Makala

Kukatwa mguu hakujawa kikwazo kwa mhudumu wa bodaboda

May 22nd, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

IWAPO sehemu moja ya mwili wako unayotumia kufanya kazi itatolewa ama kwa ajali au kwa ugonjwa, utarejea kwa kazi hiyo au utabadili mkondo wa maisha kuwa ombaomba?

Taifa Leo ilikutana na Bw Joseph Simiyu Situma,33, mhudumu wa bodaboda jijini Nairobi anayetumia mguu wa kushoto pekee akiendesha pikipiki yake ili kutafuta riziki.

Bw Situma ambaye ni baba wa watoto watatu alihusika katika ajali ya barabarani miaka miwili iliyopita na kusababisha mguu wake kuondolewa kwa kukatwa.

Bw Situma anasema hali hiyo haimpi muda wa kuombaomba licha ya kuwa ni mlemavu anayehitaji msaada.

“Muhimu ni kujikubali kwanza. Ninakumbuka kuna wakati nilikuwa ninaingia katikati mwa jiji kuombaomba lakini watu wengi wakaniambia nikijikaza, siwezi nikawa ombaomba,” asema Bw Situma.

Anasema kauli za wapitanjia zilimfungua macho na kumpa ujasiri.

Licha ya kwamba wapo wapita njia waliomkejeli, maneno yale yalimpa nguvu na akirudi nyumbani alikuwa akifanya mazoezi ya jinsi ya kutumia pikipiki.

Alianza kwa kusambaza maji kwa wateja wake akitumia pikipiki.

“Tayari nilikwa na ujuzi wa kuendesha pikipiki na nilichokuwa nikitafuta, ni udhibiti na uthabiti ninapobeba maji. Kila asubuhi nilianza kutafuta wateja wa maji,” asema.

Baada ya muda mfupi, alikuwa anaweza kubeba mitungi minane kwa wakati mmoja.

Kila upande niliweka mitungi miwili miwili na juu nikibeba mitungi minne.

Kufaulu kubeba maji kutoka sehemu moja hadi nyingine kulimpa fikra ya kurejea kwenye sekta ya bodaboda.

Kulingana naye, mwanzoni alikuwa na uoga wa kufanya kazi ya kusafirisha wateja kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Bw Joseph Simiyu Situma,33, ambaye ni mhudumu wa bodaboda jijini Nairobi. PICHA | FRIDAH OKACHI

Bw Situma anasema binadamu huwa na mawazo tofauti hivyo hili lilimpa wasiwasi.

“Binadamu wana hisia tofauti na mitungi,” asema.

Kila alipofika kwa kituo cha kubeba wateja siku za mwanzo, aliogopa kunyanyapaliwa na baadhi ya wateja.

Haidhuru, abiria walianza kumzoea kadri siku zilivyosonga.

“Kwa kweli niligundua ningefanya kazi bila kuombaomba,” asema.

Aidha anawashukuru wahudumu wenzake wa bodaboda ambao huelekeza baadhi ya wateja kwake na kuwaaminisha wateja hao kuwa Bw Situma ni mwendeshaji stadi wa pikipiki.

“Wenzangu wamekuwa wenye manufaa mengi sana. Kuna wale wateja ambao huja hapa wanakataa nisiwabebe wakati zamu ni yangu ya kumchukua mteja. Hawa wenzangu huwaaminisha wateja kwamba ninaweza kufanya kazi vizuri,” asema.

Bw Situma ambaye anatumia pikipiki ya kawaida ambayo kwa wakati mwingine mwendeshaji huhitaji kutumia miguu yote miwili, yeye hujipanga kwa ujuzi wake.

“Pikipiki ninayotumia ni ya kawaida. Kila mwendeshaji pikipiki anaweza kuitumia. Uzoefu niliopata wakati wa kuuza maji kwa wateja ndio ulinipa nguvu na maarifa zaidi na ninaweza kuendesha kama mtu yeyote,” asema.

Wakati wa kuongeza na kupunguza spidi, na kuwasha, anatumia ujuzi wake kuhakikisha kuwa anachofanya hakimtatizi.

“Ujuzi wangu na fikra zangu huwa kwenye usukani wa pikipiki na ninafanya ukarabati wa hapa na pale kubadilisha gia na kufinya breki. Ukiangalia pikipiki zote haswa wakati wa msongamano kwenye barabara, mguu wa kushoto ndio hufanya kazi sana,” asema.

Anasema alihusika kwenye ajali mwaka 2022, mhusika wa kusababisha ajali hiyo akitoweka.