KUKU WA KIENYEJI: Mtaji mdogo ila pato ni maradufu
CHRIS ADUNGO na RICHARD MAOSI
UTAFITI unaonyesha kuwa Kenya ina takriban kuku milioni 32 kwa jumla.
Kinachopendeza hata zaidi ni kuwa idadi ya kuku wa kienyeji inazidi ile ya kuku wa gredi; kuku wa kienyeji ni asilimia 75.
Hata hivyo, ipo hatari kuwa kadri siku zinavyosonga, ndivyo kuku wa sampuli hii wanavyoendelea kupungua. Inakisiwa kuwa katika muda wa miaka 10 ijayo, nyuni hao wa kienyeji watakuwa wachache ikilinganishwa na wa gredi licha ya kuwa kuku wa kienyeji wanapendwa zaidi na wateja.
Augustine Kanyanya, mzaliwa wa uliokuwa Mkoa wa Magharibi katika miaka ya 90, ni mmoja wa mifano ya kuigwa miongoni mwa wafugaji wa kuku wa kienyeji.
Alipohitimisha masomo yake ya shule ya upili, alijitosa katika ufugaji wa kuku ili kuzidisha pato almuradi aweze kujitegemea. Alinuia kuwabainishia wasomi kwamba kazi ni kazi bora kukimu maslahi ya kimaisha.
Kwa mtaji mdogo wa Sh2,000 pekee, alianza kujifugia kuku wa kienyeji na kujiboreshea ujuzi hadi ilipofikia mwaka wa 2014.
Aliajiriwa kufanya kazi rasmi ya kufuga kuku wa mayai na nyama kwa wingi katika boma la mfanyabiashara mmoja kwa jina Lawrence Karani aliyemtengea sehemu ndogo ya shamba lake katika eneo la Kiamunyeki, Nakuru.
Baadaye, Bw Karani alimsaidia kuupanua mradi wenyewe hadi Kanyanya alipoanza kujisimamia rasmi kuanzia mwaka wa 2017.
Ni tangu hapo ambapo maisha ya Kanyana yalianza kubadilika. Kuku ni ndege wa nyumbani wenye tabia sawa na kanga wanaofugika katika kila sehemu ya nchi hii.
Katika miaka ya hivi karibuni, ufugaji wa kuku umekuwa kitega-uchumi miongoni mwa wanaomiliki idadi kubwa ya ndege hao. Aghalabu ndege hawa hutegemewa kwa ajili ya nyama na mayai.
Gharama ya kuanzisha mradi wenyewe ni ndogo sana, na hutegemea lengo la mfugaji. Manufaa yake ni tele, huku baadhi ya mashirika ya kiserikali pamoja na ya kibinafsi yakiendelea kujitokeza kuwapiga jeki wafugaji wa kiwango kidogo mfano wa Kanyanya hasa kwa kutoa mikopo ya kuendeshea ufugaji wao.
Kiwango kikubwa cha protini katika nyama ya kuku pamoja na mafuta asilia ni jambo ambalo Kanyanya anatilia mkazo kwamba huwachochea watu kuwa walaji wa kuku anaowafuga.
Wakiwa ndege wenye uwezo mkubwa kuingiliana vyema tena haraka na mazingira kulingana na misimu, kuku hujitegemea pakubwa kujizolea lishe.
Upekee huu labda basi ndiyo sababu kuu inayomwaminisha Kanyanya kuwa ufugaji wa kuku si jambo gumu. Kuku hawahitaji vibanda vya bei ghali; bora tu mkulima ahakikishe kwamba hawapati baridi ambayo huenda ikawa kiini cha magonjwa. Wale wanaotaga mayai hutengewa sehemu salama ya kujilindia mayai dhidi ya joto jingi ama baridi kali kupita kiasi yasije yakaharibika.
Pili, vibanda hujengewa sefu za kuhifadhi mayai yasije yakavunjika au kuanguka, pindi yanapotagwa.
Kuku wa kienyeji na gredi ndio tuliowakuta wamesheheni katika kibanda cha Kanyanya. Kwa sasa anamiliki zaidi ya kuku 700, kila mmoja akiwa na uzani wastani wa kati ya kilo 2-4 baada ya kukomaa. Katika hatua muhimu ya ufugaji, vifaranga wanahitaji kulindwa hadi wafikie wiki sita ndipo waachiliwe kidogo kwa wiki moja hivi kabla ya kutengenezewa viota maalum wanapoanza kutaga mayai.
Huzungushiwa waya au uzio wa kati ya mita 1.5-2.0 ili kuwakinga dhidi ya wanyama hatari au wezi wanaoweza kuwadhuru. Katika msimu wa kutaga mayai, Kanyanya anawashauri wafugaji wenzake waendelee kufanya hivi kwa miezi tisa kabla ya kusitisha utagaji.
Kwa kipindi cha kama wiki 40 hivi, kuku wa Bw Kanyanya wanaweza kutaga kati ya mayai 200-300. Mayai hayo huhifadhiwa katika mazingira ya nyuzi-joto ya kati ya 15.5 na 18.5 na baada ya mwezi mmoja, wanaweza kuangua kupitia mbinu za kiasili (kuotamia) au mbinu za kisasa (kiangulio). Ili kuku wafikishe uzani wa kutosha, lazima mfugaji awape mlo uliochanganyika vyema na wanga, sukari, protini, vitamini na madini mengine muhimu.
Kwa kila kuku ambaye Bw Kanyanya huuza sokoni, yeye huwa na uhakika wa kutia mfukoni angalau Sh600 kwa yule ambaye amekomaa.
Kwa upande mwingine, Bw Kanyanya humuuza jogoo mmoja kwa kiwango cha chini zaidi cha Sh1,000. Mayai ya kienyeji ambayo anayo kwa wingi huwavutia wateja wengi zaidi.
Bei ya kuku wa kienyeji hutegemea miezi ama wiki za ukomavu ambapo wale vifaranga wa wiki moja huuzwa kwa Sh50. Iwapo kuku ana takriban wiki mbili pekee, basi atauzwa sokoni kwa kima cha Sh200, hii ikiwa bei ya kila kifaranga.
Bw Kanyanya huuza yai moja la kieyeji kwa kati ya Sh20 – Sh25 na yai moja la kuku wa gredi kwa kati ya Sh12 – Sh15.
Kulingana naye, gharama ya kuwafuga kuku wa kienyeji ni ndogo sana, ila tija itokanayo na kazi yenyewe ni kubwa mno. Kiasi kikubwa cha kuku anaowafuga ni wa asili, na hii ilichangiwa pakubwa na wateja wake wengi kuafadhalisha kuku na bidhaa za kuku wa aina hiyo.
Makuzi yake ni mepesi na wala hawahitaji kiwango kikubwa cha lishe kwani wakati mwingi wao hujitegemea tu kwa kuchakura kila mahali. Ni mara moja moja tu, hasa msimu wa mvua nyingi, ambapo haja ya kuwanunulia kuku wake nafaka na unga wa punje nyinginezo zenye kiwango kikubwa cha madini muhimu huibuka.
Pili, ili mifupa ya kuku iweze kuwa yenye afya na nguvu, ni lazima mfugaji afanye utafiti wa kutosha kuhusu aina ya kuku anaowafuga. Mbali na kuwanywesha maji mengi kila wakati, ni vyema pia kuwaangalia kila baada ya wiki moja ili kudumisha kiwango cha juu cha usafi pamoja na kuwanywesha dawa endapo atagundua dalili fulani za unyonge au pindi manyoya yao yanapoanza kunyonyoka.
Bw Kanyanya huwauza wale vifaranga wa mwezi mmoja kwa Sh300. Wateja wake wengi ni wafanyabiashara kutoka mjini Nakuru. Anaamini kwamba biashara ya ufugaji wa kuku hivi karibuni itaanza kuendesha uchumi wa mataifa mengi yanayoendelea kukua.