Kumhusu Justin Nthiiri Bundi
Na MWANGI MUIRURI
WAKATI habari za kifo cha aliyekuwa Karani wa Bunge la Kitaifa Justin Nthiiri Bundi zilianza kusambaa nchini Jumamosi iliyopita, ujumbe wa kipekee wa maombolezi nao ulichipuka katika ukurasa wa Facebook wa Mugwe United Sports Football Club.
Hii ni klabu ya mpira wa soka mashinani ya Kaunti ya Tharaka Nithi ambapo katika kijiji cha Kanoro katika Kaunti ndogo ya Chuka Igambang’ombe, Bw Bundi alizaliwa miaka 63 iliyopita.
Ujumbe huo ulisema: “Safiri salama mfadhili wetu. Mchango wako kwetu kama viajana tutaukosa. Jiunge na malaika mbinguni.”
Msemaji wa klabu hiyo na ambaye ni diwani wa wadi ya Mugwe, Denis Mutwiri anasema kuwa Bw Bundi alikuwa kielelezo bora cha mtu wa hadhi katika maisha kujumuika mashinani kufaa vijana bila chambo cha kusaka kura kuwa kishawishi cha matendo ya wema.
“Tulimjua Bundi kama tajiri na mkubwa serikalini lakini aliyekuwa na ubinadamu wa kimsingi wa kujumuika nasi mashinani akitusaidia kujipa afueni ya maisha. Alitupa ufadhili wa kila aina, akasaidia katika kukuza vipaji, kutusaidia kupata kazi na kutupa ushauri wa kimaisha,” akasema Bw Mutwiri katika salamu zake za pole.
Mwekezaji ambaye alizingatia hela zake katika sekta za nyumba na makazi, vipande vya ardhi, bima, hisa na ile ya usalama, marehemu ambaye alikuwa na shahada ya sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi alijiunga na idara za kiutawala baada ya kuhitimu.
Mkongwe wa utumishi wa umma katika utawala wa mikoa, Joseph Kaguthi anamtaja marehemu Bundi kama kielelezo bora cha kujituma katika utumishi.
Anasema si mara moja ambapo Bundi alipewa hongera na Rais Mstaafu Daniel Moi kwa kuzingatia kujituma kwake na uadilifu kazini.
Bw Bundi alihudumia utumishi wa umma katika utawala wa maeneo ya Rift Valley, Nairobi, Kaskazini Mashariki na Magharibi na ambapo Kaguthi anasema kuwa alijiangazia kama mweledi wa kupambana na uhalifu kama vile ujambazi, tohara ya wanawake, ndoa za kulazimisha wasichana wenye umri wa chini na wizi wa mifugo.
Mkuu wa tarafa
Mbunge wa Eldas, Adan Keynan anasema kuwa anamkumbuka Bw Bundi akiwa mkuu wa tarafa katika kijiji chao miongoni mwa ukoo wa Dagodia na ambapo kwa kutambua na kusherehekea juhudi zake za kuleta amani, alipewa ngamia kama zawadi.
Bundi aliaga dunia katika hospitali ya Aga Khan Jijini Nairobi alikokuwa akitibiwa ugonjwa wa saratani.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, alimtaja mwendazake kama mtu wa karibu ambaye alikuwa mshirika mkuu.
“Ni rafiki, mwanafunzi mwenzangu, mtumishi wa umma na pia kiongozi,” akasema Muturi.
Katika shule ya Kang’aru iliyoko katika Kaunti ya Kirinyaga mwaka wa 1976 na 77, wawili hawa walikuwa pamoja katika kidato cha tano na sita na ambapo Muturi akiingia katika taaluma ya uanasheria, Bundi aliingia katika utumishi wa serikali katika idara ya kiusalama.
Anamtaja kuwa mzalendo kamili ambaye hatimaye walipatana tena bungeni Muturi akiwa Spika naye Bundi akiwa karani wa bunge kati ya Oktoba 11, 2012 hadi Machi 21, 2017.
Kando na kuwa karani wa bunge, aliwahi kuhudumu kama msaidizi wa Spika Francis Ole Kaparo na pia katika tume ya ugavi wa rasilimali.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, jina lake liliwasilishwa bungeni ili ateuliwe kama mbunge wa bunge la Afrika Mashariki lakini likaondolewa baadaye na ambapo aliingia ‘mitini’ akisemwa kushughulikia biashara zake na pia huduma mashinani.
Karani wa sasa wa bunge, Michel Rotich Sialai anasema kuwa alimtembelea Bundi katika hospitali masaa machache kabla ya aiage dunia akimtaja kama “shujaa aliyekondolea hali yake macho kiume.”
Wengine ambao wamemuomboleza mwendazake ni gavana wake, Muthomi Njuki akiwa pamoja na mbunge wake, Patrick Ntwiga.
Kwa pamoja, wameahidi kufadhili sherehe ya kukata na shoka ya kumuaga mwendazake, wakisema kuwa ingawa ameondoka kutoka maisha ya uhai, wema wake pamoja na nyoyo alizogusa akiwa hai ni viungo thabiti vya kuendeleza hisia zake katika jamii kwa miaka mingi ijayo.