Akili MaliMakala

Kuokoa mazao mabichi kupitia uongezaji thamani

Na SAMMY WAWERU February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KULINGANA na data kutoka Wizara ya Kilimo, Kenya hupoteza karibu asilimia 40 ya mazao mabichi ya shambani kwa sababu ya miundomsingi duni wakati wa mavuno na baada. 

Hali kadhalika, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa linakadiria hasara ya upotevu wa matunda na mboga nchini kuwa kati ya asilimia 30 hadi 50.

Ndizi pekee, Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO) linakadiria zinawakilisha asilimia 20 hadi 30 ya upotevu.

Wambui Kiritu, mwanzilishi Bobo Bakes, hata ingawa biashara yake haijapenyeza mizizi kila kona ya taifa, anajivunia kuokoa mazao mabichi ya kilimo.

Akiwa angali kijana, Wambui anashiriki kwenye mtandao wa kuoka mikate, keki na vitafunwa, ambapo mojawapo ya viungo anavyotumia ni ndizi.

“Ingawa mchango wangu si mkubwa vile, ninajivunia kuwa kati ya wanaoongeza bidhaa za kilimo thamani,” Wambui anasema.

Wambui Kiritu, mwasisi Bobo Bakes akielezea jinsi hutumia ndizi kama kiungo cha kuoka mikate, keki na vitafunwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Ana kiwanda – kwenye nyumba yake katika mtaa wa kifahari wa Kilimani, Nairobi.

Kinachovutia zaidi kwenye safari yake ya uokaji iliyong’oa nanga 2020, ni matumizi ya ndizi zilizoiva kupindukia.

“Ndizi ninazotumia ni zilizoiva kupindukia kwa sababu ni mwororo na zinasaidia kurahisisha shughuli za kukanda unga,” anaelezea.

Ndizi zimesheheni madini kama vile Potassium, Iron na Vitamin, hivyo basi kupiga jeki unga wa ngano unaotumika, pamoja na viungio vingine.

Wambui anakadiria kutumia kati ya kilo 40 na 50 za ndizi kwa mwezi.

“Kiwango hicho ni mamia ya ndizi ambazo zingeishia kuharibika na kuoza,” anasema.

Matumizi ya ndizi kama mojawapo wa viungo vya snaki anazotengeneza, ni hatua ambayo ikikumbatiwa na washirika wa mtandao wa uongezaji thamani itasaidia kupunguza kiwango cha hasara ambacho wakulima na wafanyabiashara hushuhudia.

Si tu kwa ndizi, ila pia kwa aina nyingine ya matunda na mazao yasiyodumu muda mrefu.

Mikate iliyookwa kwa kutumia ndizi zilizoiva kupindukia. PICHA|SAMMY WAWERU