mifereji ya maji bali sio eti uko na uwezo wa kusimamia wajkenzi hao wakichapa kazi hizo,” anasema.

Anasema kuwa serikali itashirikiana na sekta ya kibinafsi kufanikisha ajenda hii ikizingatiwa kuwa miradi mingi ya kimaendeleo inafadhiliwa na kutekelezwa chini ya ushirika huo.