• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Kumhusu marehemu Jeremiah Gitau Kiereini

Kumhusu marehemu Jeremiah Gitau Kiereini

Na MWANGI MUIRURI

KIFO cha bwanyenye Jeremiah Gitau Kiereini aliyekuwa na umri wa miaka 90 kimeipokonya nchi mwekezaji na pia mtumishi wa umma aliyechangia pakubwa historia ya taifa hili.

Akifahamika vyema kwa kupenda kuvalia suti nyeusi zilizokuwa na mistari ya rangi nyeupe ikipanda na kushuka kimpangilio, ukwasi wake unakadiriwa kuwa katika kiwango cha zaidi ya bilioni 50.

Alikuwa kitindamimba katika familia ya watoto wanne na akaibuka kama kielelezo tosha kuwa inawezekana kijana wa mashinani wa kutoka katika familia ya kawaida sana na kipato kidogo kupata neema ya Mwenyezi Mungu na aishie kuwa ngome na kimbilio kwa wengi wanaosaka kazi, yeye akiwa mwajiri wao.

Akiwa mtumishi wa umma katika idara ya utawala wa mikoa katika enzi ya ukoloni hapa nchini, kuna mahabusu wa harakati hizo ambao walikiri kuwa mwendazake alikuwa afisa mkatili sana.

Mwanahistoria kutoka Amerika, Caroline Elkins katika kitabu chake ‘Britain’s Gulag: The Brutal End of Empire in Kenya’ ambacho kilichapishwa 2005, anathubutu kumuangazia: “Yule Jeremiah Kiereini mkatili ambaye katika kazi yake ya kuhudumia mahabusu wa Maumau, alikuwa akiwatesa si haba.”

Mwaka wa 2015, Kiereini alichapisha kumbukumbu zake za kimaisha na ambapo anakiri kuwa hakuwa mwingi wa huruma katika huduma yake kwa serikali ya kikoloni.

Alitumia fursa hiyo ya uandishi kukanusha kuwa alikuwa mkatili kiasi kinachoasemwa na mahabusu hao wa kikoloni au mwanahistoria huyo wa Amerika, akilalamika kuwa mwanahistoria huyo licha ya kuwa hapa nchini kwa miaka tisa akichunguza kuhusu kitabu hicho chake, hakumsaka ili amhoji ili apate ukweli wa mambo kutoka kwake mwenyewe.

Alihudumu pia kama mkuu wa utumishi wa umma na akastaafu mwaka wa 1984 na akajiunga na sekta ya uwekezaji na ambapo biashara zake alizipa jicho pevu la kuzistawisha hadi kuwa katika kiwango cha sasa ambacho ni kuzalisha ukwasi mtupu.

Akiwa na jina la majazi la ‘Jerry’ miongoni mwa wandani wake, mwendazake pia alihudumu kama mwenyekiti wa kampuni ya East African Breweries na pia kampuni ya CMC Motors.

Jumba

Mkulima hodari wa kahawa, aliripoti kuwa jumba lake la kwanza la kifahari alilijenga akitumia pato la mmea huo ambao kwa sasa ni kilio tupu kwa wakulima na ambapo wengi wanakitupilia mbali wakikitaja kuwa cha utumwa.

Mume wa wake wawili, Kiereini pamoja na Bruce McKenzie ndio walikuwa mashahidi wa urafiki Novemba 1972 katika harusi ya Charles Njonjo ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu akimuoa Margaret Bryson.

Kampuni zingine ambazo zinahifadhi ukwasi wa Kiereini ni pamoja na  African Liaison & Consultant Services Limited, Gambit Holdings Limited, CFC Life Assurance Limited, CFC Financial Services Limited, Heritage A.I.I. Insurance Company Limited, Heritage A.I.I. Insurance Company (Tanzania) Limited, Norfolk Towers Limited, Longonot Place Limited na Unga Group Limited.

Yeye ndiye alikuwa wa kwanza kupiga marufuku ya magari ya serikali isipokuwa tu yale ya kiusalama kutumika usiku na pia akatoa masharti hasi ya wageni katika ikulu baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali ya Daniel Moi mwaka wa 1982.

Alihusishwa na doa la kupunja kampuni ya CMC mwaka wa 2011 akidaiwa kutumia akaunti bandia ya benki lakini akajitetea kwa kiwango kikuu.

Alizaliwa katika kijiji cha Kibichoi kilichoko Kaunti ya Kiambu mwaka wa 1929 na ambapo alisomea katika shule ya msingi ya Kiamwangi kabla ya kutua katika shule za Government African School, Kagumo kati ya1939 na 1945.

Alifululiza hadi shule ya upili Alliance mwaka wa 1945 na mwaka wa 1950 akatoka kutoka taasisi ya Makerere.

Alijiunga na utumishi wa serikali ya kikoloni na ndipo akafadhiliwa kusomea masuala yana aliporejea nchini, aliendelea na huduma ya utawala wa mikoa na akapanda ngazi hadi kuwa mkuu wa utumishi wa umma.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Mtama zao la kutegemewa kuliko mahindi eneo...

SHANGAZI AKUJIBU: Nimempenda msichana lakini anavuta sigara...

adminleo