• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
KUMLINDA MTOTO: Watoto kujiua, suala la malezi au mtindo wa maisha?

KUMLINDA MTOTO: Watoto kujiua, suala la malezi au mtindo wa maisha?

Na LEONARD ONYANGO

JE, wazazi wamelemewa na malezi au jamii ndio inafaa kulaumiwa?

Ama teknolojia ndio imesababisha masaibu haya? Hayo ndio maswali ambayo wengi wanajiuliza kufuatia ongezeko la watoto wanaojitoa uhai kila uchao humu nchini.

Japo hakuna takwimu rasmi za serikali za kuonyesha idadi ya watoto wanaojitoa uhai humu nchini, kumekuwa na ongezeko visa hivi atika miaka ya hivi karibuni.

Mnamo Machi 2019 Wakenya walipigwa na mshangao kufuatia habari za kujinyonga kwa mvulana wa darasa la pili katika eneobunge la Lurambi, Kaunti ya Kakamega.

Kulingana na mama ya mwathiriwa, maiti ya mvulana huyo ilipatikana ikining’inia ndani ya bafu.

Juni 2019 mvulana wa umri wa miaka 12 alijitia kitanzi saa chache baada ya kusherekea siku yake ya kuzaliwa katika Kaunti ya Murang’a.

Wazazi, walimu na hata majirani walimtaja mwendazake kama mtoto mwenye bidii na mchangamfu ambaye hakuonekana kuwa na mzongo wa mawazo.

Mwezi jana, mvulana wa umri wa miaka saba alidaiwa kujinyonga kijijini Kiangwenji, Kaunti ya Kirinyaga kufuatia madai kwamba alinyimwa penseli. Kulingana na familia yake, maiti ya mvulana huyo ilipatikana ikining’inia katika mlingoti wa umeme.

Julai, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika shule ya Upili ya Alara, Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, alijinyonga baada ya kutumwa nyumbani kwenda kuleta karo.

Maiti ya Wycliffe Omondi, 16, ilipatikana ikining’inia katika paa la nyumba ya wazazi wake.

Hivyo ni visa tu vichache ambapo watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wamejitoa uhai katika hali ya kutatanisha mwaka huu.

Wasomi wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kubaini kwa nini watato wanaweza kufikiria kujitoa uhai.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Manchester cha Uingereza mapema 2019 ulibaini kuwa watoto ambao wanahisi kubaguliwa, kutelekezwa, kuteswa na hata kutusiwa mara kwa mara wako katika hatari ya kujinyonga maradufu ikilinganishwa na wenzao ambao hawapitii masaibu hayo.

Watafiti hao hao walisema kuwa watoto wanaodhulumiwa kingono wako katika hatari ya kujitoa uhai mara tatu zaidi ya wenzao ambao hawajawahi kutendewa unyama huo.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Psychological Medicine, ulionyesha kuwa watoto wanaonyanyaswa nyumbani au shuleni wako katika hatari ya kujitoa uhai mara tano zaidi ikilinganishwa na wenzao wanaoishi raha mustarehe.

Utafiti mwingine uliochapishwa katika jarida la American Academy of Child and Adolescent Psychiatry (JAACAP), ulibaini kuwa watoto wanaoteswa na wenzao shuleni au nyumbani wako katika hatari ya kujinyonga mara tatu zaidi.

Mbali na kuteswa, watafiti pia wamebaini sababu nyingine inayoweza kusuka watoto kujitia kitanzi.

Utafiti uliofanywa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha San cha Amerika, Profesa Jean Twenge, ulibaini kuwa watoto kutumia muda mwingi wakitazama filamu kwenye runinga, simu au kompyuta kunachangia katika kuwafanya kuwa na mzongo wa akili hivyo kuanza kuwa na mawazo ya kujitoa uhai.

Kulingana na Prof Twenge, wazazi wanafaa kuhakikisha kuwa watoto wao wanatumia muda mfupi kutazama filamu au kucheza michezo ya kompyuta.

Prof Twenge alihoji watoto 500,000 nchini Amerika na kuchanganua tafiti ambazo zimewahi kufanywa tangu mwaka wa 1991.

Mtafiti huyo alibaini kuwa asilimia 30 ya watoto hao wamewahi kuwa na fikra ya kutaka kujiua na wengine hata wamewahi kujaribu kujitoa uhai.

“Watoto hao waliulizwa nini walichokuwa wakipendelea kufanya kujiburudisha na idadi kubwa ya wale ambao wamewahi kufikiria kujiua walijibu walipenda kutazama filamu kwenye runinga, simu au kompyuta zaidi ya shughuli nyinginezo,” akasema Prof Twenge.

Hata hivyo, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Vermont, Amerika, wanasema kuwa watoto wanapojihusisha na shughuli za michezo, wanapunguza fikra za kutaka kujitoa uhai.

Watafiti hao walihusisha wanafunzi 13,583 wa sekondari na wakabaini kuwa idadi kubwa ya watoto wanaojihusisha na michezo au kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki hawajawahi kuwa na fikra za kutaka kujiua.

Moses Njuguna ambaye ni mzazi wa watoto wawili katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi, analaumu hali ngumu ya uchumi na ongezeko la teknolojia.

“Hali ya uchumi imekuwa ngumu na wazazi wanahangaika mchana na usiku kuwatafutia watoto chakula na mahitaji mengineyo. Lakini wakati wazazi hawapo nyumbani, hawajui wanachofanya watoto wao,” anasema.

Bw Njuguna, hata hivyo, anakiri kuwa baadhi ya wazazi ni wazembe. wanapendelea kuwaletea watoto wao filamu zinazoonyesha fujo na michezo mingineyo ya kompyuta ili wasiwasumbue.

“Ni vigumu pia kuzuia mtoto kucheza na mwenzake kwa jirani. Lakini anapoenda kwa jirani, hujui wanaangalia filamu za aina gani huko,” anasema Bw Njuguna.

Changamoto

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya ubongo, Shibero Akatsa, watoto au vijana hukimbilia kujinyonga kwa sababu hawana uwezo wa kufikiri na kutafuta ufumbuzi wa changamoto wanayopitia.

Bi Akatsa pia asema watoto au vijana hawana uwezo wa kumudu mzongo wa mawazo au presha ya maisha na wengi wao huanza kutumia mihadarati au pombe ili kutuliza mawazo. Lakini mihadarati hiyo huwafanya kuwa na mawazo ya kutaka kujitoa uhai.

“Watoto wanahitaji upendo na wazazi wanafaa kutenga muda mwingi wa kuwa nao. Mtoto anapohisi kupendwa atakuwa huru kufichua masaibu yanayomsumbua moyoni.

“Lakini makosa yanayofanywa na wazazi ni kwamba hawaonyeshi mapenzi kwa watoto wao hivyo hawajui masaibu wanayopitia. Nafahamu mtoto kutoka familia ya kitajiri ambaye alijiua kwa sababu alikuwa na shida ya kuelewa masomo shuleni na wenzake walimkejeli. Wazazi hawakuwepo nyumbani kusikiliza masaibu yake,” anasema.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa vidokezo kadhaa vinavyofaa kufuatwa na wazazi ili kuzuia watoto wao kujitoa uhai;

1. Wasiliana na mtoto mara kwa mara.

2. Msikilize mtoto kwa makini

3. Mtoto anapotoa pendekezo usimzomee, mpe pendekezo mbadala

4. Kosoa mtoto wako kwa upendo si kwa ukali na kumkaripia

5. Mambo unayomweleza mtoto yathibitishe kwa vitendo, si maneno tupu

6. Ruhusu watoto kuelezea fikra zao bila woga

7. Mfahamu mtoto wako vyema. Kwa kufanya hivyo utagundua tabia zisizo za kawaida.

You can share this post!

TEKNOHAMA: Facebook kuondoa ‘like’ kupunguza...

Sababu ya makahaba kuandamana mjini Thika

adminleo