• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Kukatizia mlevi pombe ghafla kunaweza sababisha kifo, Gachagua aambiwa 

Kukatizia mlevi pombe ghafla kunaweza sababisha kifo, Gachagua aambiwa 

NA MWANGI MUIRURI 

BAADHI ya madaktari wameonya serikali dhidi ya kuachisha ghafla walevi pombe wakihoji kwamba huenda wengine wakaaga dunia “kwa kuachishwa uraibu wao”.

Naibu Rais, Rigathi Gachagua anaongoza kampeni dhidi ya pombe haramu na hatari, na madaktari wanasema, baadhi wamezoea kufungua ‘lock’ kabla ya kuanza majukumu ya siku, hivyo basi kuna uwezekano kukumbwa na nyakati ngumu.

Lock ni lugha ya mtaani inayomaanisha mlevi kuhitaji kunywa pombe asubuhi ili mwili uchangamke, hii ikiwa ni ishara kwamba ulevi umepenya hadi kwa nafsi na kuwa kiungo cha uhai.

Haya yamejiri wakati serikali iko mbioni kuangamiza pombe za mauti sokoni na pia mihadarati kupitia misako ya kitaifa.

Katika eneo la Kati ambapo misako hiyo imetiwa makali ya kipekee, visa vya walevi kutetemeka, kutokwa na jasho, sauti kupotea na kuwashwa ngozi vimeanza kujidhihirisha huku wengine hata wakizirai kutokana na kukosa dozi ya ulevi.

Wengine wamesema bila ulevi, wanaathirika, ikiwemo kuishiwa na nguvu za kiume na pia wanawake kupoteza hamu ya kujamiiana.

“Ni ukweli kwamba waathiriwa wa ulevi wa pombe na mihadarati kwa kawaida huwa ni wagonjwa ambao wanafaa kutibiwa wala sio kunyimwa pombe ghafla,” asema Dkt Inyathiu Kive.

Anaongeza kwamba “matibabu ya mlevi mzooefu ni ghali na athari za kumwondoa kwa uraibu huo hata zinaweza kuwa mauti”.

Mkuu wa kitengo cha e-health katika Wizara ya Afya Bw Onesmus Kamau anakiri kwamba uraibu wa ulevi ni ugonjwa hatari.

“Uzoefu ni hatari na hata unaweza ukawapa wengine mshtuko wa moyo baada ya kuzimiwa dozi. Walioathirika zaidi wanafaa kuondolewa kwa matumizi kwa utaratibu wakiwa na wataalamu wa kimatibabu kuwaongoza,” anaeleza.

Bw Kamau anasema kwamba baadhi ya waathiriwa wanafaa kutibiwa wakiwa wamelazwa hospitalini ili hali zao ziratibiwe kwa karibu kwasababu kuna dawa hutumika kusaidia mwili kuondoa madini ya pombe.

“Kumwondoa kutoka uraibu huo mara moja hata kunaweza geuza mwathiriwa kuwa kichaa. Hasira zinaweza zikamsonga ghafla na atekeleze tukio la kikatili bila kukusudia,” asema.

Aliyekuwa mbunge wa Naivasha, Bw John Mututho tayari ametoa tahadhari kwamba kuachisha walevi dozi zao pasipo kuwaweka chini ya mpango maalum wa kimatibabu ni hatari.

“Tuzingatie mikakati ya kitaaluma. Hawa waathiriwa ni wagonjwa. Tukiondoa pombe tunafaa tuelewe tumeacha wagonjwa nyanjani. Tisiwasahau,” anasema mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuhudumu kama mwenyekiti wa

Mamlaka ya Kupambana na Pombe na Matumizi ya Dawa za Kulevya (NACADA).

Kulingana na Bw Mututho, serikali inapaswa kuwa na mpango maalum kusaidia waraibu wa pombe kuwa soba badala ya kuwakomesha mara moja.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kuanza kuvuna pesa kupitia Facebook na Instagram

Polisi wakataa kuzungumzia mauaji ya mlanguzi wa dawa

T L