Makala

Kuharibiwa kwa pete, muhuri miongoni mwa taratibu kuelekea kumpata Papa mpya

Na CHARLES WASONGA April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kifo cha Papa Francis hapo Jumatatu, kipindi cha maombolezi na maandalizi ya uchaguzi wa mrithi kitaanza kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Katoliki.

Jumla ya makadinali 252 wa kanisa hilo kutoka kote ulimwenguni wanatarajiwa kukutana kati ya siku 15 na 20 jijini Vatican.

Hata hivyo, makadinali 138 pekee, ambao hawajatimu umri wa miaka 80, ndio wataruhusiwa kushiriki upigaji kura.

Lakini punde tu Papa Francis alipofariki jana, majukumu yake rasmi yalitwaliwa na msimamizi wa afisi yake ambaye ni Kadinali Kevin Farrell, raia wa Amerika.

Yeye ndiye alitangaza rasmi kifo cha Francis, huku akiandamana na daktari na akibeba cheti cha kifo. Mwili wake hautafanyiwa upasuaji.

Jana, usimamizi wa Vatican ulisema kuwa mwili wa Francis uliwekwa ndani ya jeneza katika ukumbi wa maombi katika makazi yake ya Saint Martha kuanzia saa kumi na mbili jioni.

Kadinali Farrell pia atafunga makazi ya Papa na kuharibu pete na muhuri wake, inayotumiwa kuhalalisha stakabadhi, ili zisitumike na mtu yoyote.

Baadaye, yeye na makadinali wengine wasaidizi wataandaa ratiba ya maombolezi ya Papa Francis-ikiwemo tarehe ya ibada ya wafu na mazishi.

Kulingana na kanuni za Kanisa Katoliki, kipindi cha maombolezo ya Papa hudumu kwa siku tisa na huanza siku nne au sita baada ya kifo cha Kiongozi huyo.

Kadinali Farrell na kikosi chake pia wataamua siku ambayo mwili wa Papa utapelekwa katika Kanisa la St Peter’s Basilica, kabla ya mazishi, ili wanaumini watoe heshima zao za mwisho.

Kwa kuwa Papa Francis hakupenda sherehe nyingi za kanisa hilo, aliomba kwamba mwili wake usiwekwe juu ya kifaa kirefu ndani ya kanisa la St Peter’as Basilica ili waumini wautazame.

Kwa hivyo, waumini wataweza kuutazama mwili wake ukiwa ndani ya jeneza lisilofunikwa.

Kulingana na desturi za Kanisa Katoliki, ibada ya kumwaga Papa Francis itafanyika katika uwanja wa St Peter’s Square ndani ya siku nne ua sita baada ya kifo chake.

Kulingana na wasia wake, Papa Francis hatazikwa Vatican, katika Kanisa la St Peter’s Basilica bali katika Kanisa la Basilica of St Mary Major, karibu na alikozikwa Madonna.

Atakuwa ni Papa wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya karne moja, kutozikwa katika Kanisa hilo kubwa la St Peter’s Basilica, Vatican.

Papa Francis pia aliomba kwamba azikwe katika jeneza lililotengenezwa kwa mbao ya kawaida, kinyume na watangulizi wake waliozikwa kwenye majeneza ya bei ghali.

Mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya utaanza siku 15 baada ya kifo cha Francis au kabla ya siku 20.

Papa mpya atachaguliwa na kamati ya makadinali ambao huteuliwa na Papa mwenyewe na wasiwe na umri wa miaka 80 na zaidi.

Kabla ya uchaguzi huo kufanyika kundi la makadinali ndio huongoza Kanisa Katoliki, ingawa mamlaka yao yamedhibitiwa.