• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
KULEA VIPAJI: Klabu ya Ngoingwa FC

KULEA VIPAJI: Klabu ya Ngoingwa FC

Na LAWRENCE  ONGARO

KLABU ya Ngoingwa FC imejitokeza kama mojawapo ya timu hodari katika mtaa wa Ngoingwa, mjini Thika, katika Kaunti ya Kiambu.

Hata hivyo, kocha wa klabu hiyo, Jeremiah Mutinda, amekuwa mstari wa mbele kuiweka timu hiyo katika mstari wa mbele licha ya changamoto tele wanazopitia.

Vilevile Mutinda yumo mbioni kutafuta wafadhili wa kuipiga jeki timu hiyo ili kuendelea kucheza Ligi ya Kaunti Ndogo ya Thika.

Kocha huyo anasema alipobuni timu hiyo watu wengi walisema hatafaulu kuendesha timu hiyo, lakini leo kijiji hicho kinajivunia kuwa na timu ya vijana ambao wameinua sifa za eneo hilo.

Kocha Mutinda anasema kutokana na jinsi vijana wake wamejipanga, wana uhakika watafanya vyema kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu.

“Nilianzisha klabu hii ili kubadilisha mienendo ya vijana wengi eneo hilo,” anasema na kuongeza hatua hiyo inaungwa mkono tena kwa kauli moja na mashabiki pia wakazi wa eneo la Ngoingwa na vitongoji vyake.

Changamoto gani klabu hiyo inapitia?

“Tatizo letu kubwa linalotukumba ni ukosefu wa wadhamini. Tunawaomba wahisani wajitokeze kuwasaidia vijana angalau waweze kukaza buti kwenye juhudi za kusaka tiketi ya kupandishwa katika Ligi ya Kaunti ya Kiambu msimu ujao wa mwaka 2020.

Kwa wakati huu kocha huyo anajivunia kuwa na kikosi cha wanasoka 22 ambao wamejitolea vilivyo kucheza kwa bidii.

Vijana hao hufanya mazoezi yao katika uwanja wa Ngoingwa kuanzia Jumanne hadi Ijumaa, halafu ifikapo wikendi wanashiriki mechi za Ligi.

Anasema tayari ameweka kikosi cha chipukizi ambao wamejitolea kukabiliana na wapinzani wao kwa vyo vyote vile.

Kikosi kamili cha klabu hiyo ni Elijah Kimani (golikipa), difensi kuna madifenda kama James Ngugi, Gabriel Njuguna, Philip Kilonzo, na Benjamin Makwele.

Kiungo kuna Joseph Macharia, Timothy Mungai, na Patrick Ngige; nao mastraika ni Simon Ng’a ng’ a, Joseph Githongo, na Frederick Thiemba.

Kocha huyo anatoa mwito kwa Kaunti ya Kiambu, kuhakikisha Uwanja wao umejengwa uzio; hasa ukuta ili kutoa usalama wa kutosha kwa wachezaji na mashabiki wao.

Anasema kwa wakati huu wanashirikiana na Wilson Simiyu, ambaye ndiye meneja na wamefanikiwa kuendesha timu licha ya panda shuka nyingi.

Klabu hiyo ilibuniwa miaka mitano iliyopita na anajivunia kikosi cha wachezaji wenye umri kati ya miaka 17 na 20.

Kwenye kampeini za Ligi ya wilaya ya Thika kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016, ilmaliza katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 42.

  • Tags

You can share this post!

MKU, Makerere waingia katika ushirikiano kielimu

ULIMBWENDE: Faida za manjano (turmeric) katika urembo

adminleo